Bukobawadau

Mchakato wa katiba mpya: Chadema igeni hekima za Nyerere na Mandela

Na Prudence Karugendo

KUNA habari ambazo hazijawa rasmi kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo kina mpango wa kuususa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya baadhi ya mapendekezo ya chama hicho kuonekana kwamba hayakuzingatiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Habari hizo kwangu sio njema hata kidogo.

Sio njema kwa sababu gani? Ni kwamba wazo la katiba mpya ni la Chadema. Watawala chini ya chama chao cha CCM walikuwa wanalipinga wazo hilo kwa nguvu zao zote, lakini baadaye wakaja kuliteka wazo hilo na kuligeuza la kwao baada ya kusoma alama za nyakati. Mpaka hapo inaonekana kwamba CCM, wanapenda wasipende, wanalazimika kuicheza midundo inayoporomoshwa na Chadema.

Hiyo maana yake ni kwamba midundo ya Chadema ni ama ni mizuri kiasi cha CCM kuishiwa uwezo wa kujizuia kuinengua au chama hicho kikongwe hakina aina nyingine ya midundo kinayoweza kuinengua badala ya hiyo ya Chadema kutokana na utovu wa ubunifu unaokikabili chama hicho tawala. Tayari huo ni ushindi wa wazi kwa Chadema.

Kwahiyo wazo la Chadema kutaka kususia mchakato wa upatikanaji wa kitu kilichotokana na ubunifu wake kwa madai kuwa CCM wameingiza mambo au kuyakiuka mengine yaliyo katika makubaliano ya awali, nalichukulia sawa na mwindaji aliyehangaika sana kumpata mnyamapori na kisha kumsusia fisi nyama yote eti kwa sababu fisi kala bila kunawa. Fikiria unapoamua kumsusia fisi nyama ukidhani unamkomoa!

Uamuzi wa Chadema, kama kweli upo, wa kususia mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya ya nchi yetu hauna tofauti yoyote na uamuzi wa mwindaji kumsusia fisi nyama. Ni lazima fisi atakula nyama huku akimshukuru Mungu kumwezesha mwindaji kufanya uamuzi huo. Kwahiyo kibusara ni bora kutomsusia fisi nyama.

Ieleweke kwamba katiba mpya ni pigo kubwa kwa CCM ambacho muda wote kimekuwa kikilindwa na katiba ya chama kimoja cha siasa na kukifanya chama hicho kiendelee kuonekana ni chama dola hata baada ya ujio wa vyama vingi vya siasa.

Ni katiba hiyo ya zamani iliyokifanya chama hicho kikabweteka ikiwa imekikosesha ubunifu katika mambo mengi mbalimbali ukiwemo ubunifu wa kuwatumikia wananchi kwa ufasaha na kuwaletea maendeleo yanayoendana na umri wao wa kuyatafuta.

Kwa mantiki hiyo katiba mpya, pamoja na mambo mengine, inatishia kukiondolea CCM uadhimu wake wa kuendelea kuwa chama dola.

Ni wazi kwamba CCM inaanza kuliona kaburi lake likitayarishwa wakati haijakata roho. Ni lazima chama hicho kirushe mateke walau kujaribu kuchelewesha mchakato huo wa kaburi lake hata kama kinaelewa kuwa kufa ni ahadi inayoelekea kutimia. Ni lazima CCM ifanye fujo za hapa na pale kama inavyoweza kutokea kwa kiumbe yeyote anayeyaona mauti mbele yake.

Wahaya wanausemi kwamba “bakuroga wakunda wagalya” yaani kwamba maadui zako wanakufanyia uchawi huku ukiona na wewe unakubali kuupokea uchawi huo. Chadema kinaelewa kuwa CCM kilikuwa hakiitaki katiba mpya, na bado hakiitaki hata sasa, ndiyo maana kinafanya vituko katika mchakato huu unaoendelea mpaka Chadema kinataka kususa! Hiyo maana yake ni kama Chadema inataka kuupokea uchawi wa CCM!

Nikumbushe mbinu zilizotumiwa na wakoloni kutaka kuuchelewesha uhuru wa Tanganyika na kuivurugia TANU. Wakoloni kwa kuelewa kuwa Nyerere alikuwa na msimamo unaopingana na ubaguzi wa rangi wakabuni utaratibu wao unaopingana na msimamo wa Nyarere, utaratibu wa kupiga kura 3 katika chaguzi. Yaani kura ya Mwafrika, Muasia na Mzungu.

Lengo la wakoloni lilikuwa Nyerere na TANU yake wasusie chaguzi zilizo katika utaratibu huo wa kibaguzi, iwe vurumai baadaye wakoloni wapate kisingizio cha kuchelewesha uhuru wa Tanganyika.

Lakini Nyerere kwa kuwazidi ujanja wakoloni akaamua kumchinja ng’ombe alivyolala bila kuhangaika na kibula. Akachukua uamuzi mgumu wa kukubaliana na utaratibu huo wa kibaguzi uliokuwa umechomekwa kwa hila. Hatahivyo alipata wakati mgumu wa kulifafanua hilo kwa wananchi waliokuwa wakiamini kwamba Tanganyika ni ya Watanganyika, haikuwa ya Waasia wala wazungu.

Ni katika hatua hiyo ndipo Mwalimu alipojikuta machozi yakimtoka Januari, 1958, mjini Tabora hasa baada ya kuwashuhudia wenzake, Zuberi Mtemvu na wengine, wakijtenga na TANU na kuanzisha Tanganyika African Congress kwa kuupinga utaratibu huo wa kura 3.

Lakini baada ya uhuru hatukuyaona tena ya kura 3. Msimamo wa Nyerere ukawa uleule wa kutopenda kuusikia ubaguzi wa rangi. Nyerere akawa amewapiga wakoloni bao la kisigino.

Mfano mwingine katika hili ni wa makaburu wa Afrika Kusini. Kutokana na kuihofia sana ANC, makaburu wakamshawishi Gatsha Buthelezi ambaye kwa kipindi kirefu alionekana kama kibaraka wao, ili yeye na chama chake cha Inkatha Freedom Party waanzishe vurugu ili kujaribu kuharibu uchaguzi wa 1994. Lakini ANC, chini ya uongozi makini wa Mandela, wakawa wavumilivu na kuyanyenyekea madai ya kipuuzi ya Buthelezi mpaka akakubali kushiriki uchaguzi.

Mpaka hapo tunaona kwamba usemi wa mtaka cha uvunguni hulazimika kuinama unajileta wenyewe. Kwa vile Chadema ndiyo inayoona umuhimu wa katiba mpya, ni wazi CCM haiuoni umuhimu huo, inabidi izivumilie hila zote zinazofana.
Next Post Previous Post
Bukobawadau