Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA AZINDUA RASMI MAZOEZI YA KUIMARISHA MWILI NA AFYA KWA WATUMISHI WA UMMA NA WANANCHI WA MKOA WAKE

Na: Sylvester R, na Kepha Elias
Mkoa wa Kagera umezindua rasmi leo Novemba 5, 2016 mazoezi ya viungo kwa watumishi wa umma, Taasisi na Idara za Serikali na zisizokuwa za Serikali pamoja na wananchi wote ili kuimarisha miili, afya na akili kwa lengo la kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali za utoaji huduma na uzalishaji wa kujiongezea kipato.

Mazoezi hayo yamezinduliwa saa 12:30 asubuhi na Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu ambaye aliwaongoza watumishi pamoja na wananchi katika mazoezi hayo ambapo alianza na mazoezi mepesi ya kupasha mwili na baadaye aliongoza mazoezi ya matembezi ya kilometa nne.
Akizindua mazoezi hayo Mhe. Kijuu aliwaeleza washiriki wa mazoezi na wanamichezo zaidi ya 293 kuwa, kufanya mazoezi kunapunguza matatizo mengi ikiwa ni pamoja na kupunguza mafuta mwilini, kuondoa magonjwa nyemelezi na kuongeza utimamu wa akili. Aidha, asilimia 47% ya watu wanaofanya mazoezi duniani kote yanapunguza vifo vinavyotokana na mashinikizo ya damu.
Mhe. Kijuu pia alisema kuwa mazoezi ya pamoja yatakuwa yanafanyika kila Jumamosi ya kila wiki na washiriki wakizoea mazoezi hayo yatakuwa yanafanyika mara mbili kwa wiki. Mhe Kijuu alisistiza kuwa kijamii na kisaikolojia mazoezi ya pamoja yanasaidia katika kutengeneza mahusiano mazuri miongoni mwa watu kufahamiana pia kuondoa msongo wa mawazo.
Aidha, Mkuu huyo alisema ana mpango wa kuwaleta walimu wa mazoezi ya “aerobics” kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ili watoe mafunzo kwa wananchi ambao watakuwa tayari kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha miili na afya. Mhe. Kijuu alitoa maagizo Wilaya na Taasisi zote za Serikali na binafsi kutenga siku za kufanya mazoezi kila wiki yakiongozwa na viongozi wa maeneo husika.
Mazoezi ya matembezi “Jogging” yalianzia katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kupitia barabara ya Uganda mpaka stendi kuu ya Mabasi kuekea barabara ya Jamhuri na kuhitishwa katika viwanja vya Gymkhana kwa kufanya mazoezi ya viungo baada ya matembezi “Jogging”.
Aidha, katika matembezi na mazoezi hayo yaliungwa mkono na wazee maarufu wa Mkoa wa Kagera waliojumuika kufanya mazoezi hayo. Wazee hao waliongozwa na Mzee Haruna Kichwabuta Sheikh wa Mkoa wa Kagera na Mzee Pius Ngeze.
Wito kwa wananchi wa mkoa wa Kagera hasa waliopo katika mji wa Bukoba na viunga vyake wajumuike katika mazoezi ya viungo yatakayokuwa yanafanyika kila siku ya Jumamosi saa 1:00 asubuhi na kumalizika saa 3:00 asubuhi. Mazoezi hayo yatakuwa yanaanzia katika viwanja vya Ofisia ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na kuishia katika Viwanja vya Gymkhana.
Pamoja na wito huo wananchi waliojumuika katika mazoezi ya leo Jumamosi wanashauriwa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara hasa kila siku ili kuufanya mwili kuzoea mazoezi na siyo kusubiri siku ya Jumamosi pekee pamoja na kufuata mulo sahihi wa vyakula na maji.
Next Post Previous Post
Bukobawadau