TUMUENZI NYERERE BILA KUFANYA DHIHAKA
Kumuenzi mtu ni kumpa heshima ya kuendelea kukumbukwa kulingana na
thamani ya mchango wake alioutoa kwa jamii aliyokuwa akiitumikia. Jamii yoyote
huamua kumuenzi mtu kutokana na mema aliyoitendea. Ni nadra sana mtu kuenziwa kwa mabaya yake. Kwa vile
kuenzi ni kutoa heshima hapanabudi utaratibu maalumu ufuatwe ili kujenga picha yenye
kutoa maana inayoeleweka ambayo muhimu zaidi ni kuisimika heshima maridhawa kwa
mlengwa.
Inabidi pawepo na utaratibu maalumu wa kumuenzi muhusika sanasana akiwa
wa ngazi ya Kitaifa ili kuzuia watu wanaoweza kupotosha maana ya jambo hilo kwa kufanya mambo
yanayoweza kuchafua jina la mtu maarufu katika jamii kwa kisingizio cha
kumuenzi.
Hapa nchini kwetu jina la Julius Kambarage Nyerere ni jina kubwa
ambalo, sina shaka, litaendelea kuwa kubwa kuliko majina yote ya Watanzania
waliobaki kwa kipindi cha miongo mingi kama
siyo karne nyingi zijazo. Nyerere ni kiogozi wetu, mwalimu wetu na Baba yetu,
ambaye hata kabla hafariki dunia tulikubaliana, pasipo mtu yeyote kubisha,
kumuenzi kama Baba wa Taifa. Hii ni heshima ya
pekee tuliyoamua kumtunukia bila kulazimishwa na nguvu yoyote bali msukumo wa
mapenzi yetu kwake, mapenzi yaliyomfanya kila Mtanzania amchukulie Nyerere kama mmojawapo wa wanafamilia yake. Kila Mtanzania
alimuona Nyerere kama mwanafamilia wake.
Mapenzi ya Watanzania kwa Mwalimu Nyerere yalianza kujionyesha punde tu
alipoamua kuacha kazi ya ualimu na kuingia kwenye siasa akiwa na lengo la kutia
msukumo wa nchi yetu kupatiwa uhuru, Tanzania bara, wakati huo ikijulikana kama Tanganyika.
Ni wakati huo wananchi walipoanza kumuenzi Nyerere kwa kuwapa watoto wao, hasa waliozaliwa
kuanzia kipindi hicho, majina yaliyokuwa yanadhihirisha mapenzi yao kwa mwalimu. Watoto
wengi walipewa majina ya Julius, wengine wakaitwa Kambarage na wengine kuitwa Nyerere.
Ukiondoa jina la Julius ambalo ni jina la Kizungu linalotumika huku kwetu kama jina la kidini (la Kikristo), yaliyobaki yaani
Kambarage na Nyerere ni ya kikabila, bilashaka ya Kizanaki, lakini hatahivyo wananchi
waliyatumia wa makabila mbalimbali bila kujali asili yake na wala maana yake.
Watanganyika na baadaye Watanzania walijali zaidi kwamba asili ya majina hayo
ni mtu abaye tayari alikuwa mtu wao.
Pia wananchi walimjengea Nyerere uadhimu wa pekee wanaoendelea
kuuhifadhi mpaka leo pamoja na ukweli kwamba Nyerere hatukonaye kimwili.
Utasikia katika maeneo mbalimbali ya nchi, watu wanapotaka kusisitiza jambo,
mfano, kitu fulani hakiwezi kufanyika labda kama
angekuja Nyerere! Siku fulani nikamsikia mtu mmoja anapinga kwamba hawezi
kupokea barua ya kuitwa Mahakamani akisema kwamba labda kama
ingekuwa na sahihi ya Nyerere! Sio kwamba wanaosema hivyo hawajui kuwa alitoka
Nyerere akaja Mwinyi baadaye Mkapa na
sasa tunaye Kikwete, ila hii inaonyesha imani iliyojengeka katika mioyo ya
wananchi kwamba pamoja na Nyerere kuwa Rais kama
hawa waliomfuatia bado ukubwa wa jina lake ni
wa pekee.
Isitoshe kuna vitu vingi ambavyo tayari vilishapewa majina ya Nyerere kama kumbukumbu yake. Kuna shule nyingi za sekondari na
hata za msingi zinazoitwa Nyerere au Kambarage. Ukitembelea kila mji na kila
jiji hapa nchini ni lazima utakutana na
mitaa inayoitwa ama Nyerere au Kambarage
au yote mawili. Huu ni ushahidi tosha kwamba Mwalimu tumemuenzi kiasi cha
kuridhisha. Zaidi ya hapo tutajikuta tunamchafulia jina. Nitaeleza kwanini.
Kwa sasa suala la kumuenzi Nyerere limebaki kuwa suala la Kitaifa. Na
linapaswa kuwa la Kitaifa kwelikweli kwa maana ya Taifa kusimamia pamoja na
kudhibiti matumizi ya jina la Mwalimu Nyerere, huko ndiko tunakoweza kukutaja kama kumuenzi Nyerere. Tena Taifa lisiishie kufanya
mabadiliko tu tunayoyaona yakifanyika katika kile kinachoitwa kumuenzi Nyerere,
mabadiliko ambayo ni pamoja na kutaka kubadili karibu majina ya kila kitu na
badala yake vitu hivyo kuviita majina ya Nyerere! Kumuenzi Nyerere ni zaidi ya
matumizi ya jina lake.
Katika jiji la Dar es Salaam
peke yake jina la Nyerere linaelekea kupoteza umuhimu wake kutokana na vitu
chungu nzima kupewa jina la Nyerere. Ngoja nitaje baadhi. Iliyokuwa inaitwa
barabara ya Pugu (Pugu road) ilibadilishwa jina na kuitwa barabara ya Nyerere
(Nyerere road). Uwanja wa maonyesho ya Kimataifa ya biashara uliokuwa
ukijulikana kwa wakazi wa Dar es
Salaam kama uwanja wa
Sabasaba umebadilishwa jina na kupewa jina la Nyerere. Iliyokuwa ikiitwa Nyumba
ya sanaa sasa hivi ni kituo cha sanaa cha Mwalimu Nyerere! Uwanja wa Kimataifa
wa ndege wa Dar es Salaam
nao umebadilishwa jina na kupewa jina la Nyerere. Tena hii ni kwa upande ambao
mabadiliko hayo yanatolewa maamuzi na serikali au kupitia kwenye asasi zake.
Bado kuna maamuzi ya kulitumia jina la Baba wa Taifa yanayotolewa na
watu na asasi binafsi kama ulivyotolewa uamuzi
wa kulipa jina la Nyerere lile jumba la sinema la Mwenge linalomilikiwa na
mpenzi wa kutupa wa Mwalimu Nyerere Mzee Sabodo.
Mbali na hapa Dar es Salaam kuonekana jina la Nyerere limezagaa kila
pahala, mikoani nako mambo yako vilevile. Mara utasikia maonyesho ya kilimo ya
Nyerere kule Morogoro, bustani ya Nyerere kule Dodoma nakadhalika.
Nafikiri umefika wakati serikali ichukuwe uamuzi wa kudhibiti matumizi
ya jina la Baba wa Taifa ili kulinda hadhi na thamani yake ikiwa ni njia mojawapo kuu ya kumuenzi mzee
wetu. Kuliachia jina la Nyerere likaendelea kutumika kihorera isichukuliwe kuwa
ni njia ya kumuenzi tu vilevile inaweza ikawa njia ya kumfanyia dhihaka.
Fikiria mtu anaamua kumuita ndama wake aliyezaliwa jina la Nyerere kwa
kisingizio cha kulienzi jina hilo!
Sidhani kama utakuwa mwendelezo wa kulienzi jina la Baba wa Taifa kama
kutatokea hata zile sehemu zinazotumika kunajisi maadili ya jamii nazo zikaanza
kupewa majina ya Nyerere kwa madai ya kulienzi jina hilo. Hebu fikiria patakapojitokeza vitu kama
Nyerere guest house, Kambarage lodging, Nyerere pub au J. K. Nyerere camp
wakati tukielewa kwamba camp zilizo nyingi ni magenge ya kuvutia bangi na
madawa ya kulevya.
Ningeshauri vitu vilivyopewa majina ya Nyerere vipunguzwe ili kuleta
maana muafaka ya matumizi ya jina hilo.
Matumizi horera ya jina la Nyerere si kitendo cha kulienzi jina hilo
hata kidogo, kinyume chake, ni kwamba litaanza kushuka hadhi. Hii ni kwa sababu
kitu kikiwa chekwa kikakosa uhadimu thamani yake inashuka na ubora wake
unapotea. Kwahiyo kuzidi kuyatumia majina ya Baba wa Taifa kwa vitu mbalimbali
bila ulazima wa msingi kunaweza kuonekana kama
dhihaka badala ya heshima tunayolenga kumpa huyu mwasisi wa Taifa letu.
Kitu kingine ni kwamba matumizi haya tusipokuwa waangalifu, yanaweza
yakaipotosha jamii ikajikuta inamuelewa Nyerere katika maana tofauti na ile
inayokusudiwa na hao watumiaji wa jina hilo.
