Bukobawadau

UDINI: Uchafu Chini ya Kapeti tunajidanganya wasafi - Zitto Kabwe

‘Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara hii ambayo ni muhimu sana na ni moja ya Wizara ambazo ni andamizi katika uendeshaji wa Serikali yetu kwa sababu ndiyo Wizara ambayo inasimamia administration of justice. Kwa hiyo, nafurahi sana kuzungumza leo hii.

Mheshimiwa Spika, nina kitabu cha survey ambayo imefanywa na watu wa REPOA lakini ni kazi ya Serikali na kwa sababu ni kazi ya Serikali, kitabu hicho kinaitwaViews of the People 2007. Kitabu hiki ni sehemu ya shughuli za utekelezaji wa kila mwaka wa Mkakati Wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi yaani MKUKUTA. Katika kitabu hiki, inaonyesha kwamba level ya kutoaminiana mistrusts kati ya Watanzania imefikia 78%, kwa maana ya kwamba katika kila Watanzania 10 ni Watanzania 8 tu ndiyo wanaoaminiana na kuaminika. Kwa hiyo, katika kila Wabunge 10 ndani ya Bunge hili ni Wabunge 2 tu ambao akisimama akizungumza unaweza ukaamini maneno yake, hii ni hali mbaya sana katika taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nimeanza hili kwa sababu ya mjadala ninaouona wa suala la Mahakama ya Kadhi. Mjadala huu ukiangalia tu mtiririko wa watu wanavyochangia, umeligawa Bunge kwa misingi ya dini. Wabunge Waislam wanatoa sababu zao za kwa nini Mahakama ya Kadhi iwepo na Wabunge Wakristo wanatoa sababu zao kwa nini Mahakama ya Kadhi isiwepo na inafikia mpaka kutumia lugha ambazo watu wanaotusikiliza huko nje na wao wanagawanyika.

Mheshimiwa Spika, sasa sisi wengine tumekuta nchi hii ikiwa united, nchi ambayo watu wote tunaishi pamoja na kwa kuangalia level ya ujana, wengine tunaamini tutaishi muda mrefu zaidi ya wengine, kwa hiyo, tusingependa kuona taifa inaparaganyika na wengine tusingependa kuona kwa macho yetu wenyewe na kwa kweli wengine tupo tayari kusimama kuona kwamba taifa hili haligawanyiki. Mjadala huu unahitaji tolerance ya hali ya juu sana kwa sababu ni mjadala wa imani, mnapoanza kujibizana kwa imani ni kama wengine wanavyosema uvumilivu utaondoka, tunahitaji tolerance ya hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana haujaja Muswada, kuna maelezo, kwa wale ambao wanasema kwamba Mahakama ya Kadhi iwepo, ni haki yao kusema kwamba Mahakama ya Kadhi iwepo, tutakuja kukubali au kukataa tutakapoona kwamba Muswada huu unakidhi haja. Lakini majibizano ambayo yanaendelea sasa hivi siyohealth hata kidogo kwa sababu akisimama Mbunge Salum akamjibu Mbunge Paul, Paul na Salum ambao si Wabunge wataendelea kujibizana huko nje.

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani tuwe watulivu na tuwe tolerant, tusikilize hoja za kila upande kwa sababu hata baadhi ya lugha ambayo inatumika si nzuri, kwa sababu atasimama mtu atasema wenzetu wanasema hivi, Mheshimiwa Spika ukisema wenzetu kwa mfano Mheshimiwa Godfrey Zambi amesimama anasema wenzetu wanasema hivi maana yake ni kwamba tayari kuna makundi kwamba kuna hawa wenzetu na hawa si wenzetu.

