Bukobawadau

BARAZA LA WAFANYAKAZI SEKRETARIETI YA MKOA WA KAGERA LAZINDULIWA RASMI NA KUPITISHA BAJETI YA MKOA MWAKA 2016/2017

Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera yafanya kikao cha Baraza la Wafanyakazi ambacho kilikuwa mahsusi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wake, pili kuzindua rasmi Baraza la Wafanyakazi la Mkoa, na tatu kupitia na rasmu ya maandalizi ya bajeti ya Mkoa kwa mwaka wa fedha 2016/2017

Kikao hicho kilifanyika Februari 11, 2016 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na wajumbe walimchagua Bw. Pius Ngaiza (Afisa Msimamizi wa Fedha Sekretariet ya Mkoa) kuwa Katibu wa Baraza na Bw. Egidius Karatunga (Muuguzi Msaidizi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa)  kuwa Katibu msaidizi ambapo Katibu Tawala wa Mkoa ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Mara baada ya uchaguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella alizindua Baraza hilo la Wafanyakazi kwa kuwakumbusha wajumbe kufanya vikao vya Baraza hilo kama sheria na kanuni zinavyoelekeza ili masuala mbalimabli ya watumishi yaweze kuongelewa na kupatiwa ufumbuzi kwa muda muafaka.
“Kutofanyika kwa vikao vya Baraza la Wafanyakazi kunapelekea kutokuwa na ufanisi wa kazi mahala pa kazi jambo ambalo linapelekea kutokuwepo mawasiliano kati ya mwajiri na watumishi wake, aidha, kunakuwepo usimamizi finyu wa utendaji kazi katika ofisi na kupelekea malalamiko kwa wananchi.” Alistiza Mhe. Mongella.
Katika hatua nyingine Baraza hilo lilipitia na kujadili mapendekezo ya Bajeti na Mpango wa Maendeleo wa Mkoa wa Kagera wa mwaka wa fedha 2016/2017 na kuiboresha bajeti hiyo kulingana na maoni na ushauri kama ambavyo wajumbe waliona inastahili kutokana na idara walizoziwakilisha ambapo Mkoa  unaomba jumla ya shilingi bilioni 287,798,977,509 katika bajeti ya mwaka 2016/2017.
Pamoja na kujadili na kupitisha maandalizi ya bajeti ya Mkoa, Baraza la wafanyakazi pia lina jukumu la kufanya vikao  vya kushirikisha wafanyakazi ili kutatua masuala mbalimbali yanayowahusu kazini kwao, kuishauri Serikali kuboresha maslahi  pamoja na kupandishwa vyeo kwa watumishi.
Katibu wa TUGHE mkoa akitoa nasaha zake wakati wa kufunga kikao hicho aliwakumbusha wajumbe kuwa watetezi wa watumishi kwa kufanya kazi kwa uwajibibikaji mkubwa ili kuondoa malalamiko ya watumishi kazini, pia alisema TUGHE haipo kwa ajiri ya kugombanisha watumishi na waajili wao bali kuwaunganisha ili kuwepo ufanisi wa kazi.
Baraza la Wafanyakazi la Mkoa linajumuisha wajumbe kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, na  Ofisi za Makatibu Tawala wa Wilaya.




Next Post Previous Post
Bukobawadau