Kutokana na nchi yetu kukosa utamaduni wa kuvitunza vitu vyake katika hali ya
unadhifu upo uwezekano mkubwa wa vitu vilivyopewa majina ya Nyerere kuvikuta
katika hali ya shaghalabaghala. Inaweza ikatokea barabara zote zinaitwa Nyerere
zikawa mbovu kutokana na kutofanyiwa ukarabati. Mathalani, mtu anatoka Mwanza
anaacha barabara ya Nyerere ina mashimo, anafika Dar anakuta barabara ya
Nyerere iko vilevile kama ya Mwanza,
picha inayojengeka kichwani ni nini hasa kwa watoto? Vivohivyo kwa vitu
vingine vilivyopewa majina ya Nyerere kila mahali, picha inayojengeka ni kwamba vitu vinapokuwa
vibovu ndipo vinapoitwa Nyerere!
Au yanaweza yakajengeka mazoea kwamba kitu kikiwa na urefu fulani
kinaitwa Nyerere, au kikiwa na ukubwa fulani kinaitwa Nyerere! Yakaja kujitokeza
yaleyale ya jamaa zetu fulani waliokuwa wameyazoea maghorofa ya hospitali ya
Bugando ya jijini Mwanza na kujijengea imani kwamba kila mji waendako na kukuta
maghorofa basi ni Mabugando! Sasa hii itakuwa kumuenzi Nyerere au kumdhihaki?
Kwa upande mwingine Kanisa nalo limeanza mchakato wa kumuenzi Nyerere
kwa kutaka kumtangaza kwamba ni mwenye heri. Ingawa sielewi hii ina maana gani,
sababu mimi naamini kwamba maamuzi ya Mwenyezi Mungu hayana ushawishi kutoka
kwa wanadamu sababu Mungu si mla rushwa, bado hii nayo itaendelea kulitangaza
jina la Nyerere tena kwa njia ambayo nadhani ni bora zaidi kuliko hata ile
inayotumiwa na serikali. Tutaanza kuyaona makanisa yanayoitwa Mwenye heri
Nyerere na vitu vingine vinavyomilikiwa na kanisa hilo.
Mambo yanayonivutia kwa upande wa uamuzi wa Kanisa wa kumuenzi Nyerere
ni mawili. Jambo la kwanza ni kwamba kanisa linapoamua kumuenzi mtu linaangalia
zaidi matendo yake wakati wa uhai wake kuliko umaarufu aliokuwa nao. Kwahiyo
katika mchakato wa Kanisa wa kumtangaza Nyerere mwenye heri waamini wote wa
Kanisa hilo
wanatakiwa kuyazingatia na kumuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe kuyatekeleza kwa
vitendo yale yote yaliyokuwa yakielekezwa na Mwalimu Nyerere. Waamini hao
watamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie ujasiri wa kuvichukia vitu alivyokuwa
akivikataza Nyerere. Mfano, ujasiri wa
kuiona rushwa kwamba ni adui wa haki kama
alivyo eleza Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.
Vilevile kuyakataa yote aliyokuwa akiyakataza Mwalimu,kama
vile ubaguzi katika misingi ya kabila na rangi. Wizi wa mali ya umma, ufisadi
wa kujitajirisha kwa mtindo wa kujirundikia mali, uonevu na ukandamizaji kwa
lengo la kuhodhi na kuyang’ang’ania madaraka nakadhalika. Kwa misingi hii
Kanisa litatuonyesha njia iliyo sahii ya kumuenzi Baba wa Taifa hata kama kufanya hivyo
hakutupi uhakika wa moja kwa moja kwamba hicho kinaweza kuwa kishawishi cha
kumshinikiza Mwenyezi Mungu kutengua maamuzi yake. Ila kwa vile tunaamini na
kuabudu kwamba Mungu ni mwema hatuna haja ya kutilia shaka mapendekezo yetu
kwake.
Uzuri wa pili ninaouona katika mchakato wa Kanisa wa kumuenzi Nyerere
ni huu: Baba wa Taifa , mpaka mauti yalipomfika, alikuwa akilalamikia umasikini
unaozitesa nchi zinazoitwa eti za dunia ya tatu, nchi yake Tanzania ikiwa
miongoni mwa zile zilizo taabani kabisa. Litakuwa jambo la faraja kwake, kama
upo uwezekano wa yeye kutokea kule aliko kuyaona yanayotendeka huku nyuma,
akiona jina lake linachangia kuinua uchumi wa nchi yake
na watu wake kupata ahueni.
Tukiweka imani pembeni, kitendo cha kumtangaza mtu kuwa ni mwenye heri
na baadaye mtakatifu kinalenga zaidi katika uchumi wa sehemu husika. Sababu
hicho ni kivutio cha utalii wa aina yake. Sina takwimu sahihi kutoka Maliasili
na Utalii ili kujua tunapata watalii
wangapi kwa mwaka wanaotembelea nchi yetu kwa ajili ya vivutio mbalimbali, ila
sidhani kama wanafika milioni moja. Sasa kwa
kivutio kimoja cha Mwenye heri Julius Kambarage Nyerere, sintashangaa tukipata
watalii zaidi ya milioni nne kwa mwaka! Kwa hilo nalipongeza Kanisa katoliki kwa upeo wao
wa kuona mbali.
