PINDA AKAGUA ENEO WATAKAOHAMISHIWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO HANANG
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanang Rose Kamili (kushoto) alipokwenda kukagua eneo watakalohamishiwa waathirika wa Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang tarehe 5 Januari 2024.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga akimueleza jambo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda wakati akikagua eneo watakalohamishiwa waathirika wa Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang tarehe 5 Januari 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ofisini kwake alipokwenda kukagua eneo watakalohamishiwa waathirika wa Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang tarehe 5 Januari 2024.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga akisisitiza jambo mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda pamoja na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara Wenceslaus Mtui wakati alipokwenda kukagua eneo watakalohamishiwa waathirika wa Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang tarehe 5 Januari 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, WANMM MANYARA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda ametembelea na kukagua eneo limepimwa viwanja kwa ajili ya kuhamisha waathirika wa Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang.
Mhe Pinda amefanya ukaguzi huo tarehe 5 Januari 2024 akiambatana na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga pamoja na viongozi wengine wa mkoa pamoja na wa wilaya ya Hanang.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeshiriki pamoja na na wadau wengine katika zoezi la kutathmini kiwango cha uharibifu uliotokana na maafa yaliyotokea tarehe 3 Des 2023 na kushauri juu ya maeneo yanayoweza kutumika kuhamisha waathirika.
Akiwa katika eneo hilo tarehe 5 Januari 2024 wilayani Hanang mkoani Manyara, Mhe Pinda alielezwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara Wenceslaus Mtui kuwa, jumla ya ekari 100 kutoka Jeshi la Magereza kwenye eneo la Warret zimetolewa kwa ajili ya waathirika.
Tarehe 21 Desemba 2023 Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenister Mhagama alielekeza wizara ya Ardhi kuhakikisha viwanja kwa ajili ya kuhamisha waarhirika maeneo ya Gendavi, Jorodom, Ganana na Katesh - Hanang vinapimwa na kukamilika kabla ya Des 31. 2023
Kwa mujibu wa Mtui, zoezi la upimaji viwanja katika eneo hilo lililotolewa na Jeshi la Magereza umefanyika kwa weledi na kukamilika ndani ya siku saba ambapo jumla ya viwanja 269 vilipimwa na kupandwa mawe.
Amesema, viwanja vilivyopimwa viko katika mgawanyo wa makazi 226, makazi na biashara 26, pamoja na huduma za jamii 17. Hata hivyo, suala la uandaaji hati linasubiri maelekezo pamoja na orodha rasmi iliyohakikiwa na kuidhinishwa na mamlaka husika.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameishukuru Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya kazi kubwa ya kupima viwanja na kuweka mawe katika kipindi cha muda mfupi.
" Nikushukuru wewe pamoja na wizara yako na utufikishie salamu kwa waziri wa ardhi kwa kufanya kazi ndani ya muda mfupi na siyo tu kupima bali na kuweka mawe" alisema Queen Sendiga.
Kwa upande wake Naibu Waziri Pinda amesema, wizara yake imeshafanya jukumu lake la msingi la kupima eneo hilo na kutoa wito kwa TARURA kuharakisha uchongaji barabara kuelekea eneo hilo ili kurahisisha usafirishaji vifaa.
"Nimuombe Mkurugenzi wa TARURA na kupitia wizara yake waone umuhimu wa kuharakisha barabara zifike hadi site" alisema Mhe Pinda.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanang Rose Kamili ameishukuru wizara ya ardhi kwa kazi nzuri ya upimaji eneo wanalohamishiwa waathirika wa mafuriko ya maporomoko ya tope na mawe
Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang yamesababisha jumla ya wananchi 87 miili yao kupatikana baada ya kupoteza maisha na majeruhi kuendelea kupata matibabu katika hospitali ya Hydom, wilaya na mkoa. Sambamba na hilo baadhi ya wananchi wanaendelea kupata hifadhi katika maeneo ya taasisisi za elimu zilizopo Katesh baada ya makazi yao kuharibiwa.
----------MWISHO-------