Bukobawadau

TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI (UVCCM) KWA VYOMBO VYA HABARI UPANGA DAR ES SALAM IJUMAA 31 MACHI 2017

 Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Shaka Hamdu Shaka akizungumza na Wana Habari Makao Makuu UVCCM Upanga.

Ndugu waandishi wa habari,
Tunawashukuru kwa kupokea wito wetu na kuja, karibuni sana tunawaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana nanyi katika kila hatua.

Aidha Umoja wa Vijana wa CCM unavipongeza sana vyombo vyote vya habari nchini kwa juhudi zenu za kuhabarisha, kuelimisha, kuwaasa, kuwaelekeza na kuihabarisha jamiii katika masuala kadhaa yanayohusiana na mipango ya maendeleo, mikakati, sera na malengo ya Serikali na mipango ya vyama vya siasa.

Ndugu Waandishi wa habari.
Tumewaita leo kuzungumzia mambo 2 makubwa, na suala zima la mtikisiko wa demokrasia katika mchakato wa uteuzi wa wagombea Ubunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulivyoendeshwa ndani ya vyama vya upinzani nchini.

Bunge la Afrika Mashariki kama mjuavyo ni chombo kikubwa na chenye heshima ya pekee katika kanda yetu. Kuwepo kwake kunaashiria muendelezo wa kufufua dhana, dhamira, mikakati, fikra na malengo ambayo yaliasisiwa na waasisi wa Mataifa yote yaliyomo katika Kanda yetu ili hatimaye siku moja ishuhudiwe Kanda hii na Bara zima la Afrika likiunda dola moja.

Ni jambo la heri na faraja kuona EAC ya sasa ikiwa ni yenye kufikia malengo ya utengamano na mafanikio hususan katika nyanja za kiuchumi na kiusalama kama vile kuwa na Pasi moja ya kusafria, miingiliano ya wananchi wake katika ufanyaji wa biashara pia mkakati kuelekea kupata viwango sawia vya ushuru wa Forodha.

Masuala mengine ni kuona maeneo ya mipaka yetu kukiendelea kuwa na ustawi wa hali ya utulivu na usalama, wakati huo EAC ikifanya kila linalowezekana kumaliza migogoro yake ya kisiasa ambapo mazungumzo ya upatanishi huko Burundi yamekuwa yakiendelea chini ya mpatanishi mkuu Rais mstaafu Benjamin Mkapa sambamba na wananchi wa pande zote za nchi wanachama tukishuhudia wakiishi kwa maelewano, umoja, udugu na mafahamiano.
Ni katika jumla ya mambo yanayofurahisha na pengine yakiwasuta na kuwaaibisha maadui na vibaraka ambao aghalab hutumiwa kwa malipo yenye ujira wa dhambi toka kwa mabeberu katika kuhakikisha mipango batili ya kutaka kudhoofisha, kuigawa na kukwamisha juhudi za EAC isiimarike..

Aidha kuibuliwa na kupokewa kwa mpango uitwao " One Stop Boarder" yaani (OSB) sasa umefanikiwa huko mipakani baina ya nchi wanachama. Pia kuanzishwa miradi mikubwa ya kiuchumi mfano bomba la mafuta toka Kampala (Uganda) hadi Tanga (Tanzania) ujenzi wa reli toka kigali hadi Uganda huku EAC ikielekea kuwa na sarafu moja kabla ya kufikiwa azimio la uundwaji wa Shirikisho moja.

Umoja wa Vijana wa CCM tumelazimika kuyataja na kuyaainisha maeneo hayo yaliopata mafanikio kwa uchache lengo likiwa ni kuonyesha uwepo na ustawi wa EAC pamoja na umuhimu wa bunge lake kama ni jambo nyeti na wala si suala dogo au la mchezo mchezo kama ambavyo baadhi ya vyama vya siasa nchini vimeonyesha udhaifu.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Baadhi ya vyama vya siasa nchini vimeshindwa hata kuteua wagombea ubunge wengi ili kuwania nafasi katika bunge hilo la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu zinazotokana aidha na ubinafsi, umimi na udikteta.
Tunachukua fursa hii kwanza kukipongeza Chama Cha Mapinduzi na wanachama wake wote 450 ambao kwa ujasiri, uwezo na kujiamini kwao wamethubutu kujitokeza na kuchukua fomu za kuwania nafasi za ubunge wa EAC.

Kitendo cha wanachama hao wa CCM kujitokeza kwa wingi kimsingi kimeidhihirishia dunia kwamba chama chetu bado ni cha kidemokrasia kinachoungwa mkono na kuaminiwa na wananchi wengi wakiwemo Vijana, wanawake na wana taaluma mbali mbali wakitambua ndicho chama pekee imara chenye kujali, kuthamini na kufuata misingi ya usawa na demokrasia ya kweli.

Wanachama 450 wa CCM walichukua fomu kwa kufuata taratibu baada ya mchujo wa kidemokrasia kufanyika ndani ya CCM, wanachama 12 wamebahatika kuteuliwa na vikao vya kikatiba ambapo sasa wagombea hao watasimama mbele ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusaka ridhaa kwa kujieleza na kuomba kura.

Ndugu Waandishi wa habari,

Umoja wa Vijana CCM kwa tunasikitishwa sana na mwenendo wa demokrasia ndani ya vyama vya upinzani katika uteuzi wa kuwapata wagombea wa ubunge wa bunge la Afrika Mashariki (EALA) Chadema, CUF na NCCR Mageuzi kwa jinsi walivyowasilisha uwakilishi haba na finyu lakini pia kujitokeza kwa wagombea wachache hali inayoonyesha uminyaji wa demokrasia ndani ya vyama vyao.

Chadema na washirika wao mara kadhaa hujigamba vichochoroni na kujionyesha kuwa wao ni watetezi wa demokrasia lakini unapofikia wakati wa utekelezaji wa jambo hilo kwa vitendo, ndani ya chama hicho humea ukandamizaji wa haki na kujitokeza upendeleo, ukanda, kubebana aidha kwa asili, ujamaa na urafiki au kulipana fadhila.
Katu huu si mwenendo mwema ulioonyeshwa na vyama vya upinzani. Vimejipaka matope ya fedheha kwa kushindwa kuonyesha kama ni waumini wa kweli wa demokrasia badala yake havikujali wala kuheshimu dhana ya demokrasia na kujikuta vimejianika na kuuthibitishia umma wa watanzania kuwa vyama hivyo ni vya watu maalum vya kibwanyenye na vya kiimla .

Kufanya uteuzi wa wanachama wanaogombea nafasi za kidemokrasia kwa kumtazama asili yake, anatoka kanda ipi, kabila, imani yake au nasaba licha ya kwenda kinyume na misingi ya Taifa letu lakini pia ni kinyume na matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

UVCCM kwa kauli moja tunawaamsha na kuwatumia ujumbe watanzania wenzetu hususan Vijana mahali popote walipo wavikatae na kuvikwepa vyama vya aina hiyo, wasikubali kugawanywa kwa asili zao, imani au rangi na nasaba.

Taifa letu ni alama pana ya kuenzi na kudumisha demokrasia si tu barani Afrika lakini vile vile duniani kote, hivyo kwa umoja wetu, kwa nguvu zetu, akili na maarifa tulionayo, abadan tusijaribu kuichezea amani yetu, umoja na mshikamano wetu uliojengwa na waasisi wa Taifa letu na kukubali kuvishabikia vyama na viongozi wasaka madaraka kwa hila ambao ni wafujaji na wakandamizaji wa misingi ya demokrasia ndani ya vyama kama ilivyojionyesha kwa vyama vya upinzani vya Tanzania katika uteuzi wa wabunge EAC.
Mchakato wa Uchaguzi ndani ya UVCCM.

Uchaguzi Mkuu wa CCM wa mwaka 2017, unafanyika wakati ambapo CCM inatimiza miaka 40 tokea kuasisiwa kwake tarehe 5 Februari, 1977 na ni wakati ambapo nchi yetu inatimiza miaka 25 ya Mfumo wa Vyama Vingi ulioridhiwa na Mkutano Mkuu wa CCM kutokana na busara za Viongozi wake.

Ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Chama na Jumuiya zake inaonesha mchakato wa Uchaguzi wa Jumuiya za CCM kuwa unaanza kabla ya ule wa CCM. Utaratibu huu unalenga kuwawezesha wanachama wa Jumuiya za CCM ambao watakuwa ni wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika CCM, au wale waliochaguliwa kuwakilisha Jumuiya zao katika Vikao vya CCM ili waweze kuhudhuria mikutano ya Chama inayowahusu.
Umoja wa Vijana wa CCM umekamilisha maandalizi yote ya msingi ya awali kwa ajili ya Uchaguzi unaotarajia kuanza tarehe 1 April, 2017 ikiwemo kusambaza vifaa katika Mikoa na Wilaya zote nchini wa ajili ya kufanikisha uchaguzi kwa wakati.

Aidha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi imekamilisha mapitio na uteuzi wa Makatibu wa Mikoa na Wilaya katika Jumuiya ambao watakuwa ndio wakurugenzi wa Uchaguzi katika maeneo yao.
 Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Shaka Hamdu Shaka akizungumza na Wana Habari Makao Makuu UVCCM Upanga (PICHA NA FAHADI SIRAJI)

Tunaendelea kuwakumbusha Watendaji wetu muda wote kusimamia haki, ukweli na usawa lazima vijana wa CCM muda wote tuishi katika maneno na maagizo ya Mwenyekiti wetu wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli.

Hatutamvumilia mtendaji yeyote atakayekiuka Kanuni, Taratibu na miongozo kwa makusudi ili kufurahisha kikundi au watu fulani. Uchaguzi huu 2017 UVCCM tunataka kuidhihirishia dunia na Vyama vya Upinzani kuwa CCM ni Chuo Cha Demokrasia ulimwenguni.

Mwisho niendelee kuwahamasisha vyema wote nchini yenye sifa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbali za uongozi ndani ya CCM na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya Shina, Tawi, Kata, Wilaya, Mikoa na Taifa.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Shaka Hamdu Shaka (MNEC)

KAIMU KATIBU MKUU

Next Post Previous Post
Bukobawadau