Bukobawadau

MAONI YA MDAU KUHUSU CHANGAMOTO KATIKA KATA YA KATORO

@bukobawadau ,Asante sana kwa kutoa Documentary fupi kuhusu Katoro (Bukoba Vijijini).
Katoro ni nyumbani kwetu. Nimefurahi kusoma na kuona yaliyojiri wakati mlipotembelea Katoro. Mchango wangu kama mwana Katoro ni kuhusu mambo machache ambayo naona, kama BukobaWadau mtaweza kuyatilia mkazo, labda yanaweza yakapewa kipa umbele na Viongozi wa Ngazi husika: Mambo hayo ni haya:-
1) Kituo cha Afya: Kituo hiki, kama mlibahatika kufika na kuongea na wahusika, utaona kwamba kwa uhalisia, kinahitaji ukarabati wa hali ya juu. Mazingira na usafi ni tatizo. Kituo kinahudumia vijiji takriban 5, Ruhoko, Kyamulaire, Ishembuliro, Ngarama, Kayanja, Nyakitwero, Luongora, Musira, na wakati mwingine Kaibanja, Kazinga, Kyenge na vinginevyo. Sina takwimu sahihi, lakini kutokana na uhalisia na mazoea, Kata nzima ya Katoro wanategemea kituo hiki. Hakuna Ambulance, ina maana kukiwa na mgonjwa Mahututi, lazima ndugu wachangishane kumpeleka ama Bukoba mjini au Kagera Sugar. Na sasa hivi huko Kagera Sugar, kuna tatizo la Madaktari (Wataalam). Option inayobaki ni kwenda Mugana, au Katekana – Izimbya, ambako ni mbali sana. Kwa maana nyingine, mkulima wa kawaida, asiye na uwezo wa kipato – hatma yake ni Miujiza ya Mungu. Ushauri: Wahusika, (Diwani/Mbunge) walitizame upya tatizo hili – wapandishe daraja kituo hiki ili kiwe Hospitali, kiweze kutoa huduma stahiki na kupata vitendea kazi (X-ray, Ultra Sound, nk) sambamba na wataalaam wa kutoa huduma hizo. Umeme tayari upo, kinachotakiwa ni kuboresha huduma, ili wananchi waache kupata adhabu hii. MSD pia waweke duka la Dawa, na zipatikane.
2) Elimu: Kuna shule za Kata kama 2 au 3. Shule hizi zimekuwa hazifanyi vizuri kwa miaka mingi, sababu haijulikani. Unashangaa shule ya Katoro Secondary (wenyewe wanaita kwa Kagali), wengi wa wanaomaliza ukiongea nao utashangaa – kiwango chao cha uelewa ni kidogo mno. Je, Serikali haitumi Wakaguzi kufuatilia hizi shule zinazofanya vibaya? Je, Mratibu – Elimu (Kata) hajaliona tatizo hili. Si kweli kwamba watoto wetu hawana akili, si kweli. Angalau watoke wachache wapate Div. II au III – lakini IV na O, miaka yote, lazima kuna tatizo hapa. Wahusika waulizwe, tatizo ni Walimu au ni kitu gani. Wanafunzi ukiwauliza, wapo wanaosema hata majibu yao ya mitihani hawayapati – Mkuu wa Shule anachelewa kupeleka malipo Baraza la Mitihani, matokeo ya wanafunzi yanafungiwa, Je, ni kweli???? Wazazi wanakosa mwamko wa kufuatilia au ni kutoelewa. Na Mwalimu Mkuu wa shule husika, anatoa majibu gani kwa Wakaguzi?
3)Maji Safi:Miaka ya nyuma, tukiwa wadogo, kulikuwa na mabomba yametandazwa vijiji vyote, na maji yalikuwa yakitoka vizuri tu. Sasa hivi naona hata koki zenyewe zimehujumiwa. Katoro, kwa upande wa Maji, tunayo tena mengi sana na masafi. Vyanzo ni vingi, mfano Lake Ikimba, Katokoro, Kishambagilo,nk vyote hivi, kukiwa na mipango mizuri, vina uwezo wa kuhudumia wakazi wa vijiji vyote kuweza kupata maji safi. Je, nani tumkamate shati kuhusu maji? Diwani au Mbunge??? Na kama hawa watu hawafanyi kazi kama Team, sidhani kama wataweza kuhudumia wananchi. Tatizo la Itikadi za vyama, zinatukwamisha. Nani awajibishwe katika hili!!!!
4) Barabara: Ili uchumi wa eneo ukue, lazima uwe na miondo mbinu bora na hasa barabara. Barabara zikipitika, huyu mwananchi Mkulima, ataweza kusafirisha mazao yake kupeleka sokoni (popote) kwa uhakika. Umepita barabara zote kuingia Katoro umeona kwamba ni mbovu kupindukia. Ukipita Ibwera, utaona kuanzia Kaibanja, Nyakibimbili, kuja mpaka Karonge, hadi utokee Kanazi – yote ni mbovu mno. Ukipita Kashaba, kutokea Kyaka – umeona ni mbovu mno. Tuwaombe wanaokaa vikao vya miradi ya maendeleo (Wilayani) watufikirie katika Bajeti za 2017/2018 angalau kiwango cha Changarawe Safi. Lami tusubiri ule mpango wa kuboresha Kemondo – Kanazi – Ibwera – Kyaka, huo tumeuona katika makabrasha.
5) Uzalendo: Nimeona umeongea na Mzee wetu mmojawapo. Watu wa Katoro walioko nje, wahamasishwe wabadilike, wapende kwao. Waangalie mifano ya watu wa maeneo mengine. Kama unaijua Kemondo ya zamani na sasa, au Muleba ya Zamani na ya Sasa, au Bunazi ya Zamani na ya sasa, utakubaliana nami kwamba, Katoro lazima wakubali kubadilika, kama wanataka maendeleo ya kweli. Zile zama za ubinafsi, chuki, wivu, na uvivu vimepitwa na wakati. Vijana wengi waliosoma wenye maendeleo, wanaotoka Katoro, hawataki kurudi kwa sababu za historia chafu ya Katoro. Tuna vijana wasomi wengi tu, wengine wana uwezo mkubwa tu wa kuweza kuwekeza (viwanda, kilimo, hospitali, vyuo nk) lakini wanachelea kurudi kwa kuhofia unafiki na vitimbwi vya watu wa hapo.
Ifike mahali wakubali kwamba enzi tulizo nazo hazina nafasi tena na mambo yasiyokuwa na tija. Waamke, wafanye kazi, wapendane, wawe na mshikamane, watoke hapo walipo wasonge mbele.
Bukobawadau Media
#katoro #bukoba #bukobawadau #Kagerayetu
Next Post Previous Post
Bukobawadau