DKT. MSONDE AHIMIZA KASI UJENZI JENGO LA WIZARA
PICHA NA WU
DKT. MSONDE AHIMIZA KASI UJENZI JENGO LA WIZARA
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde amemtaka Mkandarasi Vikosi vya Ujenzi anayejenga jengo la Wizara hiyo kuhakikisha anapanga ratiba maalum ya utekelezaji wa mradi huo ili iendane na kasi ya muda wa nyongeza aliopewa.
Maelekezo hayo ameyatoa Septemba 26, 2024 wakati Naibu Katibu Mkuu huyo pamoja na Menejimenti ya Wizara hiyo ilipokagua jengo la Wizara ya Ujenzi, katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma na kusisitiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha jengo hilo linakamilika kwa ubora na kwa wakati.
“Wekeni mpango mkakati maalum wa utekelezaji wa kazi zenu ili uendane na muda mliopangiwa, hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huu kwani kila kitu mnacho, kumbukeni hakutakuwa tena na muda wa nyongeza”, amesema Dkt. Msonde.
Aidha, Dkt. Msonde amemtaka Mhandisi Mshauri anayesimamia mradi huo, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha anasimamia mara kwa mara mradi huo ili kuangalia maendeleo yake na kubaini changamoto zitakazojitokeza mapema ili kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Aidha, ameagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi kwa uaminifu na weledi ili kuweza kuaminika na kuweza kupata kazi nyingi zaidi ambazo zitatangaza Taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Meneja Mradi kutoka Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi, Stanslaus Mkude amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Msonde kufanya kazi kwa ubora na kuweka ratiba maalum itakayosaidia kumaliza mradi huo kwa wakati.
Ameeleza kuwa Jengo hilo limefika asilimia 76 na kufafanua kuwa kazi zinazofanyika sasa hivi ni kumalizia uwekaji wa Tiles na kufunga vioo katika maeneo mbalimbali ya jengo hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi