Bukobawadau

GAZETI LA MWANANCHI LIMEANDIKA;Alex Massawe mtegoni nchini Afrika Kusini


Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu Alex Massawe ameingia kwenye mtego wa Polisi wa Afrika Kusini ambao wamekuwa wakimsaka baada ya kuombwa na Serikali ya Tanzania.
Habari kutoka katika Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa baada ya Polisi wa Tanzania kuthibitishwa na maofisa wa Afrika Kusini kuwa wamefahamu aliko wameandaa maombi kwenda Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ili akamatwe na kurejeshwa nchini.
Licha ya kutokufahamika kwa sababu za kusakwa kwake, hakuna kiongozi yeyote wa polisi aliyekuwa tayari kuzungumzia tukio hilo lakini chanzo cha kuaminika kutoka katika jeshi hilo kilieleza kuwa wenzao wa Afrika Kusini wamewaeleza kuwa wamefahamu aliko.
Kusakwa kwa Massawe kumezua maswali kadhaa kutokana na kutokuwekwa wazi. Lakini Aprili 4, mwaka huu alitajwa mahakamani katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni,  Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara maarufu, Abubakar Marijani ‘Papaa Msofe’, mshitakiwa mwingine, Makongoro Joseph Nyerere alitoa malalamiko, mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome mara baada ya Wakili wa Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kuitaja.
Mshtakiwa huyo, aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia kazi na kutuhumu kuwa ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya kesi yao hadi Massawe akamatwe.
“Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza ili Massawe akamatwe. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol juu ya kumsaka mtu huyo ili aletwe. Ndiyo maana Polisi wa Tanzania hawawezi kuzungumza chochote hadi watakapomweka mikononi mtuhumiwa huyo,” kilieleza chanzo cha gazeti hili.
Awali, kulikuwa na habari kwamba Massawe, ambaye hufanya biashara za hoteli na mambo ya utalii katika Jiji la Dar es Salaam, Arusha na Moshi, amekamatwa katika mji mmojawapo ulioko katika Pwani ya Afrika Kusini.
Habari hizo za kukamatwa kwa Massawe, ambaye pia hufadhili masuala ya kisiasa na michezo, zilianza kusambaa jana mapema asubuhi kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya Facebook, Twitter na Jamii Forum huku ikidaiwa amekamatwa.
Kulikuwa kuna mkanganyiko wa taarifa huku wengine wakidai alinaswa akiwa ndani ya boti huko Afrika Kusini, wengine wakidai alikamatwa wakati akijaribu kuingia Msumbiji akitokea Malawi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau