Mgogoro wa Loliondo: Kagasheki aponda kauli ya Nchemba
Dar es Salaam na Arusha. Mgogoro wa ardhi katika eneo la
Loliondo umechafua hali ya hewa ndani Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada
ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kumpinga
waziwazi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mwigulu Nchemba na
kusisitiza kuwa uamuzi wa Serikali kuhusu eneo hilo utabaki palepale.
Waziri huyo amesema kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wakiwamo wabunge wa CCM, haziwezi kubadilisha msimamo wa Serikali.
Kauli hiyo inatofautiana na ile ya Naibu Katibu
Mkuu wa chama hicho, Mwigulu Nchemba aliyekwenda Loliondo mwishoni mwa
wiki iliyopita na kuamua kuupeleka mgogoro huo kwa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akisema hatua hiyo inakiuka sheria na ina athari kwa wananchi wa
huko.
Akizungumza kwa simu jana, Kagasheki ambaye pia ni
Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), alisema Serikali imeamua kuchukua
kilomita za mraba 1,500 kati ya kilomita za mraba 4,000 za eneo la
Loliondo.
Alisema ilifikia uamuzi huo ili kulifanya eneo
hilo kuwa pori tengefu kwa ajili ya kusaidia wanyama kuzaliana na kupata
malisho, hatua ambayo inapingwa na wakazi wa eneo hilo.
Waziri huyo alisema kuwa Nchemba, ambaye pia ni
Mbunge wa Iramba Magharibi, anapaswa kuelewa kuwa Serikali haikukurupuka
kuchukua uamuzi.
Alisema matamshi ya kiongozi huyo wa CCM hayawezi
kuwa msimamo wa chama kwani viongozi hao walitumwa kwenda Loliondo
kukusanya maoni na kisha kuyawasilisha kwenye vikao vyake halali na siyo
kutumia mikutano ya hadhara kutoa uamuzi.
“Hayo maneno kama kweli yamesemwa na Nchemba, basi
hayo ni mawazo yake na wala siyo msimamo wa chama. Mimi najua chama
chetu kina taratibu za kujadili mambo na siyo kuanza kuzungumza nje ya
vikao,” alisema na kuongeza: