Bukobawadau

WATUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA WAPEWA DHAMANA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo imetoa dhamana kwa baadhi ya wasanii waliokuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Wasanii hao waliokamatwa Ijumaa ya wiki iliyopita wamefikishwa mahakamani leo asubuhi ambao wamepewa dhamana ya TZS milioni 10 kwa kila mmoja ambapo wametakiwa kuwasilisha bondi ya TZS milioni 10 bila mdhamini. Mbali na dhamana hiyo mahakama imesema kuwa wasanii hao watakuwa chini ya uangalizi wa karibu kwa mwaka mmoja na kama watavunja masharti waliyopewa basi watarejeshwa mahakamani.
Wasanii hao waliopewa dhamana wanashughulikia taratibu za kuikamilisha na endapo watafanikiwa kukamilisha basi wataachiwa huru na mahakama.
Wakati baadhi ya wasanii wakipewa dhamana hiyo, Petitam na wenzake nne wao wamepandishwa kizimbani mchana wa leo kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Jumla ya watu 112 wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya ambapo 12 kati yao ni wasanii wa Bongo Fleva na Bongo Muvi.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amethibitisha kuwa wanamshikilia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kufuatia kauli zake alizozitoa dhidi ya serikali.
Tundu Lissu alikamatwa jana jioni mjini Dodoma baada ya kutoka kwenye kikao cha bunge na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam.
Next Post Previous Post
Bukobawadau