Balozi wa Tanzania Nchini Ujerumani Mhe Philip Marmo Amvisha Cheo Kanali wa JWTZ jijini Berlin
Katika hali ambayo haijazoeleka
na iliyoonekana kuwa ngeni, Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo alimvisha Cheo Kanali Joseph Bakari aliyepandishwa Cheo hivi karibuni kutoka Luteni
kanali.
Hafla hiyo fupi iliyohudhuriwa
na ujumbe wa Watanzania waliohudhuria
Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Jijini Berlin Ujerumani akiwemo
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya Utalii na
Utamaduni Mhe. Chimberi Heri, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii
Tanzania Mhe. Geofrey Meena, Maafisa wa
Ubalozi na wageni wengine ilifanyika karibuni katika Ofisi
za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Berlin nchini Ujerumani.
Akitoa maelezo mafupi kuhusu
tukio hilo Mhe. Balozi alitanabaisha
kuwa kwake ni tukio la kwanza na la la aina yake kupewa dhamana hiyo na kwamba amepokea maelekezo husika kutoka
Makao Makuu ya Jeshi kupitia Wizarani.
Akisoma sehemu ya maelekezo hayo alisema
“ kwa kawaida Afisa anapopanda cheo akiwa nje ya nchi iwapo hataweza kwenda
Tanzania kuvalishwa cheo hicho na viongozi husika wa JWTZ, cheo hicho kipya
huvishwa na Afisa Mkuu au Balozi wa Tanzania katika Nchi aliyepo”.
Hivyo, kwa mujibu wa sheria na mamlaka aliyekuwa nayo anatakiwa kumvisha Cheo kipya cha ukanali mhusika kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania. Kwa mujibu wa maelekezo hayo Kanali Bakari alipandishwa cheo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kuanzia tarehe 31 Januari 2017.
Akitoa nasaha fupi na salam za pongezi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, wageni waliohudhuria hafla hiyo na Watanzania wote kwa ujumla kwa Kanali Bakari aliyefuatana na Mkewe Bi Lucy Mlingi, Mhe. Balozi alimkumbusha Kanali Bakari kuwa ni dhahiri kuwa kupandishwa kwake cheo kumetokana na imani ya Mkuu wa Majeshi na viongozi wengine wakuu katika utendaji wake,uadilifu, bidii katika kazi na utii. Hivyo ni vizuri ahakikishe kuwa anafanya kazi kwa weledi, bidii zaidi na moyo wa kujituma ili kuleta tija na ufanisi zaidi kwa manufaa ya JWTZ, Tanzania na Dunia kwa ujumla. Mwisho aliipongeza familia yake hususani Mkewe kwa mafanikio hayo na kuwatakia heri, Baraka na afya njema.
Kanali Joseph Bakari ni mwakilishi wa JWTZ katika Sekretarieti ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (International Military Sports Council-CISM) kama Mshauri na msaidizi wa Mkurugenzi wa Michezo katika Baraza hilo.
Baraza hilo liliundwa tarehe 18 Februari 1948 mara baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Dhima kuu ikiwa ni kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili kama njia ya kueneza amani duniani badala ya vita. Baraza hilo lina jumla ya nchi wanachama 134 Tanzania ikiwemo. Miongoni mwa shughuli za Baraza hilo ni kuandaa mashindano ya michezo ya majeshi ya Dunia.
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo na Acting Colonel Joseph Bakari wakisikiliza maelezo kabla ya hatua ya kumvua cheo cha zamani na kumvika kipya
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akimvisha cheo kipya Colonel Joseph Bakari
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akipikea zawadi maalumu ya Sekretarieti ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (International Military Sports Council-CISM) toka kwa Kanali Joseph Bakari wakati wa hafla hiyo
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akiwa na Kanali Joseph Bakari na mkewe
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma (kushoto) Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya Utalii na Utamaduni Mhe. Chimberi Heri (wa pili kulia) Colonel Joseph Bakari na mkewe
Tukio hilo la kuvisha Cheo lilihitimishwa na kuimbwa wimbo wa Taifa wa Tanzania.
Picha ya pamoja na ujumbe wa Watanzania waliohudhuria Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Jijini Berlin Ujerumani akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya Utalii na Utamaduni Mhe. Chimberi Heri, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania Mhe. Geofrey Meena, Maafisa wa Ubalozi na wageni wengine ilifanyika karibuni katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Berlin nchini Ujerumani. Source: Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Berlin Ujerumani