Bukobawadau

MBUNGE WA NKENGE, ASUMPTER MSHAMA ATAKA JUMAPILI ISITUMIWE KWA KUPIGA KURA

Mbunge wa Nkenge, Asumpter Mshama (CCM) ameitaka Serikali kutoa tamko la lini itaacha utaratibu wa kutumia siku ya Jumapili kwa ajili ya kupiga kura.

Mbunge huyo alihoji iwapo Serikali haioni tatizo kuwadhulumu baadhi ya waumini muda wao na kwamba jambo hilo limekuwa likisababisha baadhi ya watu kukimbilia kufanya ibada na huku wakishindwa kupiga kura.

“Kitendo cha kufanya uchaguzi wa kitaifa siku za Jumapili kinasababisha baadhi ya watu kushindwa kupiga kura jambo linalowanyima haki yao ya kikatiba,” alisisitiza Mshama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge William Lukuvi, alikiri kuwa sheria za uchaguzi pamoja na kanuni zake, haziainishi siku maalumu ya iliyoteuliwa kwa ajili ya kupiga kura.

Lukuvi alisema kuwa uamuzi wa Serikali kuteua siku ya Jumapili kwa ajili ya kupiga kura ulitokana na sababu kuwa ni siku ambayo Watanzania wengi hawaendi kufanya kazi hivyo kuwa na fursa katika zoezi la kupiga kura.

Hata hivyo alikiri kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watu wengi kuhusu siku ya Jumapili wakitaka ibadilishwe ili isitumike kwa ajili ya kupiga kura lakini pia Serikali inatambua kwa dhati kuwa ni siku maalumu kwa ajili ya waumini wa dini ya Kikristo.

Alisema suala hilo litafanyiwa kazi katika marekebisho ya Katiba Mpya ambayo Tanzania inatarajia kuipataKatiba Mpya kuanzia Aprili mwakani wakati uchaguzi mkuu utafanyika
Next Post Previous Post
Bukobawadau