Bukobawadau

Nape Nauye aumbuliwa na Fred Mpendazowe

VITA ya maneno kati ya Chadema na CCM jana imechukua sura mpya baada ya Fred Mpendazoe kumtaja Katibu Mwenezi na Itikati wa CCM, Nape Nauye kuwa miongoni mwa vigogo sita walioanzisha Chama cha Jamii (CCJ) .Mpendazoe alitoboa siri hiyo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mbamba Bay kilichopo katika wilaya mpya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Mpendazoe alijitoa CCM Machi 30, mwaka jana akiwa Mbunge wa Kishapu na kujiunga na CCJ Aprili 16, mwaka huo kabla ya kuhamia Chadema, baada ya CCJ kukosa sifa na kufutwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Mbamba Bay, mkoani Ruvuma jana, Mpendazoe alisema ameamua kuliambia taifa ukweli kuhusu Nape, ili umma uepuke kudanganywa na propaganda za kijana huyo
.“Kelele zote anazopiga Nape kuitetea CCM ni za kinafiki kwani aliwahi kukigeuka chama hicho na kushiriki katika mipango yote ya kuanzisha CCJ”.Hata hivyo, Nape alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusiana na madai hayo ya Mpendazoe, hakukataa wala kukubali kushiriki kuanzishwa CCJ, badala yake alisema, "Cha msingi waeleze (Chadema) CCJ ilikufaje, wasiseme ilizaliwaje, maana kuzaliwa ni sherehe na kufa ni kilio.” Nape ambaye hakusema lolote kama kombora la Mpendazoe ni la kweli aliwageuzia kibao Chadema akisema, "Pamoja na hayo yote, waache (Chadema) kubaka demokrasia."

Alifafanua akisema "Watanzania walipiga kura kuichagua CCM iwaongoze kwa miaka mitano ijayo, sasa wanaposema tutaandamana nchi nzima ili serikali iondoke kabla ya muda huo, huku ni kubaka demokrasia na ni uhaini."Mpendazoe alisisitiza kuwa Nape alishiriki katika kuandaa na kuandika katiba na miko ya uongozi ya CCJ, kutafuta fedha za kukuza chama na jengo la kuweka ofisi za chama hicho.

Alisema Nape alilitekeleza vizuri jukumu hilo na kufanikiwa kuipata katiba ya chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC, ambacho ndiyo kilitumika kwa kiasi kikubwa kuandaa katiba ya CCJ.Alisema yeye, Nape na vigogo wengine aliosema atawataja muda ukifika walifanya vikao vyote vya siri hadi wakaanzisha chama hicho cha CCJ.

“Tulifungua mtandao maalumu wa kuwasiliana kwa internet, ambao baadaye wenzangu waliufuta baada ya kubadili mawazo dakika za mwisho. Lilipotulazimu kukutana mimi na Nape tulipendelea kukutana katika eneo la vinywaji pale Mlimani City, jijini Dar es Salaam”.Alisema walifanya hivyo ili wasitiliwe shaka na maafisa usalama wa taifa waliopewa kazi ya kupeleleza wanaCCM waliohisiwa kutaka kuanzisha chama kipya.

“Nape alibadili mawazo ya kutaka kuihama CCM baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, kwa kuwa alikuwa na uchu wa madaraka ,” aliongeza. Alisema Nape aliisaidia CCJ kwa kukipa siri nyingi ikiwamo mambo yaliyokuwa yakijadiliwa kwenye mikutano ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) na hata vikao vilivyokuwa vikifanyika katika Ofisi Ndogo ya CCM iliyopo Lumumba.“Nape pia alitupa siri kwamba baadhi ya walioanzisha CCJ walikuwa wanakaribia kufukuzwa kwani katika mkutano wa NEC, majina ya baadhi yao yalitajwa na kujadiliwa kwenye kikao hicho.'

Tuhuma za Chadema dhidi ya Nape na majibu ya Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM, ni mwendelezo wa siasa za jino kwa jino za kurushiana makombora yaliyobeba tuhuma nzito ndani yake.

Mei 12 mwaka huu Nape alimtaka Dk Slaa kuliomba radhi Bunge, huku Chadema nayo ikimtaja Nape kwamba ni mtuhumiwa wa ufisadi wa EPA uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo Sh133 bilioni zilikwapuliwa.
Tuhuma hizo kutoka kila upande, zimekuja baada ya Nape kutaja alichokiita unafiki wa Dk Slaa kwa kushinikiza kulipwa mshahara wa Sh7.5 milioni na Chadema, wakati alikataa mshahara wa Sh7 milioni alipokuwa mbunge akidai ni mkubwa na uliwanyonya Watanzania.

Katika mkutano wake wa hadhara siku hiyo Nape alimtaka Dk Slaa kuliomba radhi Bunge na wabunge kwa kile alichoeleza kuwa alipokuwa Mbunge wa Karatu, alichochea chuki kwa wananchi dhidi ya taasisi hiyo.
"Najua Chadema watakuwa wanajibu, lakini nasema msimamo wangu uko mbele zaidi kwamba Dk Slaa aliombe radhi Bunge na wabunge, kwani alichochea chuki kwa wananchi dhidi ya Bunge, halafu yeye anakuja kuchukua mshahara zaidi ya ule aliojidai kuukataa. Huu ni unafiki," alisisitiza Nape.

Nape alisema Dk Slaa ni Padre hivyo pia alipaswa kuungama kwa Mungu kwa kutokuwa mkweli ndani ya dhamira yake."Bahati nzuri Dk Slaa ni Padre, namshauri pia amwombe radhi Mungu, kwani amekuwa akipita mitaani kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kumbe naye hana maadili yoyote," aliongeza Nape.

Wakati Nape akitoa shutuma hizo dhidi ya Dk Slaa, siku hiyo Mei 12, Chadema aliitisha mkutano na waandishi wa habari ambako licha ya kufafanua kuhusu mshahara wa Katibu Mkuu huyo na ununuzi wa magari, ilimwita Nape kuwa ni 'Vuvuzela' na kwamba hana sifa ya kuinyooshea kidole Chadema.

“Tuna ushahidi wa kutosha kuwa mmoja wa watu walionufaika na fedha za EPA kupitia kwa Jeetu Patel ambaye ameeleza vizuri jambo hili katika maelezo yake mbele ya kamati ya Rais,” alisema Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu.(usikose kutembelea bukobawadau blogspot kila siku)
Next Post Previous Post
Bukobawadau