Bukobawadau

TUKUMBUKE KITABU: "SIKU YA GULIO KATERERO" ILI TUPATE MAANA HALISI YA NENO KATERERO, NA TUEPUKE UPOTOSHAJI ULIOIGUBIKA JAMII

Rafiki yangu mpendwa, naandika maneno haya nikiwa na uhakika kuwa yatakufikia na kuweza kukutoa katika kifungo cha mawazo. Ni wajibu wangu na ni haki yako pia, mimi kuweza kujitahidi kwa vyovyote vile niwevyo ili niweze kukutoa katika kifungo hicho ulichoingizwa kwa kujua au kwa kutokujua. Sasa jueni.
Kuendelea kukuacha katika hicho kifungo eti kisa mimi sijafungwa kimwili, nitakuwa najidanganya kwani kama sijafungwa kimwili, nitafungwa kiroho. Ninaweza kukosa hata nafasi ya kuuonja utamu wa milele kwani nitakuwa na kesi ya kujibu huko mbeleni kwa maana Muweza Wa Yote anasema kuwa, “Amuachaye mwenzie akaangamia ilihali anao uwezo wa kumnusuru atakuwa amejiangamiza yeye mwenyewe.” Pia anatuhasa: "Watu wangu wanahangamia kwa kukosa maarifa." Maadam maarifa ninayo, basi nayatumia kukufungua macho, nawe fungukeni sasa.
Kwa mantiki hiyo sasa, nataka nikunusuru wewe usiangamie pamoja na mimi pia kwa kukutoa katika kifungo cha maana ya neno KATERERO.
Ikumbukwe kuwa ni wazi na ukweli usiopingika kuwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na upindishaji wa lazima wa maana ya neno KATERERO hasa miongoni mwa Wanyamahanga, yaani Watanzania ambao asili yetu siyo Bukoba/Kagera. Watu wengi tena wenye akili zao kama mimi na wewe, ambao wangekuwa na uwezo wa kuwatoa wenzao katika dimbwi la maji machafu wameandika na wanazidi kuandika na kuongea mbele ya kadamnasi kiupotoshaji zaidi juu ya maana ya neno KATERERO.
Cha kusikitisha zaidi imefikia hatua sasa hata wale wenye nguvu kubwa na mamlaka makubwa sana kifedha na kiushawishi katika nchi yetu wamekuwa ni miongoni mwa wale wapotoshaji wa maana ya neno KATERERO.
Bora neno hili lingekuwa na maana katika lugha nyingine za kibantu kusingekuwa na shida. Kinachofanyika ni kupotosha maana na kuihusianisha maana hiyo potofu na watu wanaotokea Kagera, has Bukoba. Kwamba neno Katerero kwa Kihaya/lugha nyingine za Kagera ina maaana …. (maana potofu). Ni vizuri zaidi iwapo neno hili lingekuwepo kwa Kiha, Kikurya, Kimakonde, Kinyakyusa, Kipogoro n.k. na lingekuwa na maana hiyo inayolazimishwa. Halipo katika lugha nyingine yoyote na maana hiyo iliyovikwa kwa neno hilo ni upotoshaji mtupu.
UKWELI:
Ukweli ni kwamba, ukijaribu kutarii katika lugha zote za kibantu walau kwa hapa TANZANIA na kuangalia kama msamiati huu una maana nyingine huwezi kuikuta. Maana inayobakia na iliyotukuka ni ileile ya jina la Kata mojawapo katika Halmashauri ya Bukoba (V).
Kata hizo za Halmashauri ya Bukoba (V). ni BUHENDANGABO, BUJUGO, BUTELANKUZI, BUCHULAGO, IBWERA, IZIMBYA, KAAGYA, KAIBANJA, KANYANGEREKO, KARABAGAINE, KASHARU, KATERERO, KATOMA, KATORO, KEMEONDO, KIBIRIZI, KIKOMERO, KISHANJE, KISHOGO, KYAMULAILE, MARUKU, MIKONI, MUGAJWALE, NYAKATO, NYAKIBIMBILI, RUBAFU, RUBALE, RUHUNGA pamoja na RUKOMA.
