Bukobawadau

Watuhumiwa bomu Arusha waachiwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewaachia kwa dhamana watuhumiwa wanaodaiwa kurusha bomu kwa waumini waliokuwa wamekusanyika kuanza ibada ya uzinduzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Mei 5, mwaka huu, jijini Arusha.

Hata hivyo, watuhumiwa hao wamepewa sharti la kuripoti polisi, pindi watakapohitajika kufanya hivyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema wamelazimika kuwaachia kwa dhamana kwa kuwa sheria haiwaruhusu kuendelea kuwaweka mahabusu kwa muda mrefu bila kuwafikisha mahakamani.

Hata hivyo, alisema wakiwa nje kwa dhamana, jeshi lake litaendelea na upelelezi na kuwahoji kila litakapokuwa likihitaji kufanya hivyo.

“Tumeamua kuwaachia sababu sheria haituruhusu kuendelea kuwashikilia muda mrefu na lengo letu hasa katika hili tukio hatutaki kumwonea mtu yeyote, ndiyo sababu tunafanya uchunguzi wa kina,” alisema.

Alisema hadi sasa hakuna ongezeko la mtu mwingine aliyefikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo zaidi ya Victor Ambrose Kalist (20).

Victor alifikishwa mahakamani Mei 13 mwaka huu, mbele ya Kaimu Hakimu Mwandamizi Mkazi wa Arusha, Devotha Kamuzora, kujibu mashtaka mawili ya kuua na kujaribu kuua na kesi yake itatajwa tena Mei 27, mwaka huu.

Watuhumiwa walioachiwa kwa dhamana ni Jassin Mbarak (29) mkazi wa Bondeni Arusha, Joseph Lomayani (18)

dereva wa pikipiki na mkazi wa Kwa Mrombo Arusha, George Batholomeo Silayo (23) mfanyabishara mkazi wa Olasiti na Mohamed Suleiman Said (38) mkazi wa Ilala Dar es Salaam.

Mei 13 mwaka huu, Kamanda Sabas, alisema watuhumiwa watatu raia wa UAE ambao ni Abdul Aziz Mubarak (30) mfanyakazi Mamlaka ya Mapato, Fouad Saleem Ahmed al Hareez al Mahri (29) mfanyakazi wa kikosi cha Zimamoto na Saeed Abdulla Saad (28) ambaye ni askari polisi wa kitengo cha usalama barabarani, pamoja na raia wa Saudi Arabia, Al-Mahri Saeed Mohseens (29) waliachiwa huru baada ya kubainika kuwa hawakuwakupatikana na kosa la kuwafungulia mashitaka.

Tukio la kurushwa kwa bomu hilo lilisababisha mauaji ya watu watatu na wengine zaidi ya 67 kujeruhiwa.



CHANZO: NIPASHE
Next Post Previous Post
Bukobawadau