Bukobawadau

Maaskofu: Hotuba Ya Rais Kikwete Nzito

MAKANISA nchini yamesema hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoto juzi katika baraza la idd ni nzito na kwamba, kama angekuwa anatoa hotuba kama hizo, matatizo mengi ya nchi yangekuwa yamepata ufumbuzi.Katika baraza hilo pamoja na mambo mengine, Rais Kikwete akijibu risala ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, (Bakwata) alizungumzia mambo muhimu kuhusu taifa ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kadhi, viongozi wa dini na biashara ya dawa za kulevya na udini katika siasa.

Jana, kwa nyakati tofauti wakizungumzia hotuba hiyo baadhi ya maaskofu akiwemo Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Yuda Thedeus Ruwai’chi, alimpongeza mkuu huyo wa nchi kwa hotuba hiyo nzito.

Ruwai'chi
Ruwai'chi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Mwanza alisema: “Kauli kama za jana (juzi) zingekuwa zinatolewa mara kwa mara, masuala mengi ya nchi yangeshapata ufumbuzi, nimesoma hotuba hiyo kwenye magazeti, lakini nitafurahi sana nitakapopata hotuba yenyewe niisome kwa mtiririko wake”.

Mahakama ya Kadhi
Kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi, Askofu Ruwai’chi aliunga mkono kauli ya Rais Kikwete kuhusu waumini hao kuanzisha mahakama hiyo wenyewe na kusisitiza kuwa Waislamu ni watu wazima wasiotaka kubebwa na mtu yeyote ili kufanikisha mambo yao.

Askofu Ruwai'ch alifafanua: “Wakianzisha wenyewe Mahakama ya Kadhi hakuna anayewazuia..., kwa sababu ni dini isiyohitaji kubebwa, waanzishe chombo chao kisicho cha Serikali, wakiendeshe kwa fedha zao wenyewe”.
Hata hivyo, alisema, bado Serikali inaonekana kuwa na kigugumizi juu ya suala la mahakama hiyo, ndiyo maana kuna kauli zinazogongana.

Rais huyo wa Tec badala yake alisema, “Mara anasema suala lipo kwa Waziri Mkuu, mara waanzishe wenyewe..., wasijing’ate, wawaambie tu kuwa waanzishe mahakama yao kwa fedha zao na waiendeshe wenyewe”.

Utaifishaji wa shule
Akizungumzia madai ya kurejeshwa kwa shule zilizokuwa zikimilikiwa na taasisi za dini na baadaye kutaifishwa wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Ruwai’chi alisema ingekuwa ni kulalamika, kanisa lingekuwa la kwanza kwa sababu mamia ya shule zake zilitaifishwa.
“Lakini kanisa tumetulia na tumejenga shule zetu nyingine ambazo zinatoa huduma kwa Watanzania bila ubaguzi wowote..., tujipange tuanzishe shule na tuziendeshe,” alisema Askofu Ruwai’chi.

Dawa za kulevya
Ruwai’chi alisema Serikali ichukue hatua za kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara hiyo bila kujali kama ni viongozi wa dini wala siasa.
Next Post Previous Post
Bukobawadau