Bukobawadau

RAI YA GENERALI ULIMWENGU TUNADANGANYANA, TUNAJAZANA UJINGA

Na Jenerali Ulimwengu,

NALAZIMIKA kurejea mada yangu ya muda mrefu, mada inayojadili jinsi tunavyofanya mambo kama watu wa kupita huku tukishindwa kuangalia masafa marefu kama Taifa linaloamini kwamba litakuwapo hapa hapa kwa muda mrefu. Wiki iliyopita nilijadili suala la zahhama kubwa ya watoto wa kidato cha pili kushindwa vibaya katika mitihani ya mwaka jana, suala ambalo watawala wetu wamelishughulikia kwa staili ile ile ya fasta-fasta.

Nlitoa mfano wa nyoka unayekutana naye porini na yule unayekutana naye kitandani. Yule wa porini hawezi kukushangaza kwa sababu umemkuta katika maskani yake, lakini huyu wa kitandani ni lazima atakushangaza kwa sababu humtarajii awe kitandani kwako.

Kufeli kwa wanafunzi wetu ni kama nyoka tunayekumbana naye mwituni, kwa sababu mazingira ya kufeli yapo tayari, tunajua kwamba yapo, na tunatakiwa tujue kwamba tumeyatengeneza sisi wenyewe. Kujifanya tunashangazwa na matokeo hayo ni dalili nyingine ama ya unafiki ama ya ushirikina, ama ya yote mawili.

Tafiti zimekuwa zikifanywa kudhihirisha kwamba tunayo idadi kubwa mno ya watoto ambao wako shuleni kama sanamu. Hakuna wanachojifunza isipokuwa tabia za kuambukizana za watoto wanaojikuta katika mazingira ya kujilea wenyewe.

Hizi ni shule zisizokuwa na walimu, ambao kwa kawaida ndio wanatakiwa kuwa walezi wa watoto wanapokuwa shuleni, mbali na wazazi wao. Zinapokuwa na walimu, nao wanakuwa ni walimu sanamu, watu wasiokuwa na uwezo wa kuwaelekeza watoto kwa sababu wao wenyewe hawajapata maelekezo yanayotosheleza kuwafanya waweze kuwaelekeza watu wengine. Inakuwa ni ile hadithi ya Bwana Yesu ya kipofu kumuongoza kipofu mwenzake.

Ni shule pia zisizokuwa na vitabu wala nyenzo nyingine za kufundishia, zisizokuwa na maktaba wala maabara. Ni shule bubu, ambazo sifa yake pekee ni kwamba zinayo majengo ya madarasa na kibao kimewekwa mbele yake kutangaza kwamba hizi nazo ni shule.

Tumekuwa na taarifa za wazazi ambao wamekuwa wakweli mno, kiasi cha kuwaendea walimu na kuwaambia kwamba haiwezekani watoto wao kufaulu katika mtihani kwa sababu wanajua kwamba watoto wao hawajui kitu. Kwa maneno mengine mzazi anaona kwamba mfumo mzima wa elimu unamtapeli kwa kujaribu kumdanganya kwamba mtoto wake amefaulu wakati yeye, kama mzazi, anajua kwamba hakuna jinsi huyu mtoto wake anaweza kufaulu.

Aidha tunajua, au tunapaswa kujua, kwamba wapo wazazi ambao wanatoa vishawishi (sitaki kusema “rushwa”) ili maofisa wa serikali kijijini wasiwalazimishe kuwapeleka watoto wao shule. Hii ni kwa sababu watoto wanaokwenda shule kwa miaka saba wanapoteza miaka saba wakijifunza ujinga shuleni na wanakuwa wamebadhiri miaka saba ambayo wangeweza, kama wangebakia nyumbani, kujifunza kilimo, ufugaji, uvuvi na mengine ya namna hiyo.

Hii inamaana kwamba wazazi, na jamii kwa ujumla, wamekwishakukata tamaa kuhusu mifumo ya elimu na thamani inayoongezwa na mifumo hiyo katika maisha ya jamii. Kwa maneno mengine, kwa kiasi kikubwa, mifumo yetu ya elimu imekufa.

