TATIZO LA ELIMU TANZANIA NA MFANO WA KIONGOZI WA WASIOVAA VIATU
Ni wakati mwingine wa kulalama na
kupiga kelele za msimu. Kelele ambazo kwa historia ya Watanzania tumejifunza
kuwa sawa na upepo uvumao usio na madhara wala usiochukuliwa tahadhari kwa
madhari ya mbeleni. Naamu! NECTA
imetuletea kipande kingine cha filamu ya Elimu Tanzania. Ni kipande kitamu cha
filamu ya kuogofya na inayoacha madhara kwa vizazi na vizazi. Mfululizo wa
filamu ya hii umetengenezwa katika mtindo ambao kipande cha leo ni kikali zaidi
kuliko kile cha jana. Huwezi kupata uondo wa filamu hii kama hukuangalia au umesahau
vipande vilivyopita. Na kama umesahau wala usijisikie vibaya kwani hiyo ni moja
ya jadi zetu.
Basi ili twende sawa,
nitakukumbusha vipande vichache vya filamu hii vilivyochezwa na kutoka miaka ya
hivi karibuni. Ni vile tu ninavyokumbuka kwani nami ni Mtanzania origino!
Filamu yetu itaanzia kwa watoto 5,000 waliofaulu kujiunga kidato cha Kwanza
wakiwa hawajuhi kusoma wala kuandika. Hiki ni kipande (episode) cha awali na
cha kusisimua. Mmoja wa wachezaji wa hiki kipande alinifurahisha pale alipoamua
kuandika “mistari” kwenye mtihani. Kilipotoka, Watanzania wa kike kwa wa kiume,
wafanyakazi kwa wakulima na wanasiasa kwa wanaharakati walisisimuka kweli kweli.
Mwisho wa siku msisimko ukaisha na filamu ikapoteza mvuto bila kuacha hata
funzo na wala kuchukua hatua.
Kitambo kidogo kikaletwa kipande
kingine. Zamu hii Walimu wakiongozwa na Chama Chao (UWT) wakadai mazingira bora
ya kazi, vitendea kazi na stahili zao ikiwemo malimbikizo mbalimbali. Kwenye
hiki kipande nikiri kwamba nami sikumbuki chote. Ila siwezi kusahau pale dakika
ya 85/90 Walimu waliposema “Si hamkutusikiliza? Kitaeleweka tu!” Kwa upole wa
nyoka Walimu wakarudi kazini kwa amri ya mahakama na serikali pamoja na Wazazi
tukasahau kuwa amri ya mahakama haiendi kuwasimamia au kukagua kujua nini hawa
walimu wanafanya madalasani. Baada ya kutulia kwa takribani miezi nane,
watazamaji walikwisha sahau kabisa habari ya kipande (episode) cha mgomo wa
Walimu.
Katikati ya mapumziko ya filamu
pendwa, ikawekwa jingle ya kukosekana kwa mitaala ya Elimu Tanzania. Miemko na
tambo kubwa kubwa zikapigwa ili kuufanya ukweli uchanganyikiwe! Mwisho wa
jingle, ukweli ukawa mtanzikoni (in dilemma), wasikilizaji wakabaki wamechanganyikiwa
na kuduwaha kama ilivyo ada.
Wiki hii NECTA imeamua kutuletea
kitu kipyaaa kabisa toka kwenye makalatasi. Kama kawa mzigo umewashika
vilivilvyo Wa-Tz. Wakilala, wakiamuka wanalo—matokeo mabaya ya Kidato cha nne!
Wanafunzi wamefanya yao. Wenye fani wamechora ma-ZOMBIE, wenye vipaji wametunga
hadithi/filamu, Chokoraa wameandika matusi, Masharobaro/Wasafi wamekusanya pepa
Nyeupeeee, na wachache walioweza wamejaribu kujitetea! Kwenye kipande cha
kwanza tulipata wahitimu 5000 wasiojua kusoma na kuandika. Zamu hii tumezalisha
wahitimu 270,289 walioshindwa mtihani sawa na asilimia 60%! Na ni hisia zangu
kwamba yamkini hii nayo ni seti inayohusisha wasiojua kusoma na kuandika walau
Kiswahili kwa ufasaha.
