MAHAFALI YA 6 YA GENIUS KINGS YAFANA JIJINI DAR
Mkurugenzi Mkuu wa Shule ya Genius Kings Nusery& Primary School, Machage Kisyeri, (Kulia) akisoma hotuba.
Mwalimu Mkuu wa shule, Aloyce Siame (kushoto) akimkabidhi risala Profesa Joseph Kahamba , ambaye alikuwa mageni rasmi wakati wa mahafali hayo.Katikati ni Mkurugenzi wa shule Julius Rutabanja.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Aloyce Siame (kulia) akikabidhiwa zawadi ya kikombe na Profesa Joseph Kahamba.
Paroko msaidizi wa Roho Mtakatifu Parokia ya Segerea Velence Kisaka (kulia) akibarikia shule hiyo baada ya kufanya ibada kwa ajili ya kuwaombea wanafunzi wa darasa la saba wanaojiandaa na mitihani ya taifa.
Mwalimu wa Dini ya Kiislam Shekhe Hussein Abdalah akiongoza swala kwa ajili kawaombea watoto wa darasa la saba katika shule hiyo.
Mgeni rasmi akiangalia wanafunzi wakifanya majaribio ya sayansi.
Wahitimu wakitoa burudani kwa wazazi na wageni waalikwa.
Kikosi cha scout shuleni hapo wakifanya mambo yao
Wanafunzi wakionyesha kipaji cha kucheza ngoma za asili.
*Wahitimu waaswa kwenda na kasi ya sayansi na teknolojia
Wakati serikali ya Tanzania inao mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,wanafunzi wanaohitimu masomo wametakiwa kujiona sehemu ya mkakati huo na kusoma kwa bidii kupata ujuzi wa taaluma mbalimbali ikiwemo kutoogopa kusoma masomo ya hesabu na sayansi.
Ushauri huo umetolewa na daktari bingwa nchini wa magonjwa ya nevu (Neurosurgery) kutoka Chuo Kikuu cha Muhimbili,Profesa Joseph Kahamba, wakati wa mahafali ya darasa la saba ya msingi ya Genius Kings yaliyofanyika Segerea jijini Dar es Salaam .
Profesa Kahamba alisema kuwa nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto ya kuwa na wataalamu waliobobea katika nyanja mbalimbali ambapo aliwataka wanafunzi wanaohitimu masomo na waliopo mashuleni na vyuoni kujipanga kuhakikisha wanapata utaalamu wa fani mbalimbali tayari kwa kutumikia taifa la Tanzania.
“Wanafunzi waliopo mashuleni na vyuoni mnapaswa kujipanga kwa kuhakikisha mnasoma kwa bidii na kupata ujuzi wa fani mbalimbali kwa kuwa mapinduzi ya kuendeleza taifa letu yanayoendelea yanahitaji wataalamu wa fani mbalimbali na wanaotegemewa kuchukua majukumu hayo hawatoki nje ya nchi bali ni nyinyi vijana wa kitanzania”Alisema Profesa Kahamba.
Aliongeza kusema kuwa kinachotakiwa kwa wanafunzi waliopo mashuleni na vyuoni kujibidisha kusoma kwa bidii na kupata taaluma za fani mbalimbali na wahakikishe wanajiamini na kuhakikisha ndoto zao walizojiwekea zinatimia na wanakuwa na uzalendo wa kuitumikia nchi na kuleta maendeleo chanya katika jamii kupitia elimu waliyoipata.
Profesa Kahamba aliupongeza uongozi wa shule ya Genius Kings kwa kufanya uwekezaji katika sekta ya elimu kwa kuwa umelenga kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha elimu nchini na kuleta mabadiliko wenye jamii kwa kuwa elimu ni njia pekee ya kuleta maendeleo kwa haraka katika ujenzi wa taifa . “Naupongeza uongozi wa shule kwa kuwekeza katika elimu na nawapongeza wazazi ambao wanawekeza katika elimu kwa kusomesha watoto wao maana elimu bora katika jamii inachangia kuleta mabadiliko ya nchi haraka”.Alisema
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bw. Aloyce Siame, alisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 tangu shule ianzishwe imeweza kushikilia rekodi ya kufanya vizuri kwa kufaulisha wanafunzi wa darasa la saba na la nne kwa kiwango cha juu na kuingia katika shule tano bora wilayani Ilala na shule bora 20 mkoani Dar es Salaam mfululizo hali ambayo imewajengea hari ya kuzidi kufanya vizuri kwa mwaka huu na miaka ijayo.
“Moja ya mtazamo wa shule hii ni kuifanya kuwa shule bora ya mfano inayotoa elimu bora nchini kuanzia shule ya awali na shule ya msingi na sekondari.”Tumejipanga kuhakikisha lengo hili linatimia na tunatoa shukrani kwa serikali,wazazi na wadau wote ambao wameonyesha kutuunga mkono katika kipindi hiki cha awamu ya kwanza ya mwanzo ya miaka 10 na kuwezesha mafanikio haya kupatikana”.Alisema.
Kwa upande wake,Mkurugenzi mkuu wa shule hiyo ,Bw.Machage Kisyeri,aliwapongeza wahitimu kwa kufikia hatua hiyo na aliwataka watumie elimu waliyoipata kujipanga zaidi kwa masomo ya sekondari ambayo yanawakabili mbele yao. “Maisha sio lelemama mnapaswa kupambana zaidi katika hatua inayofuatia na kuhakikisha msingi wa elimu imara tuliyowapatia unawaongoza kuelekea katika kupata mafanikio ya kitaaluma popote pale mtakapokwenda”Alisisitiza.
Aliongeza kuwa shule imejizatiti kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha elimu nchini ambapo kuanzia mwezi Januari mwakani itaanza kutoa elimu ya sekondari katika shule yake mpya iliyojengwa sehemu ya Mataya wilayani Bagamoyo katika mkoa wa Pwani.
Kuhusiana na changamoto wanazokabiliana nazo alisema kuwa zipo changamoto za kawaida kinachotakiwa ni ushirikiano baina ya wazazi,walimu,na wadau wanaosimamia elimu ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana na elimu ya Tanzania inazidi kupanda “Walimu wakiwezeshwa vizuri na kupewa ushirikiano wa kutosha naamini shule nyingi za Tanzania zitatoa elimu bora kwa kuwa tunao walimu wengi wazuri ambao wakitumiwa ipasavyo tutasonga mbele”.Alisema.