Bukobawadau

RIPOTI JUU YA KUTEKWA KWA KIBANDA YATOLEWA.

Ifuatayo ni ripoti kamili ya uchunguzi:

Utangulizi:

Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi Juu, Dar es Salaam.

Tukio hilo lilishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa jumla hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio lililomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni 26, 2012.

Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.

Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.
Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo ilikuwa kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi.

Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi kuwa upo uwezekano na dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad, iphone na Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu wao.

Kibanda aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila ganzi. Watekaji hawa, katika unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.

Hali hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki. Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.

Katika kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na kuipa hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini limetokana na nini.

Timu hiyo iliundwa kutokana na uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF).

Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa waandishi yanapungua kila mwaka.

Timu hii imefanya kazi usiku na mchana kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili. Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake.

Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya Serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.

Leo tunawasilisha muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake, itachapishwa na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa kuchapisha habari ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya kuieleza jamii maajabu juu ya kadhia hii.
Hadidu rejea:

Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.

Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikita katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.

Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.

Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.

Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.



Yaliyojiri katika uchunguzi:

Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi dhidi yake.

Timu ya uchunguzi ilitumia muda mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya wazi yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii.

Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata kufikiri kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama ifuatayo:-

1.1. Wiki tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni

na baadaye likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo walisimamisha magari yao na kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa wanatilia shaka magari yao. Baada ya kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.

1.2. Usiku wa Februari 25, mwaka huu majira ya saa 9:00 usiku, Kibanda alivamiwa na watu walioingia kwenye uzio wa nyumba yao wakavunja kioo cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa ‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.

1.3. Kutokana na uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio mmoja, waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.

1.4. Kuna askari anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata kumpa Kibanda taarifa za kintelijensia.

Inaendelea kesho

kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na kumuumiza. Taarifa kama hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi. Kwa maneno yake Kibanda alisema:

“Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi kuniambia ‘unaandika sana usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini nyumbani kwako’. Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari sana.

“Wiki mbili kabla ya tukio, niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi wakachelewa kuja kunifungulia, niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha kabisa.

“Pia kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea.”

1.5. Ndani ya miezi mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa mara kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta damu. Haikufahamika kama damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani ni masuala ya ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa,
ITAENDELEA KESHO
Next Post Previous Post
Bukobawadau