SERIKALI YAANZA KUCHUKUA HATUA ZA AWALI ZA KUREJESHA MIUMDOMBINU YA SHULE MBILI ZILIZOHARIBIWA VIBAYA NA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA
Serikali kupitia Kamati ya Maafa ya Mkoa ikishirikiana na Idara
ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu imeanza kuchukua hatua za
kurejesha miundombinu ya Shule za Sekondari Ihungo na Nyakato kwa kuanza kubomoa majengo
yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera Septemba 10,
2016.
Hatua za kuanza kubomoa majengo
ya shule hizo zimeanza kuchukuliwa leo
tarehe 20.09.2016 baada ya Kamatti ya Maafa kupiga hatua kubwa katika
kukabirina na janga la tetemeko kwa kutoa misaada mbalimbali kama huduma za
afya kwa majeruhi, huduma za mahema na matrubali pamoja na chakula ili wahanga
waweze kujihifadhi walipoteza nyumba zao au nyumba hizo kuwa hatarishi.
Katika kuhakikisha miundombinu ya
shule za Ihungo na Nyakato inarejea katika hali yake ya awali Serikali kuu
imeamua kusimika mzizi mkoani hapa kwa
Mawaziri watatu wa Serikali kuamua
kuungana na Kamati ya maafa kuhakiksha urejeshwaji wa miundombinu hiyo unarejea
na wanafunzi wanarejea katika shule hizo
ili kuendelea na masomo yao.
Mawaziri hao ni Waziri wa Elimu,
Sayansi Teknolojia na Ufundi, Profesa
Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mhe. George Simbachawene
na Mhe. Jenester Muhagamma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu.
Akiongea na Waandishi wa Habari
katika Sekondari ya Ihungo iliyoharibiwa kabisa na tetemeko la ardhi Waziri
Muhagama alisema kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za kubomoa na
kusafisha majengo yaliyoharibiwa ili ujenzi
uanze mara moja baada ya Kamati ya Maafa kuwa imefanya kazi kubwa ya
kukabiliana na athari za tetemeko kwa wananchi .
Katika kukabiliana na janga
lolote kuna hatua tatu mhimu, hatua ya kwanza ni kuzuia na katika hatua hiyo hulenga kupunguza athari
za janga. Hatua ya pili ni kukabiliana na athari wakati wa janga ambapo Kamati
ya Maafa ilivyofanya wakati wa tetemeko. Hatua ya Mwisho ni kurejesha miundombinu
iliyoharibiwa na janga husika .
Akifafanua hatua hizo katika eneo
la Shule ya Sekondari Ihungo Mkurugenzi wa Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brigedia Jenerali Mbazi Msuya alisema kuwa Serikali
imeanza hatua ya kurejesha miundombinu huku ikiendelea kutoa misaada ya maafa.
Aidha alitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuanza kurejesha miundombinu
yao kama Serikali ilivyoanza kufanya.
Katika kurejesha miundombinu
iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi Kamati
ya Maafa imezipa kipaumbele shule mbili za Sekondari Ihungo na Nyakato kwasababu shule hizo
ziliharibiwa sana na kupelekea kufungwa baada ya kuonekana kuwa majengo yke
hayafai kutumika. Aidha, majengo yote ya umma na Serikali yatarejeshwa kwa
utaratibu ili kurudisha hali iliyokuwepo awali.
Tetemeko la ardhi lilitokea
Mkoani Kagera Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo bvya wananchi 17, Majeruhi
440 na hadi sasa wamebakia majeruhi 17 ambao wanaendelea na matibabu katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa .
Pia tetemeko hilo lilisababisha nyumba 2,072 kuanguka, Nyumba zenye
uharibifu hatarishi 14,595. Nyumba zenye uharibifu mdogo 9,471 (Jumla ya nyumba zilizoanguka na zilizopata
uharibifu hatarishi ni 16,667). Aidha, wananchi walioathirika na kuhitaji misaada
ili waweze kurudi katika mfumo wa kawaida wa maisha yao ni 126,315.