Mheshimiwa Spika, mimi nisingependa tufikie katika hali ya namna hiyo ningependa mjadala huu uwe mpana zaidi, uwe mjadala wa hoja zaidi, tusikilizane, tuangalie imani za kila mtu na tuweze kuona na wala sio kwamba mimi niseme tu kwa sababu limekuwa likizungumzwa, hujibu hoja ya kwamba ni lazima Mahakama ya Kadhi iwepo kwa kusema ikiwepo na hao wengine wataanzisha Mahakama yao, inawezekana hao wengine hawana utaratibu wa aina hiyo. Ndiyo maana ni lazima na ni muhimu sana tuweze kuhakikisha kwamba mjadala wa namna hii hautugawi bali unakuwa ni mjadala ambao ni health vinginevyo hali ilivyo sasa tumehama Bunge la kuwa Bunge la Vyama Vingi tumekuwa Bunge la dini mbili. Maana tumezoea mijadala ni Kambi hii ya Upinzani inapingana na Kambi ya Chama Tawala lakini toka jana naona mjadala ni kambi ya wanaotaka Mahakama ya Kadhi na kambi ya wasiotaka Mahakama ya Kadhi. Mimi nadhani tusubiri hiyo report ambayo Waziri ameizungumzia na ijadiliwe kwa mapana na tusiingie katika lugha ambazo zinaweza zikatufanya kama taifa tuweze kugawanyika. (Makofi)’

Haya ni baadhi ya maneno niliyoyasema tarehe 14 Agosti 2008 wakati nachangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Bunge lilikuwa limewaka moto. Wabunge Waislam wakijenga hoja za kiislam kutaka mahakama ya kadhi na wabunge wakristo wakijenga hoja za kikristo kukataa mahakama ya Kadhi. Kulikuwa na Umoja wa Wabunge Waislam na Umoja wa Wabunge wakristo. Wakikaa kwenye vikao na kupanga namna ya kujenga na kupangua hoja. Hali ilikuwa mbaya sana. Nikawatazama Wabunge wazee rafiki zangu na kuwaandikia wasimame kuonya hali ile, hawakusimama. Nikaomba nafasi kusema. Hali ikatulia na nilipotoka Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akaniita kunishukuru sana. Mzee Malecela alikuwapo Bungeni lakini akanitumia ujumbe wa kunipongeza kwa maneno yangu yale. Lakini mpasuko wa nchi kwa misingi ya dini bado ni dhahiri kabisa.

Tumeshudia vitendo vya watu kuchukua sharia mkononi na kufanya mauaji dhidi ya watu wengine kwa misingi ya dini zao. Leo Mtanzania mwenzetu Padri Everist Mushi anapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele. Ameuwawa kwa kupigwa risasi. Kosa lake nini? Kundi la wahuni wachache limetoa roho ya Mtanzania kwa sababu tu Mtanzania huyu ni Mkristo. Tumeshuhudia mauaji pia kwa sababu ya ugomvi wa kuchinja.

Eti sisi Watanzania leo tunagombana kwa sababu ya kuchinja. Bora sisi wengine tunakula majani tu na hivyo magomvi haya ya kuchinja, ambayo kwa kweli kwa muda mrefu jamii ilijiwekea utaratibu wake bila kuingiliwa na serikali, hayatusumbui sana. Hata hivyo yanasumbua jamii zetu na ni suala la ibada kwa baadhi ya Watanzania. Kugombana kwa sababu ya kuchinja ni dalili tosha kuwa sasa uzi wa uvumilivu wa kidini uliokuwa umeshika Taifa hili umekatika. Ni kweli umekatika, wala tusishtuke.

Tatizo kubwa Tanzania ni utamaduni wa kuficha uchafu. Majumbani kwetu tunafagia na kuweka uchafu chini ya kapeti na kujidai tu wasafi. Namna hiyo hiyo ndio tunavyoangalia matatizo yetu ya kijamii na hasa kiimani. Nimesema hapo juu kwenye hotuba yangu hiyo ya mwaka 2008, Watanzania hatuaminiani kabisa kabisa. Tunadanganyana sana tunapokutana na tunapoona tatizo cha kwanza tunakimbilia kutafuta ‘jamii gani ya kulaumu’ na kulaumu kwa ujumla. Waislam kadhaa wanasema eti nchi inaendeshwa kwa mfumo kristo hivyo kupendelea wakristo. Wakristo kadhaa wanasema Waislam wanapendelewa na kulindwa na dola. Lakini hawa waislam na wakristo wanaolalamika hawakai kuoanisha hayo malalamiko yao ili kupata suluhisho. Hawataki kwa sababu pakiwa hakuna ‘tension’ watapata ajenda? Kuna watu wanaishi kwa migogoro tu.

Suala la udini lipo, linakomaa. Badala ya kulitatua kwa kuchukua hatua kali za kisheria kwa watu wote wanaosambaza jumbe za chuki tunabaki kulaumulaumu na kuguguna tu. Udini upo na ni kansa inatula kidogo kidogo. Nitawapa mfano wa udini dhahiri niliyokutana nao kwenye uchaguzi jimboni kwangu mwaka 2010.

Jimbo langu lina vijiji 33. Kuna vijiji viwili vilikuwa vina mvuto tofauti kwangu. Kijiji cha Kagunga kilinipokea vizuri sana mwaka 2005, wakanipa kura nyingi sana (nilishinda kwa tofauti ya kura 600 dhidi ya mpinzani wangu Helimenshi Mayonga). Kwa kweli niliwapenda watu wa Kagunga na kufanya kazi nyingi za maendeleo kule ikiwemo kushawishi miradi mikubwa ya maendeleo kama ujenzi wa bandari, ujenzi wa soko na hata kupeleka umeme na kujenga barabara kuunganisha kijiji hiki na mji wa Kigoma. Kijiji hiki kina wakazi wengi ambao ni waumini wa kikristo.

Kijiji cha Bubango kina waislamu wengi. Mwaka 2005 Kijiji hiki wakazi wake walinikataa kabisa na kuunga mkono mgombea kutoka chama cha CUF kwamba eti ni chama cha Waislamu. Ilifikia wakati nilikuwa wala siwezi kufanya mkutano wa kampeni katika kijiji hiki kwa sababu hawakutaka hata kuniona. Nilishindwa vibaya sana katika kijiji hiki. Kuna vituo vya kupigia kura nilipata kura 4 kati ya kura 280 zilizopigwa. Katika kipindi cha miaka 5 ya ubunge wangu, niliwakasirikia watu wa Bubango na sikwenda kabisa kuwatembelea licha ya kutuma ujumbe wazee kunitaka radhi. Sasa tazama nini kilitokea mwaka 2010?

Siku moja nikiwa katika kampeni kijijini Bubango, nikaitwa msikitini na waumini wakaelekezwa wanipe kura kwa sababu mimi ni mwislamu mwenzao. Sheikh aliyekuwa anatoa mawaidha akasema msijali Zitto hakufanya lolote lile hapa kijijini lakini mpeni kura tu kwa sababu ni Mwislamu mwenzetu. Nikaenda kwenye mkutano wa Hadhara nikawaambia wale watu kuwa sitaki kura zenu kama mnanipa kwa sababu ya uislamu wangu. Nikaondoka. Nilishinda katika kijiji hiki. Nilipewa kura kwa sababu ya uislam wangu.

Ngome yangu ya kampeni ilikuwa Kagunga. Ndipo nilipoweka nguvu zangu maana ninapendwa na nilifanya mambo makubwa. Siku chache kabla ya kampeni, ilikuwa siku ya jumanne nikaitwa kwenda Kagunga kwamba mambo yameharibika sana. Nikataharuki na kupanda boti la kukodi na kwenda Kagunga nikafika saa nne usiku. Wenyeji wangu wakaniambia kuwa wametangaziwa kanisani kwamba Zitto asipewe kura kwa sababu akienda Bungeni ataleta mahakama ya kadhi. Nikaomba kuongea na viongozi wa dini kesho yake asubuhi, wakaja wachungaji 11 (Kagunga kuna makanisa mengi sana). Nikawauliza ni kweli kwamba mimi nisipewe kura kwa sababu ya uislamu wangu? Wakasema hayo ndio maagizo na wameshawaambia waumini.

Nikawauliza mnaamini katika hayo? Wachungaji wanne wakasema, mheshimiwa mbunge sisi tupo na wewe. Nikapiga ngoma kuitisha mkutano wa hadhara saa nne asubuhi pale ziwani Kagunga. Nikawaambia watu wa Kagunga, anayetaka kuninyima kura kwa sababu ya uislamu wangu aendelee na uamuzi wake. Nikaorodhesha nini tumefanya Kagunga. Nikasema kama hayo hayatoshi kuwafanya kuchagua mbunge, basi amueni kwa kutumia imani za dini yenu. Nikashuka, nikapanda boti na kuondoka. Matokeo yalipotoka, Kagunga nilishinda kwa tofauti ya kura tisini tu (kutoka kura 600 mwaka 2005).

Toka matukio haya mawili nikasema moyoni mwangu hatuna nchi tena. Viongozi wamekuwa wakitoa kauli za kugawa wananchi. Kiongozi wa CCM kwa mfano anaposema CUF ni chama cha Waislam, anawaambiwa waislam nendeni huko ndio chama chenu. Kiongozi wa CCM anaposema CHADEMA ni chama cha kikristo, anawaambia wakristo nendeni huko ndio chama chenu. Mwanachama wa CHADEMA anapotoa taarifa kuonyesha kuwa CCM inapendelea waislamu, anadhihirisha kuwa kweli chama chake hakipendi waislamu. Viongozi wa kisiasa wanatoa kauli majukwaani bila kuzipima na kugawa wananchi. Baadhi ya taasisi za kidini zimekuwa zikutumiwa na vyama vya siasa kusambaza chuki hizi kwenye jamii.

Mimi ni Mtanzania. Taifa ambalo limejengwa kwenye misingi ya usawa na haki. Misingi ya Umoja na mshikamano. Tunu zetu ni hizo na sio dini zetu. Viongozi wanapoendelea kulea upuuzi huu wa udini Taifa litapasuka vipande vipande. Kwenye masuala ya udini watu hawaweki akili, wanaongozwa na imani. Mijadala inayoendelea sasa inatugawa sana. Lazima tukatae. Tuseme udini sio tunu ya Taifa letu, inaweza kuwa tunu ya mtu binafsi lakini Utanzania wangu ni utu, umoja, uzalendo, uwajibikaji na uadilifu.

Mtu yeyote yule anayepanda mbegu za udini asionewe aibu. Ashughulikiwe haraka sana. Wapuuzi Fulani wanasema kwa kuwa Mkuu wa Polisi ni wa dini Fulani basi ndio maana hachukui hatua. Huyu sio Mkuu wa polisi wa kwanza nchini wa dini hiyo, kuna aliyekuwepo na akaingiza msikitini askari polisi na viatu. Tusiruhusu kabisa upuuzi huu kwamba watu wenye dini Fulani hawachukui hatua dhidi ya watu wa dini zao. Vyombo vya usalama vijue, mtu anayeua ni muuaji tu na lazima achukuliwe hatua kwa uuaji wake. Tena uuaji mbaya unaojenga chuki kwa nchi yetu. Mtu anayetamka maneno ya chuki dhidi ya dini nyingine achukuliwe hatua bila kujali hadhi yake.

Mwisho hatuna namna, ni lazima Taifa liongee. Lazima tuwe na mjadala wa wazi na wa kuheshimiana kuhusu masuala ya udini na kuvumiliana kidini. Hatuwezi kuweka rehani amani ya nchi yetu kwa suala la kuswali au kusali. Badala ya kurushiana lawama, tuzungumze kwa uwazi. Makundi ya wananchi wenye kuona uonevu wa kidini waje waseme kwa uwazi na masuala hayo kujadiliwa kwa uwazi. Muhimu tupate mwafaka na kujenga Taifa imara na lenye mshikamano.

Kwa nchi yenye utajiri wa rasilimali kama yetu udini ni kichocheo tosha cha vita ya wenyewe kwa wenyewe na migogoro isiyokwisha. Ni lazima tuchukue hatua sasa. Tuache unafiki wa kunyoosheana kidole. Kila mtu atazame nafsi yake na aseme ukweli wake kwa uwazi kabisa. Tusifukie uchafu chini ya kapeti.


Source: Raia Mwema
Next Post Previous Post
Bukobawadau