Bukobawadau

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWAASA WAJUMBE WA KAMATI KUU CCM MKOA KUACHA MALUMBANO NA MIGOGORO ILI CHAMA KIISIMAMIE SERIKALI KUTEKELEZA ILANI

Na: Sylvester Raphael
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa katika siku yake ya pili ziarani Mkoani Kagera afanya kikao na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa na kuongea na wajumbe wa kamati hiyo ambapo amewakumbusha wajibu wao wa kuhakikisha CCM inawafikia wananchi hadi ngazi za chini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye ni mlezi wa CCM mikoa ya Kagera na Kigoma katika kikao cha Kamati Kuu CCM mkoa aliwataka wajumbe kuhakikisha chama hicho kinakuwa mkombozi na kuleta matumaini kwa wananchi kwa kuisimamia Serikali kutekeleza ilani na kutimiza ahadi zilizohaidiwa na chama hicho mwaka 2015.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mlezi wa CCM mkoa wa Kagera aliwakumbusha Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanawasilisha taarifa za Wilaya zao za utekelezaji wa ilani katika vikao vya Halmashauri Kuu za Wilaya kama Mkuu wa Mkoa wa Kagera anavyofanya kwa kuwasilisha taarifa ya utekeklezaji wa ilani ya mkoa katika Kikao cha Kamati kuu CCM Mkoa.
Akitoa ufafanuzi juu ya uwasilishwaji wa taarifa hizo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya wanantakiwa kuandaa taarifa hizo na Wakuu wa Wilaya kuziwasilisha katika Vikao vya Kamati Kuu za Wilaya ili Chama (CCM) ambacho kimeiweka Serikali madarakani kiweze kuisimamia vizuri Serikali yake. Aidha alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera kusimamia agizo hilo kwa Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa wa Kagera.
Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka wajumbe wa Kamati Kuu CCM Mkoa kuacha malumbano na migogoro katika chama badala yake washikamane na kushirikiana kuhakikisha CCM inatekeleza ahadi zake kwa wananchi pia na kuisimamia Serikali kutekeleza ilani katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera.
Vile vile Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za Wilaya kuhakikisha wasimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ya kutosha na kushirikiana na Wenyeviti wa Halmashauri zao kutenga fedha za kuchimba visima vya maji vifupi na virefu kwa wananchi ili kumtua mama ndoo kichwani.
“Nitashangaa kama Mkurugenzi atashindwa kusimamia mabilioni ya fedha za miradi ya maji tulizo waletea ili wananchi wake wapate maji, pia nafurahi Wenyeviti wa Halmashauri mpo hapa hebu shirikianeni kukusanya mapato katika Halmashauri zenu na mtenge angalau million 20 kwajili ya kuchimba visima vya maji vifupi wananchi wetu wapate maji.” Alifafanua Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaeleza wajumbe wa Kamati Kuu CCM Mkoa kuwa Kamati Kuu CCM taifa ilimwagiza kutilia mkazo kwenye kilimo hasa kilimo cha kahawa Kagera ambapo alisema kuwa anazo taarifa kuwa Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani humo baadhi vimelipa malipo ya pili na vingine bado vinaendelea kukamilisha huku vikijiandaa na msimu mpya.
“Zao la kahawa ni zao pendwa Mkoani Kagera wahimizeni wananchi waendelee kulima kwa nguvu zao hili lakini pia sisi wajibu wetu ni kuimalisha kilimo hiki na nawaagiza viongozi kujipanga na msimu mpya ujao ili tusije kuingia katika matatizo yaliyotokea msimu uliopita.” Aliagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Mwisho Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka wajumbe wa Kamati Kuu CCM Mkoa wa Kagera kulinda mali za chama na kuacha kugombania mapato yanayotokana na baadi ya vitega uchumi vya chama hicho kwani wote wanajenga nyumba moja.
Next Post Previous Post
Bukobawadau