SIMBACHAWENE ASISITIZA USAFI WA MAZINGIRA KATIKA MJI WA DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene amewataka viongozi wa Manispaa ya
Dodoma kuwa wabunifu katika
kushughulikia suala la usafi wa mazingira ili kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa
kuvutia na wakati huo huo kuutokomeza ugonjwa wa kipindupindu.
Alisema ili waweze kutekeleza jambo hilo mapema wanatakiwa kuanza
utekelezaji katika masuala yasiyohitaji
fedha wakati wakitafuta fedha za kutekeleza mambo yanayohitaji fedha ili
kuweza kufanya mabadiliko kwa haraka.
Akizungumza katika ziara
fupi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma iliyokuwa na lengo la
kuhamasisha utunzaji na usafi wa mazingira ya mji wa Dodoma ili kujikinga na
kipindupindu katika maeneo ya River Pombe, Uwanja wa Barafu na katika Soko kuu
la Majengo iliyofanyika leo mjini Dodoma, Mhe. Simbachawene amesema itakuwa ni
aibu kuwa na kipindupindu katika mji wa Dodoma kwakuwa hivi sasa unapokea
wageni mbalimbali kutoka nchini na nje ya nchi.
Mhe. Simbachawene aliwataka
viongozi wa Mkoa wa Dodoma, Manispaa ya Dodoma na Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu
kushirikiana na kuhakikisha mazingira ya mji wa Dodoma yanakuwa safi likiwepo suala la kuifanyia mitaro usafi hasa
katika kipindi hiki ambacho mji wa Dodoma upo katika harakati za kuwapokea
wageni wengi wakiwepo Mabalozi kutoka
Nchi mbalimbali.
Alitaka uongozi wa
Manispaa ya Wilaya ya Dodoma kuhakikisha wanaweka ulinzi katika eneo la Pombe
River kwa kutumia Walinzi wa jiji au Jumuiya ya watu waliojenga karibu na eneo
hilo ili kulilinda eneo hilo na
kuhakikisha wananchi hawatupi takataka katika eneo hilo.
Aliwataka wananchi wa
Dodoma kujipanga kutumia fursa zinazojitokeza Dodoma kutokana na kuja kwa
wageni wengi ili kujiongezea kipato
lakini wakati huo huo kuhakikisha huduma wanazotoa zinazingatia ubora kwa kuwa
safi .
Mhe. Simbachawene aliwahakikishia
wageni wanaohamia Dodoma kuwa Mamlaka ya Mkoa wa Dodoma na Manispaa zimejipanga
katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinakuwepo wakati wote na kuwatoa hofu za kukosa huduma
za afya.
“ Serikali imejenga
hospitali kubwa ya Benjamin Mkapa ambayo ubora wake kwa utoaji wa huduma Tanzania inaweza kuwa ya
kwanza kwa kutoa matibabu ya daraja la Kwanza. Kituo cha Afya cha Makole pia
kimeboreshwa na kupandishwa hadhi ambapo sasa kitatoa huduma za hospitali.
Lakini pia vituo binafsi vya afya na hospitali ya DCMC vimejipanga kusaidiana
na Serikali katika utoaji wa huduma za Afya. Alisisitiza Mhe. Simbachawene.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Zainab Chaula aliwasisitiza watendaji wa Mkoa
na Manispaa ya Dodoma kuhakikisha wanasimaia vizuri usafishaji wa mazingira ili
kuhakikisha kuwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu yanatokomezwa kabisa.