Neno Katerero kwa ndugu zetu wanyamahanga kwa kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, ndivyo linavyozidi kuonekana kama tusi kubwa sana mdomoni na akilini mwao. Hali hii inapelekea hata wale ndugu zetu ambao wanaishi kwenye kata hiyo kujiuliza mara mbilimbili kulitamka hilo neno hata kama kulikuwa kuna haja ya kufanya hivyo, hii ni kutokana na dhana potofu iliyojengeka kwenye akili za wanyamahanga walio wengi. Hatuwezi kuruhusu hali hii kuendelea. Lazima hatua stahiki zichukuliwe, moja wapo ikiwa ni hii hapa, kuelimishana, na ikibidi hatua zaidi.
HISTORIA:
Kihistoria eneo ambalo hivi sasa linaitwa KATERERO, hapo zamani lilijulikana kama Kemondo. Ni eneo la Gulio la Zamani ambalo lilikuwa limechangamka sana, kwani kulikuwa na bishara nyingi sana zilizokuwa zinafanyika katika eneo hilo. Watu waliuza na kununua mazao, mahitaji mbalimbali, nguo na vitu mbalimbali katika eneo hilo.
Ni kutokana na kuchangamka kwa eneo hilo kibiashara na upatikanaji wa pesa katika eneo hilo ndipo lilipopatikana jina KATERERO na hivyo kubadili jina la awali la Kemondo na kujulikana kama KATERERO. Ijapokuwa ubadilishaji huo wa jina haukuathiri eneo lote lililojulikana kama Kemondo, na ndio maana mpaka leo hii bado kuna sehemu inaitwa Kemondo. Zingatia.
Wenyeji na wafanyabiashara katika eneo hilo walikuwa wanapata pesa nyingi sana kutokana na wingi wa watu waliokuwa wanakuja kununua bidhaa mbalimbali. Ni kutokana na upatikanaji wa pesa huo, wenyeji hao walikuwa wanaambiana “Tugende KUTERA empiha/amaela-Twende tukakusanye/tukapige pesa).
Zingatia:
Tugende ni kitenzi cha Kihaya = Twende.
Kutera ni kitenzi cha Kihaya = Kupiga
Empiha/Amaela ni nomino/jina la Kihaya = Pesa
KATERORO = Sehemu ya kupigia/kukusanyia pesa.
Hifadhi akilini mwako kuwa, kitenzi KUTERA kwa Kiswahili kina maana ya KUPIGA. Ni kutokana na kitenzi hicho kuwa kimeambishwa tukawa tumepata neno/nomino/jina KATERERO ambayo sasa kwa Kiswahili ikawa imebeba maana ya KUPIGIA. Kwa maana ya waliokusudia kuita jina hilo na pia kulingana na muktadha, walikuwa wanalenga dhana ya KUKUSANYA/KUPIGIA PESA.
Zaidi ya hayo, hata waliosoma zamani kama Mimi mnaweza kukumbuka kile kitabu cha shule ya msingi Kiswahili darasa la nne kama SIO la tano kiliandika na kuelezea juu ya gulio la KATERERO "SIKU YA GULIO KATERERO." Laiti neno hili lingekuwa tusi kama linavyolazimishwa kubeba siku hizi, lisingekubalika kutumika kama ilivyokuwa katika kitabu hiki kilichotumika nchi nzima!
Narudia tena nomino KATERERO (sehemu ya KUKUSANYIA/KUPIGIA), kimetokana na kitenzi KUTERA (KUPIGA). KUPIGA/KUKUSANYA PESA ndiyo maana halisi na ambayo haina kigugumizi ndani yake kuhusu KATERERO.
Ndugu zangu WANYAMAHANGA (Watanzania ambao siyo Wahaya), hiyo ndiyo maana halisi ya neno KATERERO ijapokuwa hamjakatazwa kukopa msamiati huo na kuutumia katika maana mtakayo nyie, Msipotoshwe na wala msidhalilishe wenyeji au ndu zenu Wahaya wanaotoka katika eneo la kata KATERERO na Bukoba/Kagera kwa ujumla.
Mungu awabariki.
Na mwenye masikio asikie!
Shukrani kwa Mtunzi wa UJUMBE HUU.
Next Post Previous Post
Bukobawadau