Bukobawadau

WAZIRI UMMY MWALIMU APIGA MARUFUKU HOSPITALI NA VITUO VYA AFYA VYA SERIKALI KUTOA VILAINISHI VYA KUSAIDIA KUFANYA MAPENZI YA JINSIA MOJA

Mhe. Waziri YUmmy Mwalimu Akizindua Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera
Maneno yaliondikwa katika kibao cha uzinduzi yakisomwa.
Mbunge wa Bukoba Mjini Mhe Lwakatare Akitoa Neno Mbele ya Waziri Ummy Mwalimu
 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Salum M. Kijuu Akitoa Taarifa kwa  Mhe. Waziri Ummy Mwalim
 Mhe. Ummy Mwalimu Akiongea na Wadau wa Afya Katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera
 Picha ya Pamoja Waziri Ummy Mwalimu na Wenyeji wake
 Waziri Ummy Mwalimu Akikifurahia Kichanga
 Waziri Ummy Mwalimu Akimpakata Mtoto Mchanga Katika Wodi Mpya Iliyozinduliwa
 Waziri Ummy Mwalimu Akimpakata Mtoto Mchanga Katika Wodi Mpya Iliyozinduliwa
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe, Ummy Mwalimu amepiga marufuku Hospitali na vituo vyote vya afya vya Serikali kuacha mara moja kugawa  au kutoa mafuta (vilainishi) vya kufanya tendo la ndoa kwa  watu wa jinsia moja hasa wanaume .
Waziri Ummy  Mwalimu ametoa msimamo huo wa Serikali akiwa Mkoani Kagera  leo tarehe 15.07.2016 mara baada ya kuzindua wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera iliyokarabatiwa na kupanuliwa  kwa msaada wa shirika la USAID wakati akiongea na wadau mbalimbali wa afya katika viwanja vya Hospitali hiyo.
“Nawashukuru sana USAID kwa msaada wenu ambao mmekuwa mkiutoa kwa Serikali yetu ya Tanzania lakini naomba kuweka mambo sawa kuwa Serikali haipo tayari kuruhusu ugawaji wa vilainishi vya kusaidia kufanya mapenzi ya jinsia moja katika vituo vyetu vya kutolea huduma vya Serikali, nasema wazi  kuwa hatutaruhusu kabisa na nasema wazi hata viongozi wa dini wako hapa wataniunga mkono.” Alikemea Waziri Ummy.
Aidha, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Salim M. Kijuu kuhakikisha wafadhili wote wanaokuja Mkoani Kagera kutoa misaada akae nao na kusoma makubaliano au mikataba yao vizuri na kuhakikisha kuwa  isiwe na mashariti ambayo yanalenga kulazimisha masuala kama hayo katika jamii.
Pamoja na  agizo hilo Waziri Mwalimu aliwapongeza USAID kwa kufadhili mradi wa Jhpiego wa Afya ya Mama na Mtoto (MCSP) ambao umewezesha utolewaji wa mafunzi na kujengewa uwezo wahudumu wa afya wanaotoa huduma kwa kina mama, watoto wachanga, na watoto chini ya miaka mitano ikijumuisha wale wanaofanya kazi katika hospitali hiyo.

Ukarabati na upanuzi wa wodi ya wazazi ulianza mwezi Oktoba mwaka jana na kukamilika mwezi Machi mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Jhpiego, Dkt. Leslie Mancuso. Upanuzi wa jengo hilo umewezesha ongezeko la vitanga kwa ajili ya kulaza akina mama wajawazito na wale waliojifungua na ambao wanahitaji uangalizi.

Upanuzi huo umeongeza idadi ya vitanda kutoka 28 hadi 66 na pia kuongeza vituo vya wauguzi katika wodi hiyo ya wazazi pamoja na vyoo. Jumla ya gharama zilizotumika ni jumla ya Tshs. 136,532,166.92 (Milioni mia moja na thelathini na sita, laki tano na thelathini na mbili elfu, mia moja sitini na sita na senti tisini na mbili).

Waziri Ummy Mwalimu kabla ya kuzindua wodi ya wazazi aliongea na wadau mbalimbali wa afya katika Mkoa wa Kagera kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa kutoka kwa Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu na kuupongeza Mkoa kwa Juhudi unazozifanya katika kuboresha afya za wananchi wa Kagera.
Waziri Ummy alisema, anaupongeza Mkoa wa Kagera kwa kutoa chanjo kwa watoto wadogo na kuvuka asilimia ya kitaifa ambayo ni 93% lakini Kagera imefikia asilimia 103%. Pili wanawake wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya Kagera ni asilimia 83% wakati kitaifa ni asilimia 52%. Tatu ni Mkoa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito hadi kufikia vifo 70 tu kwa mwaka wakati kitaifa ni vifo 400 pia kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Katika utatuzi wa changamoto ya watumishi wa afya Waziri Ummy Mwalimu alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 tayari Serkali imewaruhusu kuajili watumishi katika kada mbalimbali za  afya 10,000 na kati ya hao amehaidi kutoa kipaumbele kwa Mkoa wa Kagera ili kupunguza tatizo la watumishi.
Pia Waziri Ummy ameziagiza Hospitali teule za Wilaya za Mkoa wa Kagera kuwa makini kutokana na watumishi hewa kwani kati ya watumishi hewa 12,000 waliopatikana nchini 4,000 wanatoka katika Hospitali Teule za Wilaya. Aidha Waziri huyo wa afya alihaidi kuwa kwa watumishi wenye sifa ambao walikuwa katika hospitali hizo Serikali itaendelea kuwaajili na alitoa mfano katika Mkoa wa Kagera kuwa kati ya watumishi 81 watumishi 48 wanazo sifa na Seriakli itaendelea kuwaajili.
Katika kuunga mkono juhudi za mkoa wa Kagera Waziri Ummy alihaidi kutoa vitanda 20 na magodoro 20 vinavyopelea katika Wodi ya wazazi. Pia alitembelea Hospitali Teule ya Wilaya ya Muleba  Rubya na anatarajia kukamilisha ziara yake Tarehe 16.07.2016 katika Wilaya ya Bukoba kwa kutembelea Kituo cha kulelea Wazee Kiilima.


Next Post Previous Post
Bukobawadau