Bukobawadau

WAKUU WA WILAYA SABA WA MKOA WA KAGERA WAAPISHWA RASMI

Wakuu wa Wilaya  wateule saba wa Wilaya za Mkoa wa Kagera wameapishwa rasmi leo Julai 4, 2016 na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Wakuu hao saba wa Wilaya waliapa mbele ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu kwa kula viapo vitatu ambavyo ni Kiapo cha Utii, Kiapo cha Utumishi na Kiapo cha kutunza siri za Serikali. Aidha, tayari wamekula Kiapo cha Maadili mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli tarehe 29/06/2016 ikiwa ni pamoja na kupokea maelekezo ya utekelezaji wa shughuli zao.
Mara baada ya kula viapo vyao Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu aliwapongeza kwa kuteuliwa kuwa Wakuu wa Wilaya wapya wa wilaya za Mkoa wa Kagera pia akawaasa kufanya kazi zao kwa kuzingatia Kauli mbiu ya Mhe. Rais Magufuli  ya “Hapa Kazi tu”
“Nawaasa kuwatumikia wananchi kwa nguvu sana kwani hali za wananchi katika maeneo yenu mliopangiwa si nzuri, lakini nawataka kufanya kazi kwa kutenda haki bila kuwaonea  na mtende kazi bila woga.” Aliwaasa Mhe. Kijuu
Aidha Mhe. Kijuu aliwapongeza wliokuwa wa Wilaya za Mkoa wa Kagera ambao wamestaafu na kuwatakia maisha mema huko waendako pia aliwashukuru kwa kazi kubwa  waliyoifanya wakiwa Wakuu wa Wilaya kwani walipigana kwa nguvu kusukuma maendeleo ya wananchi mbele.
Wakuu wa Wilaya saba Walioapishwa rasmi leo Julai 4, 2016 ni Mhe. Deodatus Lucas Kinawilo Mkuu wa Wilaya ya Bukoba wa 19 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 1961. Mhe. Godfrey Ayub Mheluka Mkuu wa Wilaya ya Karagwe wa 20 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 1961. Mhe. Lt.Col. Denis Filangali Mwila Mkuu wa Wilaya ya Missenyi wa 4 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 2007.

Wengine ni Mhe. Col. Mstaafu Shaban Ilangu Lissu Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa wa 3 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 2012. Mhe. Saada Ibrahim Malunde Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo wa 22 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 1961. Mhe. Lt.Col. Michael Mangwela Mntenjele Mkuu wa Wilaya ya Ngara wa 19 tangu Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 1962.

Wa mwisho ni Mhe. Mhandisi Richard Henry Ruyango Mkuu wa Wilaya ya Muleba wa 15 tangu Wilaya hiyo ilipoanzishwa mwaka 1975. Aidha mara baada ya hafla fupi ya kuapishwa Wakuu hao wa Wilaya waliondoka na kuelekea katika vituo vyao vya kazi kuanza kutekeleza majukumu yao ya kazi.
 Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Mhandisi Richard Henry Ruyango.
 Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Mhe. Saada Ibrahim Malunde
 Mkuu wa Wilaya ya Ngara Mhe. Lt.Col.Michael Mangwela Mntenjele
 Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Deodatus Lucas Kinawilo.
 Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Godfrey Ayub  Mheluka
 Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Col.(Mst.) Shaban Ilangu Lissu
 Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Lt.Col.Denis Filangali Mwila
Next Post Previous Post
Bukobawadau