Bukobawadau

KAULI YA DK. H.G. MWAKYEMBE ALIYOITOA KWA WAANDISHI WA HABARI MJINIDODOMA LEO


Jumatatu ya wiki iliyopita, yaani tarehe 13 Juni, 2016, Gazeti la Kiswahili la kila wiki liitwalo Dira ya Mtanzania lilichapisha ukurasa wa mbele na wa pili kwa maandishi makubwa meusi na mekundu taarifa iliyosema: "Mwakyembe atuhumiwa kutapeli Bil.2: kupandishwa kizimbani wakati wowote."
Pamoja na kwamba hii si mara yangu ya kwanza kutungiwa tuhuma na baadhi ya vyombo vyetu vya habari kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kisiasa, napenda nikiri mbele yenu kuwa sijawahi, toka niingie katika siasa miaka kadhaa iliyopita, kushuhudia upotoshaji mkubwa na wa makusudi mazima, uongo na uzushi uliopitiliza na chuki binafsi iliyo bayana kama ambavyo gazeti la DIRA tar. 13 mwezi huu lilivyodhihirisha. 

Ukisoma taarifa karibu zote katika gazeti hili, unaona waziwazi umakini na weledi katika uandishi wa habari unakosekana! Hata jina tu la Wizara yangu linaandikwa wanavyotaka, umakini tunaouenzi tuliosomea taaluma hii haupo kabisa!

Dunia iliambiwa wiki iliyopita tena bila wasiwasi kabisa (upande wa gazeti la DIRA) kuwa: Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania ni tapeli na anapandishwa kizimbani, wakati wowote. Ukurasa wa pili wanafafanua kuwa: ati nimejipatia mali isivyo halali au wizi wa kuaminiwa kinyume na sheria za Tanzania. Makosa yaliyonukuliwa na gazeti hili ni makosa ya jinai, hivyo nawategemea DIRA (Msama na wenzake) kwamba:
- wana nakala ya charge sheet, hati ya makosa;
- wameiona cause list, orodha au ratiba ya kesi za jinai kujua lini, maana wanasema wakati wowote Waziri wa Katiba na Sheria anapandishwa kizimbani;
- wanazo taarifa za upelelezi zikithibitisha madai yao, hivyo jalada la kesi hii iliyobebewa bango na DIRA, lipo polisi na wameliona!;
- kwa kuwa hakuna kesi ya jinai isiyo na mlalamikaji (complainant), hivyo nina matumaini DIRA wanamjua mlalamikaji katika kesi hii na wanakijua kituo cha polisi kilichochukua maelezo ya mlalamikiwa na kuanza kuyafanyiakazi;
- kwa kuwa hii ni kesi ya jinai, hivyo kesi ya Jamhuri ambayo huwezi tu ukapelekwa mahakamani na polisi bila wewe kuhojiwa; hivyo nina uhakika DIRA wanajua tarehe niliyohojiwa na Wapelelezi wa Polisi kuhusu kesi hii ya DIRA, nk nk

Nina taarifa kuwa wameuza sana magazeti; naambiwa print order yao imeongezeka na kwamba taarifa yao imesambaa kwenye mitandao ya jamii, hivyo dunia nzima inajua mimi nina tuhuma za wizi, za utapeli!

Vivyohivyo Jumatatu ya wiki hii, yaani jana tar. 20 Juni, DIRA wameona waendeleze biashara hii kwa kuuthibitishia ulimwengu kuwa MWAKYEMBE KWELI NI TAPELI: ushahidi wao mkubwa kuna barua iliyowahi kuandikwa na kampuni ya Power Pool mwaka 2010 na mimi kutumiwa nakala kwa e-mail wanayodai ni yangu. Kwa busara za gazeti hili, huo ni ushahidi tosha kuwa mimi ni Tapeli.

Naomba nikiri kuwa sijawahi kushuhudia kiwango cha juu cha kuropoka bila kujali, kubwabwaja bila "staha na miiko ya uandishi wa habari" kama nilivyoshuhudia kwa gazeti hili la DIRA. Viongozi tukiendelea kupuuzia na kusema: ah, wananchi watabaini wenyewe kuwa huu ni uongo, BASI TUTAJENGA msingi hatarishi katika mustakabali wa Taifa letu.

Si mimi tu niliyechomekewa jambo na gazeti hili: wapo Marais wastaafu tunaowaheshimu sana. Wiki iliyopita uk wa 4 wa gazeti hili, kikosi chetu cha jeshi huko Kisarawe kilielezewa kama kikundi cha wahuni hivi kinachopiga wananchi hovyohovyo, kinapiga risasi za moto hovyohovyo hadi kumpiga mwananchi moja kiunoni nk.

Wameona hiyo haitoshi, wiki hii wamekuja na taarifa ya kulidhalilisha zaidi jeshi letu lenye rekodi iliyotukuka duniani, kuwa kifaru chake cha kivita ati kimeibwa! Huku ni kukosa uzalendo, ni kulitia doa jeshi letu bila sababu kama siyo za kimamkuki. Wiki ijayo huenda wakadai kuwa kifaru hicho sasa kinatumika kama dala dala vijijini! Mzaha umeaidi: Hiyo ndiyo DIRA!

Nimewaita kuwataarifu kuwa tunakamilisha nyaraka za shauri la kashfa na kuwadai wote wahusika fidia kubwa itakayotoa fundisho. Tutafungua kesi hii Mahakama Kuu ya Tanzania, tutawapa taarifa kila tunavyo-endelea. Bado tunaangalia impact na kuhusika kwa vyombo vikubwa vya habari kama ITV na STAR TV kutangaza taarifa za magazeti tata bila uangalifu ili na wao tuwahusishe katika kesi hii. 

Kesi hii, nina uhakika, itajenga msingi imara wa wajibu na uhuru wa vyombo vya habari Tanzania kwa muda mrefu ujao.

Ahsanteni kwa kunisikiliza!

--------       -----------    -------
Next Post Previous Post
Bukobawadau