Bukobawadau

Hatimaye Hamad Rashid, Shoka Hamis na wenzao wawili wafukuzwa CUF!

MAAMUZI YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA CUF TAIFA JUU YA HAMAD RASHID NA WENZAKE WATATU.
Baraza kuu la uongozi la taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF - CHAMA CHA WANANCHI) linaloendelea na kikao chake cha siku moja katika hoteli ya MAZSONS mjini Zanzibar limepokea tuhuma zinazowakabili viongozi na wanachama 14 wa chama kutoka kamati ya utendaji ya taifa.

Hadi saa 9 jioni leo lilisikiliza tuhuma za watano kati ya watuhumiwa ambao ni,
1.HAMAD RASHID MOHAMED(MBUNGE WA WAWI NA MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA)
2. DOYO HASSAN DOYO (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - TANGA),
3. SHOKA KHAMIS JUMA (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - PEMBA),
4. JUMA SAID SANANI (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - UNGUJA),
5. YASINI MROTWA (MJUMBE WA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA - MBEYA).
Baraza kuu liliwasomea tuhuma zao watano hawa na kuwapa nafasi ya kujitetea kwa sababu wao ni viongozi wa baraza kuu(viongozi wa kitaifa wa chama) kwa mujibu wa kifungu cha 10 (5) cha katiba ya chama.

Baada ya kutafakari kwa kina maelezo ya tuhuma zao na utetezi walioutoa, baraza kuu la uongozi la taifa limeridhika kwamba wanne kati yao wamefanya vitendo vinavyowapotezea sifa za kuendelea kuwa wanachama. Hivyo basi, baraza kuu la uongozi la taifa limeamua kuwafukuza uanachama wa CUF viongozi hao wanne ambao ni HAMAD RASHID MOHAMED, DOYO HASSAN DOYO, SHOKA HAMIS JUMA na JUMA SAIDI SANANI. Uamuzi wa baraza kuu la uongozi la taifa kuwafukuza umefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 63 (1) (j), kifungu cha 64 (4), 64 (5), 64 (6) vya katiba ya chama.

Katika kufikia maamuzi hayo, baraza kuu la uongozi la taifa pia lilizingatia matakwa ya kifungu cha 62 (4), 62 (5), na 59 (8) (d) vya katiba ya chama ambavyo vinataka uamuzi wa kuwafukuza uanachama viongozi wa kitaifa wa Chama uwe ume umeungwa mkono na zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa baraza kuu kutoka tanzania bara na zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa baraza kuu wanaotoka zanzibar.

Uamuzi wa kuwafukuza uanachama viongozi hao wanne umeungwa mkono na wajumbe 23 kati ya 25 wa tanzania bara na wajumbe wote 22 wa zanzibar. Wajumbe 2 wa tanzania bara hawakukubaliana na uamuzi huo.

Kwa upande wa Yasin Mrotwa, Baraza kuu la uongozi la taifa liliamua kumpa karipio kali kwa mujibu wa kifungu cha 64 (5), (b) huku mwenendo wake ukiendelea kuchunguzwa kati ya kikao hiki na kikao kijacho cha baraza kuu la uongozi la taifa.

Hadi sasa, baraza kuu la uongozi la taifa linaendelea kusikiliza tuhuma zinazowakabili wanachama wengine 9 waliobaki (WASIO VIONGOZI WA KITAIFA). Taarifa ya maamuzi kuwahusu wao itatolewa baada ya kumalizika kikao leo.

''HAKI SAWA KWA WOTE''

Imetolewa na;
JULIUS MTATIRO
NAIBU KATIBU MKUU (TANZANIA BARA),
04 JANUARI 2012.

CHANZO JAMII FORUMS
Next Post Previous Post
Bukobawadau