Bukobawadau

WATU WAWILI WAMEKUFA NA WENGINE WATANO WAMEJERUHIWA VIBAYA BAADA YA KURUSHIWA BOMU

Na Antidius Kalunde
Bukoba

WATU wawili wamepoteza maisha yao papo hapo na wengine watano kujeruhiwa baada ya kuripukiwa na bomu lililodaiwa kurushwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha Kamwendo kata mbuba tarafa Rulenge wilayani Ngara mkoani Kagera.

Taarifa zilizotolewa na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Hennry Salewi,juu ya tukio hilo,ameeleza kuwa tukio hilo la kusikitisha lilitokea  juzi Mei 13 majira ya saa 3 usiku ambapo wahanga wa mlipuko wa bomu walikuwa wakitoka kuangalia taarifa katika TV iliyokuwepo kijijni kwao,ambapo wakati wakitoka nje walirushiwa bomu na watu wasiojulikana ambao walitokomea gizani kwani ulikuwa usiku wa giza.

Salewi amesema kuwa wawili waliopoteza maisha hapo hapo ni Felista William(57) na kijana Antiba Adrian(14)wote wakazi wa kijijini hapo,huku majeruhi wakiwa watano ambao amewataja kuwa ni Anatoria John(40)aliyeruhiwa shavu la kushoto,Angelina Benard(29)alijeruhiwa paja mguu wa kushoto na Anna William(28)ambaye alijeruhiwa tumboni.

Wengine ni Dikson Maton(28)alijeruhiwa paja mguu wa kulia pamoja na Ndaishimiye Daniel(17)ambaye pia alijeruhiwa tumboni,wote wahanga hao walikuwa wakitoka kuangalia taarifa ya habari kabla ya kurushiwa bomu hilo.

Kamanda Salewi amekana kuwa bomu hilo halikurushwa ndani ya jengo bali lilirushwa nje mlangono ambapo wahanga walikuwa ndo wanatoka kuangalia taarifa ya habari kama ilivyo kawaida ya watu kukusanyika katika sehemu kuangalia taarifa ya usiku,japo jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi juu ya kisa cha kurushwa bomu hilo.

Aidha,Salewi amesema kuwa matukio ya mabomu katika mkoa wa Kagera,si ajabu kwani ni mara nyingi kila opereisheni za polisi ni lazima wakikamatwa majambazi lazima wabainike na mabomu ya kutupewa kwa mkono.

Amesema kuwa ingawa tukio hilo linahusishwa na ugomvi wa mashamba kati ya marehemu na wahusika wengine,lakini bado uchunguzi un aendelea kwani miaka miwili iliyopita mtoto wa marehemu (Felista)naye alirushiwa bomu kama alivyorushiwa mama yake na alikufa papo hapo.

Amebainisha kuwa matukio ya mabomu katika kijiji hicho,yawezekana kusababishwa na mwiingiliano uliopo baina ya raia wa nchi jirani(Burundi)kwani kijiji kiko mpakani na hata shilingi inayotumika ni ya nchi jirani,hivyo kila wakati matukio yanakuwa ni ya kutumia silaha.Hivyo kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano iwapo kama kunataarifa zingingine juu ya tukio hilo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau