Bukobawadau

BOB JUNIOR; MSANII ‘ALIYEVAA VIATU’VYA BABA YAKE

Samaki mkunje angali mbichi, akishakauka atavunjika. Tafsiri ya usemi huu haimaanishi kutumia nguvu, badala yake maarifa yatumike kwa namna yoyote ili kumfundisha mtoto afuate mstari mwema wa maadili, utakaokuwa neema katika maisha yake ya baadaye.
Ipo mifano mbalimbali ya wasanii wakongwe waliotembea juu ya methali hiyo ya Kiswahili kuwajenga watoto wao mapema kwa kuwafundisha na kuwarithisha fani zao na sasa watoto hao ni mastaa katika muziki. Baadhi ya wakongwe hao ni pamoja na Hamza Kalala aliyemfundisha na kumrithisha kazi ya muziki mtoto wake Kalala Junior, Zahir Ali Zoro aliyemrithisha Banana Zoro, pia Mahunda Zoro, hata Nguza Vicking aliyewarithisha watoto wake Papii Kocha na Nguza Mbangu.
Katika mlolongo huo yumo pia Rahim Nanji ‘Bob Junior’ ni miongoni mwa vijana waliorithishwa mikoba na wazazi wao. Yeye alirithishwa na baba yake mzazi, mzee Nanji ambaye kwa sasa anaendesha shughuli zake za muziki wake nchini Finland.
 Mazingira hayo, yamemwezesha Bob Junior kuwa ni miongoni mwa wasanii wachache walioongeza chachu, ladha hata changamoto kwenye soko la muziki wa Bongo Fleva lililo na ushindani akifanya hivyo kupitia nyimbo zake mbalimbali na utambulisho wake wa rais wa Masharobalo.
“Baba yangu ni mtayarishaji wa muziki na hadi sasa anaimba akiwa nchini Finland, alinitengeneza na kwa juhudi baadhi ya watu hawaamini ninachokifanya,” anasema Bob na kuongeza;
“Sikuwahi kupitia mashindano wala sehemu yoyote, nilikuwa karibu sana na mzee wangu, ndiyo sababu ya mimi kuwa na uwezo wa kuandaa muziki na kuimba mwenyewe.”
Alivyouanza mwaka 2014
Wastani wa siku 50 zimepita tangu mwaka 2014 ulipoanza huku idadi kubwa ya wasanii wakitaja kipindi hicho kuwa kisicho na mafanikio.
Bob anakiri mazingira hayo huku akibainisha kwamba binafsi ameshiriki shoo tatu za ndani, kabla ya kupata mwaliko wa sherehe za Valentine Day katika Jiji la Arusha.
“Mwaka ulianza vibaya, siyo mimi peke yangu ni wengi wanasema hivyo. Nimefanya shoo moja Zanzibar na mbili pale Ukumbi wa Bilicanas, hata hivyo kuna neema inayoonekana kujitokeza baadaye kupitia mialiko ya shoo,” anasema na kuongeza;
“Mashabiki wangu wasubiri kazi nyingine mpya itakayotoka mwezi Machi, inaitwa Ukweli wangu, lakini pia naandaa video ya wimbo wa Bashasha.”
Anapokuwa na familia

Bob anaeleza kuwa huwa na furaha kila anapokutana na mtoto wake Rummy ambapo kila baada ya wiki mbili hulazimika kwenda Visiwani Zanzibar ili kumwona.
“Anaishi na mama yake, ameshatimiza umri wa mwaka mmoja, ni mwenye furaha na afya hatua inayonipa furaha katika kazi zangu,” anasema Bob.
Akizungumzia matumaini aliyonayo kwa mwanaye Bob anasema: “ Mpaka sasa sijaona dalili zozote za kipaji alichonacho, lakini anaonekana mtundu wakati wote.”
Anaongeza: “Akifikisha umri wa miaka mitatu tu, nitaanza kumfuatilia kujua kipaji chake mapema ili kumjengea msingi mzuri. Katika umri huo nahisi itakuwa rahisi kujua mwelekeo wake.”
Anapokuwa studio
Bob ni mmoja kati ya maprodyuza walioandaa kazi mbalimbali za wasanii wakubwa kupitia studio yake ya Sharobaro Records tangu ilipoanzishwa miaka minne iliyopita jijini Dar es Salaam.
“Kwa mwaka huu nimeandaa wimbo mpya wa Lady JD, utatoka mwezi Machi na mwingine wa TID, hivyo kazi ninazofanya na wasanii wakubwa ni nyingi,” anasema na kutaja changamoto akisema:
“Changamoto kubwa inayojitokeza studio ni uwezo mdogo wa wasanii chipukizi wanaokuja kurekodi, wengi wanapenda kuimba, lakini hawana uwezo kwani mara kadhaa nimekuwa nikiwarudisha ili wakafanye mazoezi zaidi kuongeza uwezo wa sauti.

Anapokuwa mfanyabiashara
Bob anasema kwa upande wake pia amekuwa akijishughulisha na biashara mbalimbali za uagizaji wa simu za mkononi, viatu pamoja na mavazi mbalimbali ya kisasa.
“Biashara hiyo nimeanza miaka kadhaa iliyopita, nimekuwa nikiifanya kwa ukaribu na mama yangu mzazi. Mafanikio kupitia biashara hiyo ni ya kuridhisha kwani hata ikitokea nimeacha kufanya muziki, lazima nitaendelea na biashara hizo,” anasema Bob.
MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau