Bukobawadau

Chenge kushitakiwa juu ya sakata la Rada

TIMU ya wabunge walioenda nchini Uingereza kufuatilia malipo ya rada kwa Serikali ya Tanzania imekabidhi ripoti yake kwa Spika wa Bunge inayopendekeza mambo mawili, ikiwamo kushtakiwa kwa wahusika wa sakata hilo hapa nchini.Timu hiyo ya wabunge wanne ikiongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai, ilimkabidhi ripoti hiyo kwa Spika Anne Makinda jana mchana.

Wajumbe wengine wa timu hiyo ni Angellah Kairuki (Viti Maalumu-CCM), Mussa Zungu (Ilala-CCM) na John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP).

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao waliwaeleza waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa imegundua madhambi ya kutisha katika sakata la ununuzi wa rada hiyo ya kijeshi yanayoweza kuwatia hatiani wahusika.

Ingawa wajumbe hao hawakuwataja watuhumiwa hao kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), ni mtuhumiwa namba moja na aliyekuwa Gavana wa BoT, Dk Idrisa Rashid.

Wakati wa uchunguzi wa sakata hilo, Kampuni ya SFO ilibaini zaidi ya Dola za Marekani 1.2milioni kwenye akaunti ya Chenge iliyoko katika kisiwa cha Jersey nchini Uingereza. Lakini alipohojiwa na waandishi wa habari, Chenge alisema 'hivi ni vijisenti tu'

"Miongoni mwa mapendekezo yake (ripoti) kwa Serikali ni kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote waliohusika kwenye ufisadi huo," alisema mmoja wa wajumbe wa timu hiyo.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa imeweza kufichua mlolongo wa kashfa na njama ambazo zilitengenezwa nchini Uingereza ili kufunika uovu huo ambao ni wizi dhidi ya fedha za Watanzania.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, timu hiyo ilisema, mbali na kupendekeza wahusika katika sakata hilo washtakiwe, walitaka pia Bunge na Serikali kushirikiana kwa karibu hadi fedha ambazo Tanzania inazidai kutoka Kampuni ya BAE System, zipatikane.

Cheyo, mmoja wa wajumbe wa timu hiyo, hakuwapo katika mazungjmzo hayo na waandishi wa habari jana.

Wabunge hao walisema katika safari yao wamegundua mengi ikiwa ni pamoja na namna uovu huo wa kifisadi ulivyozimwa ili dunia isifahamu.

Angellah alisema kuwa timu hiyo ya wabunge ilibaini pia kuwa Serikali ya Tanzania ilikuwa imekatazwa na SFO isiwachukulie hatua watuhumiwa wa hapa nchini kwa sababu ingekuwa ni mwingiliano wa kesi mahakamani.

Alisema kwa sasa ambapo tayari mahakama ya Uingereza imetoa hukumu, Tanzania iko huru kuwachukulia hatua wahusika. Pamoja na hali hiyo, alisema nguvu kubwa kwa sasa ielekezwe katika kuiwezesha Tanzania kupata fedha hizo bila mizengwe.

Alisema kama Serikali ya Tanzania inataka kuwashtaki inapaswa kupata pia ushahidi wa SFO ambao waliutumia kuibana BAE hadi ikaamua irejeshe fedha zote.

Kuhusu uwezekano wa kuwaunganisha maofisa wa BAE kwenye kesi hiyo, Ndugai alisema kuwa tatizo ni kwamba waliohusika kwenye mpango huo tayari wameondolewa kwenye kampuni hiyo.

Zungu alisema mkakati wao ni kwamba iwapo kampuni ya BAE haitatoa fedha hizo hadi Desemba mwaka huu, Serikali ya Tanzania ifungue upya mashtaka nchini Uingereza.

Kwa upande wake, Ndugai alianza kwa kuelezea lilikoanzia sakata hilo, akisema: "kama mnavyojua Desemba 20 mwaka jana mahakama nchini Uingereza ilitoa hukumu ambayo iliiadhibu kampuni ya BAE kulipa fidia ya paundi 29 milioni kwa Tanzania."

Alisema Kampuni ya Kuchunguza Rushwa kubwa kubwa nchini Uingereza ya (SFO) ndiyo iliyofungua mahakamani kesi hiyo. Ndugai alisema kwa kuwa BAE ilibaini kuwa shtaka hilo lilikuwa ni zito na lingeweza kuharibu sifa ya kampuni hiyo duniani, walifanya mpango wa kesi hiyo kuzungumzwa nje ya mahakama na kufanikiwa.

Wakiwa nje ya mahakama, Ndugai alisema BAE walitengeneza mkataba na kusema kwamba watarejesha fedha zote ambazo Tanzania ilinunulia rada hiyo pamoja na fidia.

