Bukobawadau

SERIKALI MKOANI GEITA YAJIPANGA KUTATUA KERO YA MAJI

Serikali Mkoani Geita imejipanga kutatua kero ya maji kwa wananchi inayowakabili wananchi kwa muda mrefu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel ametoa kauli hiyo alipotembelea miradi ya uzalishaji wa maji inayosimamiwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Geita, GEUWASA.
Amesema serikali imedhamiria kuona mji wa Geita unakuwa na maji ya kutosha ambapo kwa sasa kuna tanki lenye Mita za ujazo 1200 na kwamba zipo jitihada za kuweka pampu itakayosaidia kuongeza maji kwenye tanki hilo ili kuweza kuongeza zaidi uzalishaji wa maji kwa maeneo ya mji huo.
Aidha, amewataka wataalam wa Maji kuhakikisha wanatoa ushauri kwa Serikali Kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo na pia kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kwa kuwa wanautaalam mkubwa kwenye Sekta ya maji.
 Naye Katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshugulikia masuala ya Bonde la Ziwa Victoria Dr Ali Said Matano amesema mji wa Geita utanufaika na awamu ya tatu ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ufadhili wa Benki ya Afrika(ADB).
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Geita, GEUWASA Bw Joseph Mwita amesema mahitaji ya maji mjini Geita ni Mita za ujazo 15160 na kwamba maji yanayozalishwa ni Mita za ujazo kati ya 3 500 hadi 4000.
Akiwa katika Ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ametembelea chanzo cha maji cha Nungwe ambacho kiko ziwa victoria, mitambo ya kusafisha maji nyankanga, tanki la maji mjini Geita lenye uwezo wa kutunza maji zaidi ya mita za ujazo 120 elfu na ujenzi wa tanki la maji Kagera.
Next Post Previous Post
Bukobawadau