Bukobawadau

JAGUAR;MWANAMUZIKI MILIONEA ALIYEANZA KWA KUOSHA MAGARI

Zipo baadhi ya kauli za Wahenga wa Kiswahili ambazo siyo rahisi kutimia au uhaliasia wake kuonekana kwa haraka katika maisha ya kila siku.
“Hata mbuyu ulianza kama mchicha” Kauli hii maarufu katika jamii hasa vijana wanaojihusisha shughuli ndogondogo huku wakiamini kwa kazi hiyo ipo siku wao wapata utajiri kwa kidogo wanachokipata na kuhifadhi.
Fikra hizo pia zilikuwa kichwani mwa Charles Kanyi (Jaguar), mwanamuziki kutoka nchini Kenya ambaye sasa anatikisa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kupitia nyimbo zake mbalimbali,zinazoendelea kumpa umaarufu.
Jaguar aliye miongoni mwa wanamuziki matajiri nchini Kenya kwa sasa alianza maisha ya kujitegemea kwa kufanya kazi ya kuosha magari.
Msanii huyo nyota anayedhihirisha uwezo mkubwa kifedha kwa kumiliki magari na vito vya thamani, anakiri kwamba alikuwa na maisha magumu kiasi cha kulazimika kutegemea kazi ya kuosha magari ili kupata mkate wake wa siku.
Pamoja na kuwa na uwezo mkubwa kimaisha sasa, Jaguar anasema kuwa hapendi kujionyesha kuwa yeye ni tofauti na wengine wanaomzunguka hivyo hupenda kujichanganya.
Anaeleza kuwa hali hiyo inatokana na maisha magumu aliyoishi tangu alipokuwa mdogo, baada ya kifo cha mama yake ambapo alijikuta akilazimika kulala katika daladala alizokuwa akiziosha.
Jaguar alikuwa akitembea mwendo mrefu kwenda shule, lakini kutokana na mapenzi makubwa katika elimu alikuwa akiwashawishi hata baadhi ya madereva wa daladala wammruhusu kupanda bure magari yao ili kuwahi shuleni, pia kurejea nyumbani.
Changamoto alizopitia Jaguar, zinamfanya kupenda kujiweka karibu na jamii yake licha ya utajiri na maisha ya juu anayoishi nyota huyo kwa sasa.
Mara kwa mara Jaguar amekuwa akishiriki katika shughuli na kampeni mbalimbali za kijamii kwa lengo la kuleta mabadiliko na kuwasaidia wengine wanaopitia kwenye changamoto za kimaisha.
Katika Sikukuu ya Krismasi ya mwaka jana, Jaguar alikwenda katika moja ya magerezani nchini Kenya na kusherehekea siku hiyo pamoja na wafungwa.
Akiwa amevalia sare zinazolingana na wafungwa hao, msanii huyo alishiriki chakula cha mchana na kundi hilo lililosahaulika katika jamii.
Siku zote Jaguar amekuwa na imani kwamba kila mtu ana umuhimu katika jamii, hivyo ni jukumu lake kuhakikisha anamsaidia kila anayeweza kumfanyia hivyo kadiri ya uwezo wake.
Imeandaliwa na Elizabeth Edward
Next Post Previous Post
Bukobawadau