ZIJUE AINA ZA VIGANJA;Unakijua kiganja cha mwizi wewe?
Ndugu msomaji,
Wiki ya jana tuliuangalia mstari wa busara au Head line na nilielezea namna ilivyo rahisi kwa watu maarufu kusomwa viganja vyao ikilinganishwa na mtu wa kawaida. Leo nitazungumzia aina za viganja. Unajua, unaweza ukamjua mtu mwenye tabia ya udokozi kwa kumwangalia tu viganja vyake? Leo naomba tuwe pamoja ili tusipoteane halafu ukajikuta unatapeliwa kijinga jinga. Ni mchezo rahisi sana.
Ndugu msomaji, hakuna ubishi kuwa viganja ndio mtumishi wa viungo vyote vya mwili mzima! Viganja vitaosha uso, kupiga mswaki, kula, kuandika, kuoga n.k. bila idadi ya huduma kwa siku huku kiganja cha kushoto mara nyingi kikikitegea cha kulia kusulubike daima…
Viganja ndio majani ya kiumbe aitwaye binadamu na ndio maana huhusika na kila kitu katika maisha ya binadamu ikiwemo kumtafutia binadamu riziki zake na ndipo ubongo unapata nafasi ya kuviingiza viganja katika wizi, la kusikitisha ni kuwa viganja ndivyo vinabaki na kumbukumbu za wizi wote aliofanya binadamu huyo toka azaliwe!
Tusije tukapoteana jamani. Mtu anapoanza kushiriki udokozi au wizi basi vidole vyake huanza kujikunja kama vinafumba. Kadiri binadamu anavyozoea kushiriki wizi ndivyo vidole vyake vinavyozidi kujikunja na hakika kama utampa pesa mtu aliye na vidole vilivyojikunja ukamwacha mwenye vilivyonyooka halafu ukajikuta umetapeliwa basi mimi simo!
Kiganja ni muunganiko wa vipande vidogo vidogo sana vya mifupa vyapata kumi na vinne ndio vinatengeneza taswira na umbo la kiganja, lakini kulingana na elimu ya usomaji viganja kuna ukweli kuwa kiganja kinatofautiana na kingine na kila kiganja kinatoa tafsiri sahihi kabisa ya taswira ya mtu husika kwa kumwangalia tu. Unajua Kaisari Julius aliwahukumu watu kwa kuangalia tu viganja vyao kivipi? Sikia hii:
Kiganja kidogo sana! Mtu mwenye kiganja cha aina hii ana akili nyembamba sana usimpe majukumu makubwa! Anapenda kugombania vitu vidogo vidogo, Huwa anashangaa na kushtuka sana, anaweka maslahi yake mbele daima na wala si mtu wa maana popote pale.
Kiganja kidogo: Mtu wa aina hii hutasema nimekosea nikimwita ni mvivu popote unapokutana naye ndugu msomaji. Hukueleza mipango mikubwa sana ambayo huwa haizai matunda siku zote kwa uzembe wake tu.
Watu hawa si wakweli ndugu msomaji, huongopaongopa maisha yao yote na hupenda mazingira ya ubishi ubishi daima na wanapenda kujitengenezea mazingira ya kuvuta watu na wana akili sana ya kuwadanganya watu ila wanashindwa kutunza kumbukumbu za wongo na kugundulika mara kwa mara kuwa si waaminifu. Ni wenye bidii sana na washindani wazuri lakini huwa hawana mafanikio katika maisha.
Kiganja cha kawaida- Watu wenye viganja hivi ni wenye busara za wazi. Wanajua namna ya kuishi na watu na wanajihusiha na jamii kivitendo na kweli hupata heshima za stahili zao. Hutaabishwa sana na maisha lakini la kutia moyo ni kuwa watu hawa hufanikiwa sana katika maisha. Afya zao ni bora daima na sio waumini wa mahospitali. Ni wepesi sana kujua jamii na mazingira yanasemaje na kuyatumia kitija zaidi…
Kiganja kirefu:- Hawa ndio watu wanaitwa “waheshimiwa” mbele ya jamii popote. Si wenye furaha japo si wenye wasiwasi kihiiivyo. Wapo kivitendo zaidi katika mambo yao, wanatumia akili zaidi na wanaahidi ukweli daima. Ni wepesi wa kubaini tatizo na utatuzi huku wakiwa kimbilio la wasiojiweza popote.
Kiganja kirefu sana!- Watu hawa hawana shughuli yoyote katika jamii. Si watu wa kuwategemea kwa lolote! Ni wenye majivuno, wanatembea kwa mikogo huku akili zao zikiongozwa na ndoto za utajiri. Japo ni watu wenye vitisho, wakikumbwa na matatizo kidogo tu huathirika sana kwa kuwa si watu wanao yamudu maisha hivyo wanandugu bebeni msalaba.
