Bukobawadau

BALOZI KAGASHEKI AFUNGUKA KWAMBA SERIKALI HAITASITA KUZIFUNGIA KAMBI ZA UTALII ZINAZOKIUKA TARATIBU


SERIKALI imesema haitasita kuchukua hatua za kuzifunga kambi zote za kitalii ambazo zimo katika  maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyama pori WMA,ambazo zitaendelea kukiuka sheria na Kanuni kwa kulipa mapato yatokanayo na shughuli ya utalii kwa uongozi wa  vijiji badala ya malipo hayo kufanyika kupitia WMA.

Agizo hilo limetolewa na waziri wa Maliasili na Utalii Mh Balozi Khamis Kagasheki,wakati akizungumza na viongozi wa WMA ya Ikona wadau wa sekta ya utalii katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Amesema hivi sasa kumeibuka migogoro kwa baadhi ya WMA kwa kuhusisha viongozi na wananchi wa vijiji husika ambayo imekuwa ikihatarisha amani na mahusiano kati ya kijiji na kijiji kwa kugombea mapato baada ya baadhi ya kambi za utalii kukiuka kanuni na kwa kulipa tozo hizo moja kwa moja kwa baadhi ya serikali za vijiji kinyume cha sheria.

Waziri Kagasheki,alifikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mgogoro ambao umekuwa ukiendelea katika WMA ya Ikona wilayani Serengeti umechangiwa na baadhi ya kambi za kitalii kulipa mapato yake kwa baadhi ya vijiji wakati wakitambua wazi kuwa kambi hizo ziko ndani ya eneo la WMA.


Kwa upande wao baadhi ya wananchi na viongozi wa vijiji vitano vinavyounda WMA ya Ikona,walimesema mgogoro huo pia umechangiwa na uongozi wa WMA kushindwa kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi,madiwani kujineemesha huku wananchi wakishindwa kuvuna mazao  mashambani baada ya kushambuliwa na wanyamapori kutokana tu na kuthamini shughuli za uhifadhi.


WMA ya Ikona inaundwa na vijiji vya  Nyatambiso,Park Nyigoti,Nyichoka,Makunduzi na Rubanda ambapo tayari WMA 38 zimeanzishwa nchini 17 zikiwa zimetangazwa rasmi katika gazeti la serikali lengo likiwa kuhakikisha wananchi wanahifadhi na kunufaika na raslimali hiyo kwaajili ya kupunguza umasikini miongoni mwao.
 Waziri wa Mali asili mh Balozi Khamisi Kagasheki akitoa ufafanuzi kwa wananchi katika mkutano huo

 Maafisa wa Jeshi la Polisi Wilayani Serengeti wakiwa katika mkutano huo
Next Post Previous Post
Bukobawadau