Bukobawadau

HALMASHAURI YA MANISPAA YA BUKOBA YAWASILISHA TAARIFA YA HOJA ZA UKAGUZI KATIKA BARAZA LA MADIWANI.

 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe Akiongea na Waheshimiwa Madiwani na Wataalam wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Wakati wa Kikao cha Kujadili Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Katika Ukumbi wa Manispaa ya Bukoba.

Baraza la Madiwani Katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba lilipokea na kuijadili taarifa ya hoja za Ukaguzi za mwaka wa fedha 2010/2011 ya Mkaguzi na Mdhibiti  Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kikao kilichofanyika tarehe 5/07/2012 chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Massawe katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.

Katika kikao hicho cha baraza la Madiwani, Wataalam wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na Mkuu wa Mkoa hoja zote za Ukaguzi ziliweza kujadiliwa kwa kina na Waheshimiwa Madiwani pia na kukubaliana na majibu yaliyoandaliwa na kamati ya ukaguzi ya Halmashauri.
Pia Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba walisistiza juu ya wataalam kuzingatia kanuni, sheria na taratibu zilizopo katika kufanya kazi zao ili kupunguza au kumaliza hoja za ukaguzi pale unapofanyika ukaguzi. Pia kuhakikisha fedha hazibadilishiwi matumizi yake ili kutekeleza miradi kwa wakati.
“Kama wataalam wanayo majibu mazuri ya kujibu hoja tunaomba wafanye kazi zao vizuri badala ya kutafuta majibu mazuri ya kujibu hoja za ukaguzi mara baada ya ukaguzi kufanyika ili kuongeza uwajibikaji katika kazi.” Alisistiza Mhe. Karumna Diwani wa Kata ya Ijuganyondo.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Massawe katika kikao hicho alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na Halmashauri zote za mkoa wa Kagera kuhakikisha zinafanya vizuri zaidi katika baadhi ya miradi mfano TASAFU, barabara na sekta ya maji.
Kuhakikisha Halmashauri zote zinafuta hoja za ukaguzi za miaka ya nyuma ambazo zinaendelea kuonekana kwenye vitabu vya ukaguzi kama hoja mpya. “Katika mkoa wa Kagera Halmashauri zote ikiwemo Chato hoja za ukaguzi ni jumla ya shilingi bilioni tatu, hoja hizo zifungwe mara moja.” Aliagiza Mhe. Massawe.
Halmashauri zote za Mkoa wa Kagera zitoe mikataba ya miezi mitatu mitatu na kuvunja mikataba kwa mawakala ambao wanaonyesha ubabaishaji katika kukusanya kodi au mapato ya Halmashauri husika. Pia kuhakikisha thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa na halmashauri.
Mhe. Massawe aliwakemea wakaguzi wa ndani kuhusu kutotoa taarifa za ukaguzi ubadhilifu wa fedha na wakati wapo katika halmashauri na hoja kuibuliwa na wakaguzi toka nje. Vilevile aliagiza kila baada ya miezi mitatu wakaguzi wa ndani wa Halmashauri zote kuwasilisha taarifa zao katika ofisi yake.
Aidha Halmashauri zote zimeagizwa kutunza nyaraka mbalimbali kwa ajili ya ukaguzi, kuchukua hatua dhidi ya watendaji wazembe, kusimamia ulipwaji wa mishahara ya watumishi pia na kuimarisha kamati za ukaguzi zilizoundwa kisheria na kukusanya kodi kwa kiwango cha kuridhisha.

Mwisho Mkuu wa Mkoa alisistiza kuwa hatosita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtendaji au Halmashauri yoyote itakayofanya kazi zake kwa uzembe bila kuzingatia kanuni sheria na taratibu zilizopo. Pia alisema hataki kusikia tena katika mkoa wa kagera kuna Halmashauri yenye hoja za ukaguzi kuanzia mwaka huu wa fedha 2011/2012.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael,
Afisa Habari Mkoa,
Kagera.
Next Post Previous Post
Bukobawadau