Bukobawadau

Man Utd na Schalke 04 Rooney kupumzishwa

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson atampumzisha Wayne Rooney katika mchezo wa nusu fainali ya Ubingwa wa Ulaya mzunguko wa pili dhidi ya Schalke 04 siku ya Jumatano.
Wayne Rooney

Wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-0 waliyopata katika mchezo wa mzunguko wa kwanza na huku wakikabiliwa na mchezo muhimu wa kuamua hatma ya ubingwa wa England dhidi ya Chelsea siku ya Jumapili, Ferguson anajipanga kupumzisha baadhi ya wachezaji wa kikosi chake cha kwanza.

Dimitar Berbatov huenda akaanza pamoja na Michael Owen katika safu ya washambuliaji wawili.

Fabio da Silva hata hivyo hatacheza, kutokana na kuumia mguu.

Mbrazili huyo aliumia siku ya Jumapili, Manchester United ilipolazwa bao 1-0 na Arsenal, matokeo yanayoufanya mpambano baina ya Man United na Chelsea katika uwanja wa Old Trafford kuwa muhimu zaidi kwa kuweka wazi nani hasa atakuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la ubingwa msimu huu.

Manchester United inaongoza kwa pointi tatu nyuma ya Chelsea huku zikiwa zimesalia mechi tatu kabla msimu kumalizika, lakini wakipoteza mchezo huo siku ya Jumapili, itawafanya Chelsea kushikilia usukani wa ligi huku wakikabiliwa na michezo miwili rahisi ya kumalizia dhidi ya Blackburn nje na Blackpool nyumbani.

Wakilifahamu hilo, ndio maana Ferguson atapumzisha wachezaji kadha nyota dhidi ya Schalke ya Ujerumani katika mchezo wa Jumatano.

Manchester United waliizidi kwa kila hali Schalke katika mchezo wa kwanza juma lililopita, na kufanikiwa kushinda kwa mabao 2-0.

Next Post Previous Post
Bukobawadau