Bukobawadau

KCU (1990) Ltd. yageuka kichaka cha ufisadi

Na Prudence Karugendo

VIONGOZI wa chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. wameanza kuwatuhumu wanahabari kuwa wananunuliwa kukichafua chama hicho kutokana na wanahabari kuufichua na kuuanika uozo uliomo kwenye chama hicho cha ushirika. Hatahivyo viongozi hao wanashindwa kukikanusha kwa vielelezo chochote kilichoandikwa juu ya KCU (1990) Ltd. na kuonekana si cha kweli, wanabaki kushikana uchawi wao wenyewe kwamba fulani ndiye katoa siri.

Ukianzisha dhambi inakutafuna, madai ya kwamba wanahabari wananunuliwa bilashaka yanatokana na mazoea ya viongozi wa chama hicho kuwanunua watu mbalimbali kwa ajili ya kuficha madhambi yaliyomo kwenye chama hicho, au kutimiza malengo fulani.

Haieleweki ni siri gani inayopaswa kuhifadhiwa katika chama cha ushirika, tena siri inayotakiwa kuwa ya viongozi peke yao bila kuwashirikisha wanaushirika!

Mazingira ya aina hiyo ndiyo yanayozaa kitu kinachoitwa ufisadi kinachopigiwa kelele na kulaaniwa nchi nzima. Ufisadi unalaaniwa kwa vile ndani yake kuna dhuluma ambapo wachache wanadhulumu haki ya walio wengi. Wachache wananeemeka walio wengi wanaendelea kutaabika huku wakiwa wamewabeba migongoni mwao wale wanaoneemeka kwa jasho lao.

Makala hii imetokana na mambo mawili; la kwanza ni hali tata iliyokikumba chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha Kagera, na la pili ni kauli ya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adamu Malima, aliyoitoa Bungeni tarehe 16/ 5/2013, kwamba atakayewadhulumu wakulima ataumia.

Wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. ni wakulima, wakulima wa kahawa. Wanayofanyiwa na chama chao kikuu cha ushirika, ya chama hicho kujifanya ndicho kinachowamiliki wakulima wa kahawa badala ya wakulima kukimiliki chama, tayari hiyo ni dhuluma kwa wakulima, kwa kuanzia kabla ya kuyageukia mengine ambayo ni pamoja na uendeshaji mbovu wa shughuli za chama hicho.

Chama hicho kilikuwa na mkutano mkuu tarehe 8/5/2013, na baadaye tarehe 13 na 14/ 5/ 2013, kwa ajili ya mizania na makadirio. Wajumbe wa mkutano mkuu kawaida ni wawakilishi kutoka kwenye vyama vya msingi ambavyo ndivyo vinavyoiunda KCU (1990) Ltd.

Mkutano wa makadirio wa tarehe 14/5/2013 ulianza kwa kusomewa taarifa ya mwenyekiti ambayo baadaye wajumbe hupewa nafasi ya kuijadili. Lakini cha ajabu badala ya taarifa hiyo kuongelea maendeleo ya chama na namna ya kuyatatua matatizo yanayokikabili, ikawa inamuongelea mtu, mjumbe, mwakilishi kutoka chama cha msingi cha Kamachumu, Archard Felician Muhandiki.

Taarifa ya mwenyekiti ilikuwa inamtuhumu Muhandiki kwamba ndiye anayetoa siri za uozo wa chama kwenye vyombo vya habari. Papo hapo, wajumbe ambao tayari walionekana wameishapangwa na mwenyekiti wakaichangia taarifa hiyo wakitoa hoja kuwa mjumbe huyo afukuzwe kwenye mkutano. Hiyo ikawa dhuluma nyingine kwa wanaushirika wa chama cha msingi cha Kamachumu kinachowakilishwa na mjumbe huyo aliyefukuzwa mkutanoni na watu ambao hawakumchagua. Wakulima wa kahawa wa Kamachumu wakadhulumiwa uwakilishi wao na watu wa sehemu nyingine.

Nimemtafuta Mzee Muhandiki ili aweze kuelezea kilichompata na mtazamo wake kuhusu ushirika hususan hatma ya KCU (1990) Ltd. Yafuatayo ndiyo maongezi yetu yaliyo katika mfumo wa swali kwa jibu.

Swali: Wewe ni mfanyabiashara wa miaka mingi hapa Dar es salaam, kitu gani kilikushawishi uende kugombea uongozi katika KCU (1990) Ltd. Kagera?

Muhandiki: Kwanza mimi napenda sana nyumbani. Baada ya kuona mwenendo wa KCU (1990) Ltd. unatoka nje ya maadili ya ushirika nikaona bora nijiingize humo ndani kusudi nipate nafasi ya kuwaonyesha vitu ambavyo walikuwa wakiviruka ama kwa makusudi au kwa kutokuviona. Kama ujuavyo, huwezi kumwelekeza mtu akakuelewa vizuri ukiwa nje ya shughuli anayoifanya, mpaka uwe naye karibu kwenye shughuli husika.

Swali: Unao uzoefu wowote wa mambo ya ushirika hususan biashara ya kahawa?

Muhandiki: Ninao uzoefu wa masuala ya ushirika. Nimefanya kazi na vyama vya ushirika vya Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya na Uganda, kwa karibu miaka 40 nikivipa miongozo ya namna ya kujiendesha nikiwa katika kampuni ya Kalamazoo. Kuhusu biashara ya kahawa ni kwamba nimefanya kazi ya kuitangaza na kuitafutia soko kahawa iliyosagwa ya TANICA kwa kipindi cha miaka 5 kupitia kampuni ya Food Specialities Ltd.

Swali: Ili uwe mwanaushirika wa KCU (1990) Ltd. ni lazima uwe mkulima wa kahawa, je, wewe unalo shamba la kahawa?

Muhandiki: Ninayo, siyo ninalo. Ninayo mashamba ya kahawa makubwa na mazuri sana.

Swali: Nini kilichotokea ulipogombea uenyekiti wa KCU (1990) Ltd.?

Muahandiki: Sikugombea moja kwa moja uenyekiti. Kuna mchakato mrefu. Mimi niligombea uwakilishi wa chama changu cha msingi cha Kamachumu.

Swali: Baada ya kuukosa uenyekiti ukabaki mjumbe wa kawaida, mwakilishi wa Kamachumu. Je, KCU (1990) inakuwezesha kuhudhuria vikao Bukoba ukitokea Dar es salaam kama inavyofanya kwa wajumbe wengine walio Kagera?

Muhandiki: Hapana. Najigharamia mimi mwenyewe. Isipokuwa pesa ninayopewa ni ya malazi na chakula.

Swali: Kuna tetesi kuwa wewe si mkulima wa kahawa, kama tetesi hizo ni za kweli ilikuwaje wanaushirika katika chama chako cha msingi, ambao ni majirani zako wanaokufahamu vizuri, wakakuamini na kukuchagua uwe mwakilishi wao?

Muhandiki: Kwa akili za kawaida ni kwamba wasingenichagua kama madai hayo yangekuwa ya kweli.

Swali: Unadhani ni kitu gani kinaufanya uongozi wa KCU (1990) Ltd. ukuone wewe kama tishio?

Muhandiki: Huo ni uzoefu wa ufisadi. Wamezoea kula hovyo bila kuulizwa. Angalia, uongozi wa KCU (1990) Ltd. unazungukia kila chama cha msingi wakati wa uchaguzi, kumbuka kwa kutumia pesa ya wakulima, kuhakikisha wajumbe wanaochaguliwa katika vyama vya msingi ni wale wanaotakiwa na uongozi wa chama kikuu ambao hawawezi kuubana uongozi huo kwa namna yoyote ile katika uendeshaji wake mbovu wa chama kikuu.

Swal:Uongozi wa KCU (1990) Ltd. unaeneza propaganda kwamba wewe si mwenzao, propaganda hizo zimeenezwa mapaka kwenye chama chako cha msingi na kukishawishi, au kukilazimisha, kikufukuze uanachama. Una kauli gani juu ya hilo?

Muhandiki: Ni kweli mimi sio mwenzao. Siendi kwenye ushirika kuiba pesa ya wakulima kama wafanyavyo wao. Mimi niko tayari kutumia gharama zangu kuhakikisha ushirika unasimama na wanaushirika wananufaika. Hao wanaosema mimi si mwenzao wanafanya kinyume. Wao wanautegemea ushirika uwasimamishe huku ushirika wenyewe ukianguka. Kwenye chama changu cha msingi sitarajii wausikilize upuuzi wanaoletewa na viongozi wa chama kikuu.

Swali: Kuna habari kuwa umefukuzwa kwenye kikao cha KCU (1990) Ltd. ukiwa mjumbe halali. Unalisemaje tukio hilo na unalichukulia hatua gani?

Muhandiki: Ni kweli nimefukuzwa na mwenyekiti na sikupenda kuuliza maswali kutokana na kumheshimu. Kwa ufupi hakufuata kanuni tena mbele ya Mrajis Msaidizi.

Swali: Zipo tuhuma na shutuma dhidi yako kuwa unatoa siri za ushirika na kukipaka matope chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. kwenye vyombo vya habari. Ni kweli unafanya hivyo?

Muhandiki: Hapana. Mimi sio mwandishi wa habari. Ni kwamba baadhi ya wakulima wa kahawa wanao ndugu zao ambao ni waandishi wa habari. Inawezekana kabisa habari zikawa zinafika kwenye vyombo vya habari kwa njia hiyo pia. Lakini hatahivyo, kama uongozi unajiamini ni msafi kuna haja gani ya kuvihofia vyombo vya habari?

Swali: Unadhani ni siri gani unazotuhumiwa nazo ambazo hazipaswi kuwekwa kwenye vyombo vya habari na kwa nini zinafanywa siri wakati katika chama cha ushirika hapafanyiki uchawi?

Muhandiki: Sijui. Ila nadhani inatokana na kuulizwa maswali juu ya matumizi ambayo hawawezi kuyatolea maelezo. Mfano, utanunuaje hoteli mpya, kama walivyonunua Yasillah Hoteli wakati hoteli kongwe kama ile ya Lake ikioza?

Swali: Wakati akiongea juu ya ushirika, katika Bunge linaloendelea, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Chiza, alisema kwamba ushirika nchini kote umeoza. Wewe kama mjumbe katika chama kikuu cha ushirika unaichukuliaje kauli hiyo ya waziri?

Muhandiki: Ni kweli kabisa. Kama sehemu nyingine nako mambo ni kama haya ya KCU (1990) Ltd. kweli ushirika nchini utakuwa umeoza vibaya. Ila nasikitika kwamba waziri huyo alikuja Bukoba akajionea kila kitu lakini akakubali kuondoka na kuuacha uozo jinsi alivyoukuta. Hata tunapopiga kelele anakuwa kama hatusikii!

Swali: Na ni nini maoni yako juu ya hatima ya KCU (1990) Ltd.?

Muhandiki: Kama haya mambo yanafanyika waziwazi namna hii bila kificho, mbele ya macho ya waziri na mbele ya macho ya kila mtu, na wakati mwingine hata mbele ya macho ya rais, hatma ya ushirika nchini ni lazima iwe mashakani. Na kwa maana hiyo hata KCU (1990) Ltd. tusitegemee kama kinaweza kuwa na maisha marefu kama hali inaachiwa iendelee kuwa hii tunayoishuhudia kwa sasa. Uozo huu waziri kaja kaushuhudia na kuuacha, naogopa kusema kwamba kaupa Baraka zake ili KCU (1990) Ltd. kiwe kichaka cha ufisadi.

Niko tayari kugharamia ukaguzi wa mahesabu ya KCU (1990) Ltd. kama inakubalika ufanywe na CAG badala ya COSCO ambao inaonekana kwamba wameshindwa kazi kabisa.

Hayo ndiyo mazungumzo yangu Na Mzee Archard Felician Muhandiki kufuatia habari za kwamba uongozi wa chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. unampiga vita kiasi cha kumfukuza hata kwenye mkutano mkuu wa makadirio ya chama hicho akiwa mjumbe halali.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau