Bukobawadau

Wizara Maliasili kuajiri askari wanyamapori 400

Dodoma. Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kuajiri askari 400 wa Wanyamapori nchini katika kipindi cha Julai mwaka huu.
Ahadi hiyo ilitolewa bungeni na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamisi Kagasheki ambaye aliahidi pia kupeleka bungeni Sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori katika Bunge la Novemba mwaka huu.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema) ambaye alihoji mpango wa Serikali kuchelewesha kutungwa kwa mamlaka hiyo kuwa ni ukiukwaji na dharau kwa Bunge ambalo lilipendekeza hivyo.
“Ndiyo maana tunalalamikia sheria hiyo kwani kila wakati tembo wanauawa na hasa wale ambao wako nje ya hifadhi, kuna kigugumizi gani cha kutoleta sheria hiyo mapema bungeni,” alihoji Zitto.
John Lwanji (Manyoni Magharibi-CCM) alihoji mpango wa kuanzisha Mamlaka itakayosimamia hifadhi za mapori ya akiba ya wanyamapori badala ya idara ya wanyamapori.
Naibu Waziri wa Malisili na Utalii Lazaro Nyalandu alisema kuwa ahadi ya Serikali ya kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori iko palepale ambapo hadi sasa rasimu za kwanza za sheria hiyo zimekwishakamilika.
Nyalandu alisema kuwa katika mkutano wa nane wa Bunge, Serikali iliahidi kuwa ifikapo Desemba 2012, mchakato wa uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori utakuwa umekamilika.
“Hata hivyo, baada ya kamati ya uanzishwaji wa Mamlaka kupata maoni ya wadau, iligundua uwepo wa mambo muhimu yaliyohitaji kujadiliwa kwa kina,” alisema Nyalandu.
Alizitaja sababu zilizochelewesha utaratibu huo ni kupanuka kwa wigo wa wadau kwani walikusanya maoni kutoka kwa watu wengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kikamilifu
Next Post Previous Post
Bukobawadau