Tofauti na Kanisa, serikali inasisitiza kumuenzi Nyerere lakini kwa
njia ambazo zinaonekana wazi kwamba ni dhihaka, kebei, kejeli na uzandiki.
Huwezi kusema kwamba unamuenzi Nyerere kwa kutenda mambo ambayo yalikuwa haramu
kwake na mpaka anakufa alikuwa akiyalaani. Huko si kumuenzi ila ni kumdhihaki.
Tendo la kupachika jina lake kwa
karibu kila kitu lakini yakipuuzwa yale yote aliyokuwa akiyahimiza yafanyike ni
kumkejeli si kumuenzi.
Inawezekana jina la Nyerere likawa bado linahitajika na utawala wa sasa
ili liusaidie kujiimarisha madarakani kwahiyo ikawa sababu ya utawala kuonekana
unalienzi jina hilo, huu ni uzandiki!
Mpaka katika hotuba zake za mwishomwisho Mwalimu alikuwa anasisitiza
jinsi ilivyo vigumu kwa mwanadamu kutumikia mabwana wawili, yaani kutumikia mali na
kumtumikia Mungu. Viongozi wa watu ni watumishi wa Mungu. Maana yake ilikuwa kwamba wenye mali, matajiri,
ambao zamani aliwaita mabwenyenye, hawakufaa kuwa viongozi wa wananchi. Lakini
sasa hali ikoje? Asiyekuwa na mali
ndiye hafai kuwa kiongozi! Je, huku ndiko kumuenzi Nyerere?
Mwalimu alikuwa na msimamo kwamba raslimali asili za nchi hii si kwamba
ni za kizazi kilichopo kwa sasa peke yake, bali hata vizazi vijavyo karne
nyingi mbele. Ndiyo maana alikuwa anasisitiza kwamba zile raslimali asili
ambazo tulikuwa hatujaweza kuzishughulikia sisi wenyewe hatuwa na haja ya
kufanya haraka sababu alikuwa akiamini kwamba utafika wakati watakaokuwepo kwa
wakati huo wakawa wameishaweza kuzishughulikia wangefanya hivyo sababu nao ni
haki yao.
Lakini viongozi wetu wanasema hapana, hii ni haki(yao?)yetu, hata kama hatuna uwezo wa
kuishughulikia bora tukawatafute wenye uwezo huo wakaishughulikie na kuzoa,
potelea mbali chochote watakachoamua kutupatia si haba kuliko kuiacha eti kwa
ajili ya vizazi vijavyo! Vizazi vijavyo vitashughulikia mahandaki na milima
bandia inayotengenezwa na hao wataalamu wa kuchimba na kuzoa mali asili za
wenzao. Je, humu kuna dalili zozote za kumuenzi Nyerere?
Mwalimu amekufa akiwa bado ni muumini hai wa Azimio la Arusha. Na si
ajabu wakati anakata roho alikuwa na vitabu viwili mfukoni mwake, kama
alivyokuwa akitueleza kila mara, kitabu cha Biblia takatifu na kile cha Azimio
la Arusha. Azimio ambalo viongozi wa awamu ya pili walikaa kule Zanzibar mwanzoni mwa
miaka ya 1990 na kulipangua katika Azimio la kimyakimya lililokuja kujulikana kama Azimio la Zanzibar.
Wengi wa walioshiriki katika Azimio la Zanzibar
bado tunao hadi leo na wengi wamo katika Serikali ya awamu ya nne wanaendelea
kula kuku kwa mrija huku wakiwa mstari wa mbele wakiongoza wimbo wa kumuenzi
Nyerere!
Nyerere alikuwa anakataza mtumishi wa umma kutumia fursa hiyo
kujinufaisha na mali
ya umma au kuiba mali
ya umma. Kwa msimamo huo hata nyumba yake ya Msasani aliyoijenga kwa mkopo wa
Benki alikuwa ameamua kuisalimisha serikalini
baada ya yeye mwenyewe kukiri kuwa alishindwa kulipa mkopo wa benki. Leo
hii viongozi walioamua kujibinafsishia nyumba na maeneo ya serikali wanaimba
wimbo wa kumuenzi Nyerere! Hii kama siyo kejeli ni nini?
Tumemuona kiongozi mmoja aliyetumia ndege ya serikali (Jeshi) kufanya
ziara binafsi nyumbani kwao, alipoulizwa ilikuwaje naye akauliza, mlitaka
niende kwa baiskeli? Naye huyu anadai anafanya hivyo kwa kumuenzi Nyerere!
PRUDENCE KARUGENDO