Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA AWATOA HOFU WANANCHI KUHUSU M23

Kagera. Serikali mkoani hapa imewataka wananchi walioko wilaya zinazopakana na nchi jirani kutokuwa na hofu ya usalama baada ya tishio la Kundi la Waasi la M23 la DRC kutishia kuvamia Tanzania.
Akiongea na wandishi wa habari wilayani Ngara, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Masawe alisema kuwa, wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano na kuwabaini watu wasio wafahamu watakaojipenyeza kwa kutoa taarifa ili waweze kushughulikiwa kikamilifu
Masawe alisema, Serikali iko macho kuhakikisha mipaka yake haivamiwi na kwamba kufuatia taarifa hizo hatua za kiusalama zimeshachukuliwa kwa kutandaza vikosi mbalimbali vya usalama kwenye mipaka yake na nchi jirani.
“Atakayejilengesha kuivamia Tanzania atakutana na kilichomg’oa Nduli Iddi Amini wa Uganda katika vita vya mwaka 1978-79, nami nilikuwa mpiganaji mahiri,” alisema Masawe.
Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantin Kanyasu aliiomba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuingilia kati na kuilinda mipaka ya Kijiji cha Kasange wilayani humo na ileya vijiji vinavyopakana na Wilaya ya Giteranyi Burundi.
Kanyasu alisema, wananchi wa maeneo hayo wanagombea ardhi kwa jili kilimo kwa kila mmoja kujiona kuwa yupo sahihi ndani ya nchi yake na hivyo kuzua tafrani katika uhusiano wa pande zote mbili.
Aliiomba Wizara ya Jumuia ya Afrika ya Mashariki kufanya mazungumzo ili kupatikane suluhu ya usalama wa wananchi wa nchi hizo mbili kwa kukaa meza moja pamoja na kudhibiti wahamiaji haramu wanaotoka nchi wanachama wa shirikisho hilo bila kufuata taratibu za kuhamia nchi nyingine.
Hata hivyo Kanali Masawe amewataka wananchi na viongozi wa maeneo hayo kuwashauri wanaotaka kuingia nchini na kuishi kujiandikisha kwa kufuata taratibu na kuwa raia wa kuandikishwa.
Next Post Previous Post
Bukobawadau