Hiki kipande cha matokeo cha wiki
hii kimeanza kugawanyika katika vipande vingine vidogo vidogo vingi. Mimi
nakipenda na nimekikalili kile ambacho Mkurugenzi wa NECTA anaelezea waliofanya
Wanafunzi ndani ya chumba cha mtihani. Wacha nimnukuu “Mwaka
jana tulikutana na ‘single’ yaani waliandika mashairi kwa uchache, lakini mwaka
huu tumepata albamu nzima… ni vituko vitupu, wengine wanaandika mapenzi,
mwanafunzi anatumia ukurasa mzima kumlalamikia mpenzi wake. Miongoni mwa
yaliyoandikwa ni mpenzi, umeniacha, natamani kunywa sumu, usiku silali nakuwaza
wewe…” alisema Dk Ndalichako. Agha gha gha gha gha gha! Subiri tu-forward
kidogo. sikiliza na hapa “Unakuta
mwanafunzi anaeleza anavyolishangaa Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge,
wamekaa kama wapo kijiweni, wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za
wananchi waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda
Kombe la Kagame inapokelewa bungeni. Bunge limekuwa kama kijiwe, bungeni siyo
ukumbi wa starehe kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika ofisi zao au
viwanjani…” Mama Ndalichako mcheshi
sana.
Mpendwa msomaji masimulizi yote
hapo juu ni matokeo ya matatizo. Vyanzo vya matatizo haya ni vingi na kila
mmoja, awe mzazi, Mwalimu au mwanafunzi ameshiriki kufanikisha na kukuza
matatizo. Kwa kuwa hii ni makala ya porojo za kahawa ya jioni, basi nitaandika
bila rejea na kwa kutumia mtazamo binafsi.
Moja ya sababu kubwa ya matatizo
ya sekta ya Elimu ni kuwa na viongozi waliojikinga na kujitenga mbali na mahali
yanakoibuka matatizo yanayoathiri jamii wanayoiongoza. Tuna viongozi waliovaa
viatu, wanaotuongoza kutafuta suluhu ya tatizo la barabara kwa kutupitisha
kwenye njia iliyojaa miiba. Hawachomwi na miiba hivyo hawana hisia za uchungu
tuupatao, hawaoni simanzi kwenye nyuso zetu maana wametupa visogo vyao, na hata
wakisikia tunaguna wao wanadhani tunaifurahia safari. Ni sababu hii hii
unayosababisha viongozi wapalilie matatizo yaliyopo katika sekta ya afya.
Hatuwezi kuwa na viongozi ambao watoto wao wanasoma shule zenye walimu wazuri,
vifaa na mahabara zilizokamilika
tukategemea wajue matatizo ya
shule zetu za umma na wawe na uchungu wa kuziboresha. Sana sana tunawajengea
mazingira ya wao kujifunza usanii wa kuonyesha nyuso zenye huzuni lakini rohoni
na kichwani kumetulia, midomo yenye kupiga kelele na kulaani wakati kifuani kuko
tuli. Najua kuna matatizo mengine ya kimfumo, kitaalamu na kimuundo katika
sekta ya Elimu. Lakini haya yote ili yafanyiwe kazi kwa ufasaha tunahitaji
wanaofanya maamuzi juu ya Elimu yetu na Watendaji katika sekta husika wapate
msukumo wa ndani. Na huu msukumo hauji kama tunaendelea kuwaacha watuongoze
kupita njia yenye miiba wakiwa mbele na wamevaa viatu. Lazima tuwavue viatu na
wakae nyuma ya visogo vyetu kwanza ili nao wajue kwamba ukali wa tindikali
hauonjwi kwa hisia. Wakubali ama sote tuvae viatu au watembee peku nasi tuwafuate tukiwa
tumevaa viatu.
Kwa ufupi kutafuta suluhu ya
matatizo ya Elimu yetu tunahitaji kuwa na suluhisho la haraka, la muda wa kati
na muda mrefu. Lazima tufikie mahali frameworks za sekta muhimu kama Elimu ziwe
kama misahafu. Nisingependa kuendelea na porojo. Naomba kalamu yangu leo iishie
hapa.
Imeandikwa na:
Ericus Kimasha
+255-713-177372