Bukobawadau

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAFUA MAKALI YA NDEGE MKOANI KAGERA

Wananchi wote wa Mkoa wa Kagera mnataarifiwa kuchukua tahadhari kuhusu ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege ambayo yamethibitika kuwepo nchi jirani.
Kwa kuzingatia kwamba Mkoa wetu wa Kagera unapakana na nchi jirani ya Uganda na pia unazungukwa na nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki isipokuwa Sudan ya Kusini kupitia nchi kavu na majini. Wananchi wa Kagera tunao wajibu mkubwa zaidi wa kuchukua tahadhari zote na kuhakikisha kwamba ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege hauingii nchini Tanzania kupitia Mkoani kwetu.
Hivi karibuni vyombo mbalimbali vya habari vilitangaza kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege (Highly Pathogenic Avian Influenza –HPAI) kwa ndege wa porini na wale wanaofugwa nchini Uganda ambapo ugonjwa huo unasababishwa na virusi vinavyojulikana kwa jina la Influenza A, H5N1.
Aidha, taarifa za kuwepo kwa ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege nchini Uganda zilithibitishwa na Waziri mwenye dhamana na Maendeleo ya Mifugo nchini humo tarehe 15 Januari, 2017 na kutaja maeneo yaliyoathirika kuwa ni yale yanayozunguka Ziwa Victoria na maeneo ya ndani ya ziwa katika Wilaya za Entebbe na Masaka.
Taarifa za awali za kutokea kwa vifo vingi vya ndege pori katika ghuba ya Lutembe kandokando ya Ziwa Victoria karibu na mji wa Entebbe zilitolewa na Wavuvi kutoka sehemu hiyo. Vifo hivyo vya ndege pori vilianza kuonekana tangu tarehe 2 Januari, 2017 na viliendelea kutokea. Baadaye taarifa nyingine zilipatikana za vifo vya baadhi ya ndege wafugwao (kuku na bata) katika Wilaya ya Masaka.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu alitoa taarifa kwa umma tarehe 18 Januari, 2017 kuhusu kuwepo kwa virusi vya Mafua Makali ya Ndege katika nchi jirani ya Uganda, aidha, alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo.Pia Mhe. Ummy Mwalimu alisema kuwa kufikia tarehe 18 Januari, 2017 hakukuwa na taarifa ya kutokea kwa vifo vya ndege au binadamu kuugua ugonjwa huonchini Tanzania.
Mafua Makali ya Ndege ni ugonjwa unaowapata kuku, bata, ndege pori na binadamu. Binadamu anaweza kupata ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege kwa njia zifuatazo:
Kugusana na ndege wanaofugwa au ndege pori, maji maji au damu ya ndege wenye virusi vya ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege. Pili, Kugusana na nguo zilizovaliwa wakati wa kuwahudumia kuku, matenga au magari yaliyotumika kusafirisha kuku, na vifaa vilivyotumika kulishia kuku waliougua Mafua Makali ya Ndege.
Madhara yatokanayo na ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege ni pamoja na kusababisha ugonjwa na vifo kwa binadamu pale anapoambukizwa ugonjwa huo.
Pili, husababisha vifo kwa ndege wafugwao na ndege pori na hivyo kupunguza kasi yao ya kuzaliana. Tatu, ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege hupelekea hasara au kushuka kwa uchumi kwa wafugaji kutokana na kupoteza ndege wafugwao pia kupanda kwa bei ya nyama katika soko.
Katika kuchukua Tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege Serikali mkoani Kagera imepiga marufuku mambo yafuatayo:
Hairuhusiwi kuingiza ndani ya Mkoa kuku na ndege wengine na mazao yao kutoka nje ya nchi bila kibali cha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Pili, mwananchi yeyeyote harusiwi kununua, kuuza au kuchinja kuku bila kupata ushauri wa wataalam kuhusu afya za hao kuku (ndege).
Tatu, wananchi wasichanganye kuku wa nyumbani na kuku wageni bila kufanyiwa uchunguzi wa afya zao na kupatiwa kinga za magonjwa mbalimbali.
Nne, kila wakati wananchi wavae nguo maalum na safi wakati wa kuwahudumia kuku (ndege), pia wanawe vizuri kwa maji na sabuni kila wamalizapo kuwahudumia kuku, kubeba mayai au mazao mengine ya kuku.
Tano, Kuku (ndege) wanaosafirishwa wasiwekwe sehemu moja na watu na pia wakaguliwe na Mtaalam wa mifugo na kupewa kibali cha kusafirisha, aidha, ndege tofauti tofauti wasichanganywe wakati wa kusafirisha. Vifaa vinavyotumika kusafirishia kuku vifanyiwe usafi mara baada ya kutumika.
Ili kujikinga na ugonjwa wa Mafua Makali ya ndege Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu ameagiza mambo muhimu yafuatayo:
Wataalam wa Vituo vya Ukaguzi wa Mazao ya Mifugo Mipakani, Mutukula –Wilayani Missenyi; Murongo – Wilayani Kyerwa; Rusumo, Kabanga, na Murusagamba – Wilayani Ngara; Bandari ya Bukoba na Kemondo na uwanja wa ndege wa Bukoba waimarishe udhibiti wa uingizaji wa kuku, ndege wengine wanaofugwa, ndege pori na mazao yao kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Pili, Mwananchi yeyote atoe taarifa kwa Daktari wa mifugo, Afisa mifugo au vyombo vingine vya Serikali kuhusu kuku au ndege pori wanaougua au kufa. Aidha, mwananchi asikamate ndege pori wanaonesha dalili za kuugua au waliokufa kwa ajili ya kitoweo.
Tatu, Wataalam wa mifugo wa Halmashauri wahakikishe kuwa kuku na ndege wengine wanaoingizwa katika maeneo yao kwa ajili ya kuuza au kufuga na mayai hayatoki nje ya nchi isipokuwa kwa kibali cha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Kila mwananchi anatakiwa kuchukua hatua za tahadhari kuhusu ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege ili ugonjwa huo usiingie nchini mwetu kupitia Mkoa wetu wa Kagera.
Imetolewa na; Sylvester M. Raphael
Afisa Habari Mkoa
KAGERA
25 Januari, 2017

Next Post Previous Post
Bukobawadau