Hili si jambo la kudhani wala si jambo la kubuni. Nchi yetu hivi sasa haina mfumo wa elimu tunaoweza kuutamka kwamba ndio mfumo wa elimu wa Taifa letu, na kwa maana hiyo mifumo ya elimu inayoenenda sambamba nchini (kila anayeweza anafanya ajuavyo) inasaidia kupunguza utaifa wetu na kuzidi kutufanya mkusanyiko mkubwa wa watu.

Dalili zinaonekana waziwazi kabisa, na mwenye macho haambiwi ”ona.” Wazazi wenye uwezo wa kifedha wanawasomesha watoto wao katika shule za aina Fulani ambazo wazazi wengine hawawezi kuzimudu. Hii ni hali ambayo nilikwisha kuiandikia kama hali yenye kuongeza kasi ya mifarakano ndani ya jamii yetu. Hii ni kwa sababu jamii isiyolea na kukuza vizazi vyake juu ya misingi iliyokubaliana haiwezi kuwa jamii yenye utangamano.

Tumejenga mazingira ya ujuha, nasi tumejitosa ndani ya ujuha huo, na sasa tunaogelea mumo. Tunao wazazi wanaodhani kwamba wakiwapeleka watoto katika shule ziitwazo “academy” na majina mengine ya kuchekesha, na watoto wakirejea nyumbani wakizungumza “Kizungu” hiyo ndiyo elimu.

Nimewashuhudia watoto na wazazi wao wakilazimishana kuzungumza “Kizungu” nyumbani mwao kiasi kwamba unajiuliza ni nini hasa wanataka kukuonyesha: kwamba mtoto hajui Kiswahili, achilia lugha ya asili ya baba au mama? Tumekuwa wajinga wa kupindukia, na tunaongozana kuelekea ujinga mkubwa zaidi kila siku.

Fikira kwamba katika shule hizi ambazo hazina walimu, wakiwapo walimu hawana uwezo, na hazina nyenzo, na hazina maelekezo ya kutosheleza kufanya kazi zao kama inavyopasa, halafu zimeongezewa kufundisha katika lugha isiyoeleweka, si kwa mwanafunzi wala kwa mwalimu.
Hivi sasa tunazo shule nyingi kote nchini ambazo zimejaa walimu wanaokazana kweli kweli kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia lugha ambayo walimu na wanafunzi hawaielewi, na wala haitatokea siku wakaielewa. Lakini tumekazana tu, lazima watoto wasome kwa kutumia “kizungu” kwa sababu hiyo ndiyo elimu, kwa kuwa tulikwisha kuambiwa eti “Kiingereza ndicho Kiswahili cha dunia.” 

Ujinga mtupu.
Nchi ndogo ndogo kabisa, ambazo idadi za watu wao hazifiki hata asilimia tano ya idadi ya Watanzania, zinafundisha watoto wao kwa lugha zao. Sisi wenye watu milioni arobaini na tano u shey, ambao wanazungumza aina moja au nyingine ya Kiswahili, tunadhani kwamba Kiingereza ndiyo elimu, na hata kama watoto hawakielewi na walimu wao pia lazima watumie lugha hiyo!

Hii ni aina ya ujuha wa kushangaza, hasa kwa sababu ushahidi u wazi kwa kila anayetaka kuuona. Tatizo ni kwamba hatutaki kutazama kule ushahidi huo ulipo; tumeangalia kwingine kwa kuogopa kwamba ushahidi huo ukiisha kudhihirika utatuonyesha jinsi tulivyokuwa wajinga kwa muda wote huu.

Sasa, inapotokea watawala wetu wakakabiliwa na ushahidi wa kutisha, kama huu wa mitihani ya mwaka 2012, watawala, kwa hofu ya kuwajibishwa na wananchi, kama kawaida yao, wana majibu ya haraka sana: chapa bakora, futa matokeo. Dhahiri, tumeshindwa kabisa kufikiri.
Mbeleya safari, nitajaribu kuonyesha sehemu tu ya ushahidi huo, kwa mara nyingine tena.

RAIA MWEMA
Next Post Previous Post
Bukobawadau