Kiganja halisi:- Kiganja hiki siku zote kimekakamaa, kizito, na kimenona. Kiganja hiki utakiona kimebeba vidole vinavyofanana kwa urefu. Watu hawa ni waungwana sana. Huwa hawapendi maneno maneno ya kijinga. Nyumba zao hazipungui chakula malazi na mavazi. Familia yake ni watu wa kula na kunywa tu. Hawa kwa bahati mbaya hawataabishwi na kitu gharama wala bei juu. Wao hununua tu. Hawajui thamani ya maisha hawa kazi zao si za maana sana hivyo usiwaudhi kwa kuwa wanaongoza kwa kesi za jinai kila wanapo pandwa na hasira kwa kuwa hawazuiliki.
Kiganja Mraba:-Watu wenye viganja mraba ni watu muhimu katika jamii. Viganja vyao vina umbo sawa kwa urefu na upana huku vikijidhihirisha wazi kuwa vina mifupa imara. Viganja hivi havijakakamaa kama viganja halisi. Wenye viganja hivi ni watu “genious” na “intellectuals” ambao husaidia sana jamii nap engine huwa viongozi wa jamii zao. Hawa ni watu maalum na utawaona kuhubiri, kufundisha, kutabiri, kugundua, kuokoa, kuvunja rekodi n.k. Watu hawa kifupi hawajali kitu malipo na huidharau pesa hata ingekuwa nyingi kiasi gani.
Kiganja Kazi:- hawa ni wale ndugu zangu ambao wakikulamba kibao lazima uzimie! Lakini cha ajabu ndugu msomaji utakubaliana nami kuwa watu hawa si wakorofi na Mungu aliwaumba ili wawe msaada maana hujisikia raha kusifiwa kuwa walizuia tukio kubwa lililohusisha mabavu. Ukiwaomba nguvu hutoa hata bure na hawapendi kuona wanyonge wanaonewa. Mungu asifiwe, maana hufanikiwa sana katika maisha yao.
Kiganja Busara:- Hawa ni watu ambao viganja vyao vinaonyesha kuwa ni watu wanaojua sana kucheza na maneno na vitendo pia. Hutoa majibu ya maisha bora kwao na kwa jamii nzima kirahisi mno. Watu hawa ni tegemeo la jamii na ndiye msuluhishi wa jamii popote. Mungu atuepushe maana watu hawa japo tunaweka maisha yetu juu yao kumbe wao wenyewe ni waumini wazuri wa mahospitali kwa kuwa afya zao si shwari siku zote na hufa akiacha pengo kwa jamii yote...
Kiganja Msanii:- Hiki kiganja kwanza kabisa utakijua kwa ulaini wake, kina afya na kinavutia. Angalia pingili za vidole zote zinakaribiana urefu na alama za siri na kiasili za vivutio zikionekana wazi. Vidole ni vyembamba, virefu na vimekaa kisanii zaidi hata ikibidi kukoleza kwa urembo sawa tu kwa watu hawa na ni aghalabu kumkuta bila urembo kama pete, bangili n.k.. Hawa watu wanajua kupenda ni nini lakini bado wana donda ndugu la kutopendwa kiukweli na kihalisia kama wanavyopendwa wengine. Wakijiangalia kwa haraka hujihisi hawana mafanikio hasa kifedha, japo wanayo na kutokuwa na pesa ni hofu yenye ugonjwa wa kulazwa wodi ya wagonjwa mahututi katika maisha yao.
Kiganja Jeuri:- Hiki ndio kiganja kinachovutia zaidi. Kimeumbika vema, kilaini na kina afya njema sana. Kiganja hiki wala si kirefu wala kipana na hakina mapungufu. Watu wenye kiganja hiki ni watabiri wazuri sana na ukiwasikia tuondoke basi ondoka maana kuna janga litaanguka hapo mida hiyo hiyo baada ya wao kuondoka. Lakini upande wa pili unasoma kuwa hawa ndio watu wanaokumbwa na matatizo zaidi yaw engine. Kila siku wao huwa hawana pesa na hawana mwisho mzuri katika lolote duniani.
Kiganja mchanganyiko:- Kiganja mchanganyiko ni kile kilicho na sura ya busara na kazi. Wenye kiganja hiki ni wale waanzao jambo kwa makeke namikiki mingi lakini mara hukata tamaa na kusahau kila kitu. Akili zao zimelala katika simulizi, kufikirika na sio kusadikika hata siku moja. Hii huwafanya wasifaulu chochote maishani na kujipotezea heshima katika jamii. La kutia moyo ni kuwa uzeeni hufanikiwa kidogo japo kwa misaada na ni baada ya kujituma zaidi bila kukata tamaa.
Kwa makala hii tunafikia tamati ya mtiririko huu wa kusisimua wa jinsi ya kusoma viganja. Yapo mambo mengi sana katika sayansi hii, lakini bado tunayo mambo mengi zaidi ya kuambiana kupitia ukurasa huu. Wiki ijayo tutakuwa na “Jijue, wewe ni nani?” Makala hii itatoboa majibu ya maswali mengi sana yaliyojificha ndani ya tabia za watu na mahusiano yao mbele ya jamii inayowazunguka. Utajua kwa undani kabisa nani ni nani na kwa nini hivyo?
Asanteni kwa kunisoma na karibuni sana Temeke Mwembeyanga.
John Haule
Rumours Africa
0768 215 956
rumoursafrica@gmail.com