Bukobawadau

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John  Pombe Magufuli ametengua  rasmi  nafasi ya   Mtendaji  Mkuu wa Shirika  Elimu Kibaha  Dkt. Crispin  Mpemba  ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za kiutendaji zinazomkabili.
Akijibu swali la Waandishi wa Habari waliotaka kupata ufafanuzi juu ya hatma ya tuhuma mbalimbali zinazolikabili Shirika la Elimu Kibaha ambazo zimekuwa zikiandikwa kwenye vyombo vya habari kwa muda mrefu sasa, Mhe. Simbachawene alisema kutokana na kuwepo kwa tuhuma mbalimbali za uendeshaji, Mhe. Rais  Magufuli tarehe  4/3/2017  ametengua rasmi nafasi ya Mtendaji huyo ili kupisha uchunguzi.
“ Ni kweli tuhuma juu ya uendeshaji wa Shirika la Elimu Kibaha likiwemo suala la Mikataba iliyoingiwa na Shirika hilo zimekuwepo kwa muda mrefu sasa. Sisi kama Wizara hatukutaka kukurupuka kufanya maamuzi na tukaamua kuunda kikosi kazi ili kufanya uchunguzi na matokeo ya uchunguzi huo  yanapelekea kuwepo kwa hoja  zinazohitaji uchunguzi zaidi.  Hivyo, ili uchunguzi huo uweze kufanyika  Mhe. Rais amemsimamisha kazi Mtendaji huyu Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha ili kupisha uchunguzi wa kina dhidi yake. Alisema Mhe. Simbachawene
Alisema uamuzi wa kumsimamisha umechukuliwa kwakuwa tuhuma za awali zilizojitokeza dhidi yake zinajenga hoja ya kuhitajika kufanyika kwa uchunguzi zaidi.
Kwasasa nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha inakaimiwa hadi hapo  uchunguzi utakapokamilika.

Rebecca Kwandu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
06/03/2017.
Next Post Previous Post
Bukobawadau