Bukobawadau

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA KAGERA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU WIKI YA UNYONYESHAJI KITAIFA MKOANI KAGERA TAREHE 04 AGOSTI, 2O16

Ndugu Waandishi wa Habari, Wiki ya Agosti 1 hadi 7, Tanzania huungana na nchi nyingine ulimwenguni kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama Duniani. Maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika tangu mwaka 1992 kufuatia Azimio la Innocent (nchini Italia) ambalo linasisitiza umuhimu wa kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji na ulishaji bora wa watoto. Wiki ya Unyonyeshaji inatukumbusha kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto na kuendelea kunyonyeshwa mpaka umri wa miaka miwili au zaidi. Aidha, Wiki ya unyonyeshaji, mwaka huu 2016 inaadhimishwa Kitaifa Mkoani kwetu Kagera. Ndugu Waandishi wa Habari, Kauli mbiu ya mwaka huu 2016, ni “UNYONYESHAJI WA MAZIWA YA MAMA: MSINGI KWA MAENDELEO ENDELEVU.” 
 Tunaelewa wazi kuwa pamoja na maendeleo ambayo Mkoa wetu umekuwa ukiyapata katika maeneo mbalimbali, bado utapiamlo umeendelea kuathiri jamii hususani katika nyanja za afya,elimu na uchumi; hivyo kusababisha kasi ya kupungua kwa umaskini kutoridhisha. Lishe duni si tu inaathiri maendeleo ya mtoto lakini pia inaathiri ukuaji wake kimwili na kiakili hatimaye kuathiri mchango wake katika maendeleo ya Taifa katika kipindi chote cha uhai wake.
Ndugu Waandishi wa Habari, Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama ina umuhimu mkubwa sana kwa Mkoa wetu ukizingatia kuwa takribani asilimia 52 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Mkoa wetu, wamedumaa. Udumavu huu unatokana na lishe duni waliyoipata watoto hawa tangu wakiwa wadogo ikiwemo suala zima la unyonyeshaji. Lazima tuungane wana Kagera kubadilisha hali hii; Mkoa wetu ni kati ya Mikoa yenye chakula cha kutosha na fursa nyingi, hivyo ni lazima tuungane kuondoa huu udumavu kwa watoto.
 Sababu kubwa ya utapiamlo huu kwa watoto ni ulishaji usio sahihi ambao huchangiwa na majukumu mengi yanayomkabili mama na hivyo kukosa muda wa kutosha wa kumtunza mtoto. Ni dhahiri kuwa mchango wa mwanamke katika familia, ajira na uzalishaji kwa ujumla ni mkubwa hivyo ni muhimu kuwatia moyo na kuwasaidia wanawake ili waweze kutimiza majukumu ya uzalishaji na utunzaji familia kwa ukamilifu.
Ndugu Waandishi wa Habari, Nasistiza Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini ya mwaka 2004 kuzingatiwa hasa katika mkoa wetu ili kumruhusu mama mwajiriwa anayenyonyesha apewe ruhusa ya masaa mawili kila siku ili akamnyonyeshe mtoto wake, pia mama aliyejifungua mtoto mmoja kupewa likizo ya uzazi ya siku 84 kama amejifungua mtoto mmoja na siku 100 kwa watoto zaidi ya mmoja. Pia baba kupewa likizo ya siku 3 ndani ya wiki moja aliyojifungua mama ili kutoa huduma kwa mama. 
 Aidha sheria hiyo inakataza mama aliye ajiriwa na ambaye ananyonyesha au mjamzito kufanya kazi ngumu au za hatari kwa afya yake au ya mtoto wake. Kwasababu hii, ninatoa wito kwa Taasisi zisizo za Kiserikali, Taasisi za Kijamii na za Kidini, jamii na familia kwa ujumla kuwasaidia wanawake ambao hawapo kwenye ajira rasmi ili waweze kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Ushauri) Mtoto anyonyeshwe ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa. Pia mtoto anyonyeshwe maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo. Uji, ugali, ndizi, maziwa ya kopo au ng'ombe, havitakiwi kwa mtoto mwenye umri chini ya miezi sita; Mwili wa mtoto wa umri huu hauna uwezo wa kuvitumia, hivyo mtoto akipewa vyakula hivi hujaza tumbo tu na kumfanya mtoto kujisikia ameshiba na kumzuia kunyonya aidha, mtoto anyonye mara kwa mara kadiri anavyohitaji.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Umuhimu wa Maziwa ya mama) Kunyonyesha maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto ndio njia bora na salama ya kumpatia virutubishi vyote muhimu kwa ukuaji na maendeleo yake. Maziwa ya mama yana sifa ya kipekee ya kuwa na kinga ambazo humkinga mtoto dhidi ya magonjwa hivyo kuchangia katika kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano. Unyonyeshaji sahihi wa maziwa ya mama katika miezi sita ya mwanzo pia huweza kutumika kama njia ya uzazi wa mpango. Tendo la kunyonyesha pia linajenga mahusiano kati ya mama na mtoto wake. Mtoto anapofikia umri miezi sita, anapaswa kuanzishiwa vyakula vya nyongeza, lakini aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama mpaka atimize miaka miwili au zaidi.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Mikakati) ili kufanikisha unonyeshaji jamii inashauriwa kutekeleza mikakati ifutayo; Kuanzisha na kuendeleza vikundi vya kusaidia masuala ya unyonyeshaji ambavyo vitawashirikisha baba au wanaume.
Kuhakikisha kuwa vituo vya afya, maduka ya dawa na maduka ya bidhaa mbalimbali yanatekeleza kanuni inayodhibiti uuzaji na usambazaji wa maziwa na vyakula vya watoto.
Kuwaunganisha vijana wa kike na wa kiume ili waweze kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kuboresha unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Kuhakikisha kuwa vituo vyote vinavyotoa huduma ya afya vinatekeleza vidokezo kumi vya kufanikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama na hivyo kuwa Rafiki wa Mtoto. Nawaombeni wananchi kabla hamjaondoka hakikisheni mnapitia kwenye mabanda yetu hapa chini kuelekezwa juu ya vidokezo hivyo.
Ndugu Waandishi wa Habari, (Wito) Serikali inatambua kuwa bado zipo changamoto nyingi katika kukabiliana na utapiamlo hapa Mkoani mwetu. Pengine, changamoto kubwa kuliko zote ni ile ya uelewa mdogo wa masuala ya lishe katika jamii ikiwemo unyonyeshaji, kuanzia ngazi ya familia hadi kwa watendaji na viongozi wa Serikali. Uelewa mdogo kuhusu masuala ya lishe umesababisha masuala ya lishe kutopewa kipaumbele katika jamii ambako ndiko waliko watoto na wanawake wengi wanaohitaji zaidi huduma bora za lishe.
Nipende kutoa wito kwenu Wanahabari kutumia ujuzi wenu na vyombo vyenu vya Habari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya kuielimisha jamii hasa katika Mkoa wetu wa Kagera juu ya kukabiliana na utapiamlo na umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kama inavyoshauriwa na wataalamu wetu wa lishe ili tuwe na kizazi cha watoto wenye afya zilizoimarika.
Imetolewa na; Sylvester Raphael, Afisa Habari,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
KAGERA.
Next Post Previous Post
Bukobawadau