"Yaani walifanya kana kwamba rada hiyo Tanzania imepewa bure. Maana walinunua kwa pauni 28 milioni na sasa wanatoa pauni 29.3 milioni," alisema Ndugai. Alifafanua kuwa mkataba huo ulikuwa ni wa kufunika aibu na uliandikwa na mwanasheria wa BAE huku ukieleza kuwa fedha hizo zitatolewa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ili yatoe huduma za kijamii.

Alisema hata kabla kesi hiyo haijaenda mahakamani, walitoa mapendekezo ya fidia itakayopatikana iletwe nchini ili kununua madawati na kujenga nyumba za walimu kwa kuwa waathirika ni Watanzania.

Baada ya makubaliano hayo ya nje ya mahakama, Ndugai alisema SFO na BAE walikubaliana kesi iliyoko mahakamani ijulikane kuwa ni ya kosa la kushindwa kuweka vizuri kumbukumbu.

Alisema SFO na BAE wakaingia mkataba wa kufunga faili la uchunguzi kuhusu kashfa hiyo ikiwa na maana kwamba uozo uliofanyika hautatolewa kwa namna yoyote kwa chombo chochote.

Ndugai alizidi kueleza kuwa hii ni njama kati ya SFO na BAE ya kutotaka madhambi yaliyofanywa katika ununuzi huo wa rada yasiwekwe hadharani na dunia ikafahamu.

Hata hivyo, Ndugai alisema kamati yake imegundua ujanja huo na kwamba kitendo cha kusema fedha hizo ziende kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kuisaidia jamii, ni njia ya kuzitumia wao wenyewe.

"Wao wanataka ionekane BAE wametoa msaada halafu wafanye safari za kuja nchini kwa ndege na walipane posho halafu mwisho wa siku fedha nyingi watatumia wao," alilalamika Ndugai.

Ndugai alisema fedha hizo zitolewe kwa Serikali ya Tanzania na zisimamiwe na Bunge katika kutengeneza madawati na nyumba za walimu na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) aweze kuzikagua.

"Zikitolewa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, CAG hataweza kuzikagua na hata matumizi yake yakipindishwa hakuna namna ya kuwabana wahusika," alisema Ndugai.

Akizungumzia kuhusu safari yao ya Uingereza, Zungu alisema walichogundua ni kwamba BAE ilifanya mchezo mchafu kuanzia ununuzi wa rada hadi kuficha madhambi yake kwa kutaka kesi izungumzwe nje ya mahakama.

Taarifa zao kuvuja
Alilalamika kuwa hata baadhi ya wabunge wa upinzani waliozungumzia suala hilo juzi, ilitokana na kuvuja kwa taarifa za ripoti yao.

Hakumtaja mbunge huyo wa upinzani, lakini John Mnyika ndiye aliyeliambia Bunge kuwa fedha hizo zisipelekwe serikalini kwa sababu walishindwa kuzisimamia na wala hawakuomba washirikishwe kwenye kesi hiyo.

Zungu alilalamika kuwa miongoni mwa lawama dhidi ya SFO ni kutoshirikisha Tanzania kwenye kesi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa iliwasiliana na Takukuru ili kupata ushahidi ambao uliisaidia kuibana BAE.


Lakini akamsifu Jaji aliyeamua kesi hiyo kwa sababu alisisitiza kuwa dhuluma hiyo ilikuwa ni dhidi ya wananchi wa Tanzania hivyo lazima fedha hizo zipelekwe moja kwa moja kwa manufaa ya waathirika hao.

Zungu alisema kuwa Jaji aliamua itozwe fidia ndogo ya paundi 500,000 katika fedha hizo ili zigharimie kesi hiyo.

Zungu alionya kuwa kama mshikamano hautakuwapo katika suala hilo, BAE itatumia fedha za Watanzania na kujigamba imetoa msaada.

Alisema katika Bunge la Uingereza, Tanzania inasifiwa kuwa imekuwa ikitumia vizuri fedha za misaada na wanaridhika iendelee kupewa misaada.

"Sasa kitendo cha kutoa fedha hizi, zilizotoka mikononi mwa Serikali ziende kwa asasi za kiraia kwa madai kwamba hazitatumika vizuri ni udhalilishaji mkubwa," alieleza Zungu.

Alisema kamati hiyo ilipanga kukutana na Mkurugenzi wa SFO, Richard Agaman, lakini alikataa huku akisema yuko tayari kuwasiliana na balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Zungu alisema balozi huyo alisema mkurugenzi huyo wa SFO aliomba radhi kwa kutoshirikisha Serikali ya Tanzania kwenye kesi hiyo.(habari kwa niaba ya gazeti la mwananchi)
Next Post Previous Post
Bukobawadau