Bukobawadau

WANANCHI KAGERA WAASWA KUACHA KUTUMIA VISHOKA KATIKA KUTAFUTA HUDUMA YA HAKI MAHAKAMNI – JAJI MWANGESISiku ya Sheria nchini Mkoani Kagera imeadhimishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ambapo wananchi kama wadau muhimu wa Mahakama wameaswa kuepukana na vishoka wa sheria katika kutafuta haki yao Mahakamani  na kutumia wataalam wa sheria kupata haki isiyo na mashaka ya kisheria.
Rai hiyo ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba  Sivangilwa Mwangesi alipokuwa akihutubia wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini Mkoani Kagera Februari 4, 2016 katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
 Jaji Mfawidhi Mwangesi  alisema kuwa madhumuni ya kuadhimisha Siku ya Sheria ni kufungua mwaka mpya wa Kimahakama ambapo shughuli zote za Mahakama huanza rasmi kwa mwaka husika, Pili ni kuwaombea dua wale wote wanaofanya kazi za Kimahakama ili watekeleze majukumu yao ipasavyo, na Nne ni kuelimisha wananchi juu ya kaulimbiu ya mwaka husika.

Kaulimbiu ya mwaka huu 2016 inasema, “Huduma ya Haki Kumlenga Mwananchi ni Wajibu wa Mahakama na Wadau”. Jaji Mfawidhi Mwangesi akifafanua kaulimbiu hiyo alisema kuwa mchakato wa kutoa haki unahusisha  kufungua mashauri Mahakamani, kuyasikiliza, kuyatolea hukumu na mwisho hukumu hiyo kutekelezwa ambapo mchakato huo huwahusisha  wadau wote wa Mahakama. 
Jaji Mfawidhi Mwangesi alitoa wito kwa wananchi kuiamini Mahakama na kuacha kutumia vishoka wa sheria katika kutafuta huduma ya haki Mahakamani bali watumie Mawakili wenye weledi mzuri katika sheria ili kupata haki. Aidha, alisema Mahakama kwa sasa imejipanga kutoa huduma ya haki kulingana na sheria kwa kila mwananchi bila kujali uwezo wake wa kifedha ilimradi sheria ifuatwe.
Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali Mkoani Kagera Hashim Ngole katika maadhimisho hayo alisema Mahakama ina wajibu wa kuijisikia kila mara kutoa huduma ya haki kwa wananchi wake, Pili Mahakimu wana wajibu wa kutoa dhamana kwa watuhumiwa kulingana na sheria isemavyo, Tatu Mahakama kuzingatia sheria wakati wa kutoa huduma ya haki kwa wananchi, na Nne Mahakama inaowajibu wa kutoa huduma ya haki bila kufungamana na upande wowote.
 Bw. Ngole akiwataja wadau wa Mahakama na majukumu yake alisema, Mdau wa kwanza wa Mahakama ni Ofisi ya Mwanansheria Mkuu wa Serikali mwenye jukumu la kufungua na kuendesha mashauri ya wananchi kwa weledi Mahakamani, Kuhakikisha mashahidi wanahudhuria Mahakamani, Kupokea na  kujibu malalamiko ya wananchi kuhusu masuala ya kisheria.
Wadau wengine ni Jeshi la Polisi na wajibu wao ni kupeleleza mashauri kujua ukweli wa makosa, Magereza wajibu wao ni kuhakikisha wafungwa wanahudhuria Mahakamani bila kukosa, Mawakili kuhakikisha wanasimamia kesi za wananchi kwa weledi ili haki ipatikane, Bunge wajibu wake ni kutunga sheria ambazo siyo kandamizi na mwisho ni Wananchi wanaotakiwa kutoa ushahidi wenye ukweli Mahakamani.
Naye Mkuu Mkoa wa Kagera ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya sheria akiwasalimia wananchi aliipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kwa kufanya vizuri kwa mwaka 2015 kwa kuvuka malengo ya kutoa haki na kushughulikia mashauri mengi yaliyokuwa yamekwama aidha, Mahakama hiyo kuwa ya kwanza kati ya mikoa mitatu iliyofanya vizuri nchini.
 Aidha, Mhe Mongella alitoa wito kwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kuhakikisha inaongeza nguvu kwa Mahakama za chini hasa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo ili kutoa huduma ya haki kwa wananchi walio wengi zaidi ili kupunguza malalamiko kutoka kwa kwenye jamii.
Mikakati ya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kwa Mwaka 2016
Kuanzisha Dawati la Malalamiko ili kupokea malalamiko ya wananchi na kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria pia kutoa majawabu ya malalamiko yao.

Mahakama Kuu kuondoa mashauri yote Mahakamani ambayo yamekaa kwa muda wa miaka mitano, Mahakama ya Mkoa kuondoa mashauri yote yaliyokaa miaka miwili na Mahakama za Mwanzo kuhakikisha mashauri yote yaliyokaa mwaka mmoja yanaondolewa na kubaki na mashauri ya chini ya mwaka mmoja.
Majaji na Mahakimu kutembelea Magereza ili kuondoa kesi zenye mikwamo za wafungwa ili kupunguza msongamano katika Magereza. Aidha, mashauri ya jamii au yenye maslahi mapana katika jamii kuhakikisha yanaondolewa au kushughulikiwa haraka  ili kupunguza misuguano katika jamii mfano kesi za uchaguzi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau