Bukobawadau

MZAZI ANAYEPELEKA MTOTO WAKE SHULE BUBU ZISIZOSAJILIWA KUCHUKULIWA HATUA PAMOJA NA MWENYE SHULE


                              Naibu mthibiti mkuu  ubora  wa shule  kanda  ya  nyanda  za  juu  kusini  Aldo Masonda  Bw Aldo Masonda
                                               Na MatukiodaimaBlog 

KUFUATIWA  uwepo  wa utitiri wa shule   binafsi  za  awali  na msingi  za English  Midium au  kiswahili Midium School   maeneo  mbali mbali   mkoani  Iringa   wazazi mkoani hapa  waonywa  kuacha  kuwaandikisha  watoto  wao katika shule hizo   bubu zisizosajiliwa ili  kuepuka kuchukuliwa hatua mzazi na mmiliki wa  shule husika.

Akizungumza na  waandishi wa habari  leo   ofisini  kwake   jana  naibu mthibiti mkuu  ubora  wa shule  kanda  ya  nyanda  za  juu  kusini  Aldo Masonda   alisema  kuwa   mzazi  kabla ya  kumpeleka  mtoto  wake  kuanza  elimu ya awali ama ya msingi  kwenye  shule   yoyote ni lazima  kuomba   kupatiwa namba ya  usajili wa  shule   husika kabla ya kumwandikisha mtoto na  iwapo atakuwa na hofu na namba ya  usajili wa  shule  husika afike  ofisi za mratibu elimu  kata ama ofisi za   elimu  wilaya na mkoa kuweza kupata uhakika  wa usajili wa  shule  husika.

Hivyo  alisema ni  kosa kwa  mzazi kumpeleka  mtoto  shule  isiyo  sajiliwa na  kuepuka  kuwajibishwa  mzazi na mmiliki wa  shule  hiyo  ni  vizuri  wazazi  kufika   ofisi  za  elimu  kujiridhisha ama kufika  ofisi  ya mthibiti   ubora wa  shule  ngazi ya  wilaya   au  ofisi ya kanda na kwa wale  wanaoweza kuingia katika tovuti ya  wizara ya  elimu  ambako  wataona  shule  zote  nchi  nzima ambazo zimesajiliwa na zina sifa ya  kuitwa  shule .

Alisema  kumezuka tabia ya  watu  kuendesha  shule pasipo  kuwa na usajili jambo ambalo ni  kosa la  kisheria na  iwapo  itabainika  mhusika atachukuliwa hatua na kuwa tayari katibu  mkuu wa  wizara  amekuwa  akichukua hatua  mbali mbali ya  kuwaandikia barua  wale  wote  wanaoendesha  vituo  vya elimu wanavyoviita  ni shule  za English Midium .

Masonda  aliwataka  wananchi  wote  kuendelea  kutoa taarifa katika  ofisi yake iwapo watabaini kuwepo kwa shule bubu katika maeneo yao kwani kwa  kimsingi  ni marufuku kwa mtu  yeyote  kutoa elimu kuanzia  watoto  saba na  kuendelea kwa kuwa  iwapo itabainika  kuwa mtu  anatoa elimu kwa  watoto kuanzia  saba na  kuendelea  bila kuwa na namba ya  usajili ni  kosa .

Alitaja  sifa ya  kuitwa   shule  ni pamoja na kuwa na vyumba  vya madarasa  vizivyopungua  saba ,vyoo matundu yasiyopungua 10 ,ofisi  za  walimu tatu  pia kuwa na ardhi yenye  ukubwa  kuanzia heka tatu  ila  alisema  wapo  baadhi  ya  watu wamekuwa  wakivunja sheria  kwa  kuanzisha  shule  bila ya  kuzingatia taratibu .

Kuhusu  mambo  kumi muhimu ya  kuzingatia katika  usajili wa  shule  alisema  ni  pamoja na  andiko la mradi ,hati  miliki ya  kiwanja ,kibali  cha  kujenga  shule ,site plan ya  shule ,barua ya  uthibitisho  wa kuwa  mwenye  shule ,barua  ya uthibitisho kuwa  meneja  wa  shule ,taarifa ya  mhandisi wa majengo wilaya ,taarifa ya  bwana afya  wilaya ,taarifa  ya ukaguzi wa mwisho wa  shule ,orodha ya majira ya  walimu na vyeti  vyao ,mikataba ya ajira ya wafanyakazi  na fomu ya  usajili wa  shule (form no RS 8)

Hivyo  alisema  iwapo  kuna  shule  imeanzishwa na inapokea  wanafunzi  pasipo  kufuata  taratibu  hizo  kumi katika uanzishwaji wake mmiliki wa  shule  hiyo atakuwa amevunja  sheria  na ikibainika atawajibishwa  kisheria  japo  aliwataka  wananchi  kuendelea  kuwekeza katika sekta ya  elimu kwa  kujenga  shule ila kwa  kufuata taratibu  zote .

Masonda  alisema   wao  wanasimamia  ubora  wa  shule  zote   kuanzia shule za awali  hadi vyuo  vya  ualimu vya  binafsi na  serikali na  kuwa changamoto  kubwa wamekuwa wakiipata  kwa taasisi  binafsi kwa  baadhi ya  watu  kuanzisha   kuanzisha  shule  bubu.

Kutokana na  uchunguzi   uliofanywa na mtandao  wa matukiodaimaBlog  katika mkoa  wa Iringa  kumekuwepo  kwa  shule zinazoendeshwa  pasipo  kusajiliwa  huku  wazazi  wakitozwa mamilioni ya shilingi kwa  ajili ya  kulipia ada .

Usikose wiki   Alhamisi  wiki ijayo mwendelezo wa habari  hii 

Next Post Previous Post
Bukobawadau