Bukobawadau

BULEMBO: KIMBUNGA MUGASHA NA AHADI ZA KISIASA

Na Prudence Karugendo

“Mugasha” ni jina ambalo kiutamaduni Wahaya waliupatia upepo mkali, dhoruba au kimbunga, unaotokea na kusababisha maafa kwa wakazi wa eneo unalolikumba.

Ni upepo unaoangusha migomba, kuezua nyumba na nyingine kuziangusha kabisa na kuwaacha watu wa eneo husika bila chakula wala mahali pa kujihifadhi. Kwa kilugha Wahaya wanasema “Mugasha yaitema” wakiwa na maana ya kwamba Mugasha kacharuka na kuifyeka migomba.

Kwa vile chakula cha asili cha Wahaya ni ndizi, kuifyeka migomba ni sawa na kuwahukumu kifo. Ndiyo maana upepo huo unaoitwa Mugasha unaogopwa sana na Wahaya. Yaani upepo unaoangusha migomba na kuwaacha bila chakula.

Mwishoni mwa mwezi wa tatu, mwaka huu, wananchi wa kijiji cha Bulembo, Kamachumu, Muleba Kasikazini mkoani Kagera, wamepatwa na mkasa huo wa upepo mkali unaojulikana kama Mugasha.

Upepo huo umekiharibu kabisa kijiji cha Bulembo. Kawaida watu walizoea upepo mkali kuiangusha migomba tu ukiyaacha mazao mengine,  na makazi yao kubaki salama. Lakini upepo wa mara hii haukuacha chochote! Umeangusha na kung’oa kila kilichokuwa ardhini, hata magugu yaling’olewa!

Miti mikubwa ambayo kwa Kihaya inajulikana kama “ebigabiro” imeangushwa na upepo huo na mingine kung’olewa kabisa kitu ambacho si cha kawaida. Nyumba nyingi zimeezuliwa paa zake ambapo paa nyingine zilikuwa zinarushwa umbali wa zaidi ya mita 100, wakati nyumba nyingine zilikuwa zinaangushwa kabisa na upepo huo hasa zile zilizoangukiwa na miti mikubwa na kuwaacha mamia ya watu bila makazi wala chakula.

Wiki mbili zilizopita nilisafiri hadi kijijini Bulembo kujionea mwenyewe kiwango cha madhara yaliyowapata wananchi wa Bulembo. Na huu ufuatao hapa chini ndio ushuhuda nilioupata kwa wanakijiji hao huku mengine nikiyashuhudia mwenyewe kwa macho yangu.

Mtu wanayemshukuru sana wanakijiji hao ni Ansbert Ngurumo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vox Media na Mhariri Mtendaji wa Free Media. Wanamshukuru hasa kwa mambo makuu mawili wanayoyachukulia kama ya kuunusuru uhai wao.

La kwanza ni la kutumia nafasi yake hiyo ya usimamizi wa vyombo vya habari kutaarifu juu ya maafa yaliyowakumba wananchi wa Bulembo. La pili wanalomshukuru nalo ni la yeye kuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutoa msaada wa hali na mali kufuatia maafa hayo huku akizidi kuhamasisha misaada zaidi kutoka kwa wahisani wanaoguswa na matatizo yanayowapata wengine.

Jambo la kushangaza ni kwamba wakati wananchi wa Bulembo wanapatwa na maafa hayo hawakumuona mbunge wao, Charles Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini. Muda wote wananchi hao walibaki kama watoto yatima wakikimbiliwa kwa dharura na watu ambao si wawakilishi wao rasmi!

Mbunge huyo amewasili jimboni tarehe 28/4/2014,  zikiwa ni siku 30 tangu wanakijiji wa Bulembo wapigwe  na kimbunga hicho.

Siku hiyo ya Jumatatu  akazuru maeneo yaliyoathirika, lakini kwa kuwa kafika baada ya muda mrefu, kakuta maeneo mengi yameishabadilika, hakuweza kuyaona madhara halisi ya maafa yaliyowapata wananchi.

Tofauti na watu wengine waliofika Bulembo kabla yake,  tuseme ndani ya mwezi mzima uliopita, Mwijage aliondoka kijijini hapo bila kutoa msaada wowote.

Kesho yake, Jumanne 29/4/2014,  aliitisha mkutano wa hadhara kijijini hapo. Mkutano ulihudhuriwa  na maofisa pamoja na makada waandamizi wa CCM Wilaya ya Muleba,  wakiwamo Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya, maofisa wa kata na Wenyeviti wa vijiji mbalimbali.

Katika hotuba yake, mbunge huyo  alisema kwamba hajapeleka kitu Bulembo kwa sababu Serikali imekubali kutoa msaada mkubwa wa mahindi usiopungua tani 160, na shilingi milioni 60 kwa ajili ya kununulia maharage.

Alitumia fursa hiyo kuwashambulia waliomtangulia kutoa misaada Bulembo, akisema kwamba waliotoa kilo mbili mbili tu hawajafanya lolote! Akasema yeye, kwa kupitia Serikali, atatoa gunia moja moja kwa kila mtu!

Inaonekana kwamba mbunge huyo anatumia uelewa mdogo walio nao wananchi juu ya mpangilio wa mambo ya serikali kutaka kujinufaisha kisiasa. Msaada anaosema utaletwa hasemi kwamba unatoka serikalini na umecheleweshwa sana. Yeye anataka wananchi waamini kwamba kautoa yeye mwenyewe  msaada huo, wakati ukweli ni kwamba unatoka katika Mfuko wa Maafa wa Ofisi ya Waziri Mkuu, mfuko unaochangiwa na kila mwananchi kama akiba ya kujikinga na maafa.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema wananchi wa Bulembo walipaswa kupata chakula hicho cha dharura walichokiweka kama kinga ya maafa katika muda wa masaa 24 tangu walipokumbwa na kimbunga. Lakini kwa vile mbunge wao haonekani kuyatilia maanani yanayowapata wapiga kura wake,  ndiyo maana anajitokeza baada ya mwezi mzima na kujifanya anawaahidi kitu muhimu sana ambacho pengine hawakukisitahili!

La kujiuliza ni kwamba mwakilishi wa wananchi anawezaje kupata habari juu ya maafa yaliyowapata anaowawakilisha akapitisha mwezi mzima bila kwenda kuwajulia hali kwa madai ya kwamba pengine kabanwa sana na shughuli nyingine? Ni shughuli gani muhimu kuliko uhai wa anaowawakilisha?

Huo ni ushahidi tosha kwamba kwa wakati huu uwakilishi wa wananchi umegeuzwa mtaji binafsi wa wale wanaochaguliwa kuwawakilisha wananchi.

Kutumia maafa yanayowapata wananchi kujinadi kwa mbwembwe kwa malengo ya kisiasa ni jambo linalopaswa kulaaniwa kabisa na kila mwananchi mwenye akili timamu.

Na mbunge huyo anapozibeza anazoziita kilo mbilimbili, anatuhakikishiaje kuwa bila kilo hizo mbilimbili wananchi wangeweza kuishi bila mlo wowote kwa mwezi mzima wakisubiri kilo 100 kwa kila mmoja wao toka Mfuko wa Maafa wa Waziri Mkuu? Kumbe watu wanaweza kuishi kwa kula tu ahadi za wanasiasa!

Mengine niliyoyashuhudia ni kwamba msamaria mwema mmoja,  mwenyeji wa kijiji cha  Rwanda, Tarafa ya Kamachumu, Justus Mushemba, ameamua kumpa makazi ya muda Yasinta Godfrey na mtoto wake, ili kuwanusuru kwenye mvua za masika na baridi kali, kusudi wasije wakapata madhara makubwa zaidi.

Mushemba ambaye ni mtumishi wa Shirika la Posta,  anayeishi Mwanza, anasema alipata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari,  Nipashe, ITV, na Tanzania Daima, wiki mbili zilizopita kuhusu tabu anazozipata mama huyo.

Baada ya kupata taarifa hizo, aliwasiliana na Ansbert Ngurumo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vox Media na Mhariri Mtendaji wa Free Media, ambaye ndiye alikuwa anahangaika kuiomba Serikali iwasaidie wanakijiji wa Bulembo waliopatwa na maafa na baadaye kidogo akaenda Jijini Mwanza.

Wiki iliyopita Ngurumo alikuwa kijijini Bulembo, akazungumza na mwanamke huyo, akampa taarifa za msaada huo.

Kwa mujibu wa Ngurumo, walijitokeza watu wawili kumpa hifadhi mama huyo. Mmoja anaitwa Rutashobya Rutashobya mwenyeji wa Kanazi anayeishi Dar es Salaam, na mwingine ni Justus Mushemba mwenyeji wa Kamachumu anayeishi Mwanza. Kila mmoja kwa wakati wake, baada ya kuguswa na habari za mama huyo, alisema kwamba yupo tayari nyumba yake iwahifadhi mama na motto wake kwa muda hadi mumewe,  Godfrey, atakapokuwa amerejea na kukarabati au kujenga upya nyumba yao,  wakapata makazi imara na salama. Msaada walioupata  ni wa makazi na chakula kutoka shambani walikohifadhiwa.
Yasinta alikubali,  na alichagua kuishi katika nyumba iliyoko kijjini Rwanda, kilomita zipatazo 10 kutoka Bulembo. Tayari ameishafanya mawasiliano na Mushemba kwa ajili hiyo.



Miongoni mwa waliosaidia wanakijiji hao ndani ya siku 30 zilizopita, ni pamoja na Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka,  aliyetoa kilo 1250 za maharage; Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Conchesta Rwamlaza, aliyetoa kilo 1,100 za mchele, na Ansbert Ngurumo aliyetoa kilo 1,100 za mchele.

Wakati anatoa msaada wake, mbunge Conchesta Rwamlaza, alisema kwamba, kwa usemi wa kilugha, ajuna akanyonyi akajuna kakyaharara, wenye maana ya kwamba anayetaka kumnusuru ndege anapaswa afanye hivyo wakati ndege akiwa bado na uwezo wa kuruka, lakini ndege akishashindwa kuruka maana yake ni kwamba huyo kafa, kujaribu kumsaidia ni kazi bure.

Wengine waliosaidia katika maafa ya Bulembo ni Shirika la Kolping la Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiluteri, Parokia ya Rutabo ya Kanisa Katoliki, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera, na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Muleba.

KITUKO:
Akihutubia mkutano wa hadhara, Mbunge Mwijage aliwashambulia waandishi wa habari eti wamewadhalilisha wanakijiji wa Bulembo, na wamemuaibisha yeye kwa kuchapisha mitandaoni na magazetini picha za kuonyesha nyumba mbovu za kijijini, na kuonyesha taifa kwamba wanakijiji wa Bulembo ni maskini sana!

Alifikia hatua ya kusema kuwa Ngurumo anapaswa ashitakiwe binafsi kwa kuwa amechapisha picha ya Yasinta Godfrey na mtoto wake, na kwamba amewadhalilisha mama huyo na mumewe!

Wakati akiyasema hayo, baadhi ya wananchi walikuwa wanaguna. Kikundi kidogo cha makada wa CCM kilikuwa kinamshangilia. Na ilionekana ndio msaada kilioamua kuutoa kwa wananchi wa Bulembo kikundi hicho cha makada wa CCM! 

Mwijage alitumia fursa hiyo kuomba kura za ubunge mwaka 2015, akisema yeye ni tajiri ana pesa, si kama wengine wanaoleta misaada uchwara  kuwa wanawasaidia wananchi.
Kabla ya mbunge kuhutubia, Katibu wa CCM Wilaya ya Muleba alikuwa ametahadharisha kuwa mkutano ule si wa kisiasa, na kwamba usitumiwe kisiasa. Lakini hotuba ya mbunge ilijikita katika kufanya siasa badala ya kuwafariji waliopata maafa.

Baada ya mbunge kuondoka, bila kutoa msaada wowote, wanakijiji walikusanyika katika makundi kadhaa na kusema hawakuridhishwa na kauli za udhalilishaji zilizotolewa na mbunge wao  dhidi ya Ngurumo, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu, mashirika  mbalimbali pamoja na Serikali  ili watoe usaidizi Bulembo.
Walisema Ngurumo ameshafika Bulembo mara tatu kupeleka msaada, kutoa taarifa na kusalimia wananchi, na mara zote alipozungumza na wananchi hakubeza mtu, wala hakushambulia mtu.

Wananchi wa kijiji cha Bulembo walisema mbunge wao alipaswa kuvishukuru vyombo vya habari vilivyotangazia taifa juu ya maafa hayo, kwani Serikali isingetoa msaada bila taarifa za mara kwa mara kupitia vyombo vya habari. Eti hiyo ni kutokana na serikali kutokuwa na uwezo wa Kimungu wa kuona kinachotendeka  kila sehemu.

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau