Bukobawadau

MAMA MJANE MLEMAVU APATIWA MGUU BANDIA NA MKUU WA MKOA ILI KUENDELEA KUJIKIMU KWA KUFANYA SHUGHULI ZAKE

Kuwa kiongozi mzuri kwa mtu yeyote ni lazima uwe na huruma, kuwajali watu waliokaribu na wewe na wasiokuwa karibu, kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi, lakini jambo muhimu sana kutimiza ahadi unazozitoa mbele ya wale unaowaongoza na mwisho kuguswa na matatizo ya wenzako na kuwatia faraja.
Kwa hayo yaliyotajwa hapo juu ameyatimiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu kwa mama mjane Shemsha Rajab kutoka Kata ya Kashai Mtaa wa Rwome Manispaa ya Bukoba ambaye ni mlemavu wa mguu (ana mguu mmoja na mguu wa pili umekatikia gotini) na anatumia mguu bandia.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu kwa fedha zake takribani shilingi 700,000/= (laki saba) amemnunulia mguu bandia na kumkabidhi leo tarehe 11/05/2017 ofisini kwake. Akiongea kabla ya kumkabidhi mama huyo mguu bandia Mkuu wa Mkoa alisema kuwa alikuwa anatimiza ahadi yake aliyoitoa mwaka jana Juni 27, 2017 kwa mama Shemsha alipotembelea Haospitali Teule ya Wilaya ya Missenyi Mugana.
“Nilipotembelea Hospitali hiyo kwenda kukagua shughuli za upasuaji wa akina mama wenye tezi shingo ambao ulikuwa umefadhiliwa na Hospitali Teule ya Mugana kwa kushirikaiana na Mzee Raza Fazar wa mjini Bukoba kupitia katika mradi wake wa matibabu (Izaas Medical Project) niliguswa na mama huyu kwani niliona jinsi anavyopata shida na nilimuhaidi kumpatia mguu bandia mpya.” Alieleza Mhe. Kijuu.
Mama mjane Shemsha Rajabu alimshukuru Mkuu huyo wa Mkoa na kusema kuwa anaguswa na matatizo ya wananchi wake. Pia alimshukuru sana Mzee Raza Fazar kwa huruma yake ya kuhakikisha anawahudumia wananchi wenye matatizo hasa wale wasiokuwa na uwezo kwa kuwapatia huduma za matibabu bure kupitia mradi wa matibabu wa Izaas.
 Kutoa ni moyo usambe ni utajiri kama wahenga wa zamani walivyosema, kila mmoja wetu anatakiwa kumsaidia mwenzake mwenye matatizo ili wenye matatizo wajisikie kama binadamu wenzao. Mama Shemsha alisema kuwa mguu wake wa bandia wa kwanza aliupata mwaka 1997 lakini kwa sasa mguu huo ulikuwa hautumiki tena kwasababu unyayo wake ulikuwa umeharibika.
Next Post Previous Post
Bukobawadau