Bukobawadau

Kibanda ni nani Wasira ni nani Na Prudence Karugendo

WIKI kadhaa zilizopita ilitolewa kauli Bungeni iliyokuwa imejaa kebehi na kejeli dhidi ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Absalom Kibanda, ikiuliza “kwani Kibanda ni nani?”. Kauli hiyo ilikuja kutokana na dukuduku lililokuwa limetanda kufuatia kutekwa na kusulubiwa kinyama kwa mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Wahariri na watu wasiojulikana.

Sio lengo la makala haya kufanya kazi ya ukachero wa kubaini nani atakuwa amehusika na unyama huo ambao umeanza kuota sugu hapa nchini, hiyo kazi tunaviachia vyombo husika mpaka hapo vitakapotuhakikishia bila shaka yoyote kuwa vimeshindwa kuifanya kazi hiyo.

Hapa nataka nijihusishe tu na kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Steven Wasira, aliyoitoa Bungeni akiuliza kwa kebehi kwamba kwani Kibanda ni nani?

Nafanya hivyo kwa sababu kauli tata za aina hiyo zikiachiwa zipite bila kujadiliwa ni rahisi kuwapotosha wananchi na kuwafanya wajigawe wenyewe kwenye matabaka, na ikizingatiwa kwamba kauli ya aina hiyo inatolewa na mtu anayetambulika kama waziri tena akiitolea ndani ya Bunge, jumba ambalo ni kwa ajili ya wawakilishi wa wananchi kuikagulia serikali na utendaji wake.

Kwahiyo mada iliyo hapa ni kauli ya kibaguzi iliyotolewa na Wasira Bungeni, “Kwani Kibanda ni nani?”

Nasema kwamba ni kauli ya kibaguzi kwa vile naifananisha na kauli ya msemaji wa serikali ya makaburu, James T. Kruger, ya “Who is Steve Biko after all” pale mwanaharakati mzalendo wa Afrika Kusini, Steven Bantu Biko, alipopoteza maisha yake akiwa mikononi mwa polisi wa makaburu.

Kauli ya Wasira dhidi ya Kibanda, kama ilivyokuwa kauli ya Kruger dhidi ya Biko, ilikuwa ni kauli dhidi ya Watanzania wote wanyonge. Maana ni kauli ya kutaka kuushusha hadhi utu wa Kibanda ili aonekane ni kiube dhalili aliyepaswa kufanyiwa lolote, kama ilivyotokea, bila ya yeyote kuhoji kulikoni, “Kwani kibanda ni nani?”

Kwa maana hiyo Kibanda alistahili kutekwa, kutobolewa jicho, kunyofolewa kucha na kukatwa kidole, kwa vile hajulikani yeye ni nani!

Ni jambo la kushangaza na kusikitisha kuona kauli kama hiyo ya kinyama inatolewa mbele ya wawakilishi wa wananchi nao wanaridhika nayo na kumwachia Wasira aendelee na majigambo yake bila kumshika shati. Kwahiyo Wasira akaendelea mpaka akamaliza akiwa amewaaminisha wawakilishi wa wananchi kuwa Kibanda si lolote si chochote.

Kwa mshangao wa kila mwananchi wawakilishi hao wakatulia tuli, kama alama ya kuonyesha kwamba wamekubaliana na Wasira wakiwa wamesahau dhima yao ya kuwa pale Bungeni.

Pamoja na yote wanayotakiwa kuyafanya wabunge kama wawakilishi wa wananchi, la kwanza na muhimu kuliko yote ni kuhakikisha usalama wa wananchi wanaowawakilisha na haki yao ya kuishi vinapewa kipaumbele. Mengine yote yanafuatia. Sababu huwezi kuwafanyia wananchi lolote linaloonenakana la manufaa kwao kama hawaishi na au kuwa salama.

Mwananchi hawezi kutobolewa macho, akang’olewa meno, akanyofolewa kucha na kufanyiwa unyama wa kila aina wewe ukadai hiyo sio kitu ila cha muhimu ajengewe barabara ya lami na kupatiwa umeme nakadhalika nakadhalika! Sidhani kama uwakilishi wa wananchi unaweza ukaeleweka kwa mtindo huo.

Ndiyo maana sikuwategemea wabunge wamwachie Wasira bila kumsulubu baada ya kauli yake hiyo ya ajabu dhidi ya Mtanzania mwenzake.

Kauli ya “kwani Kibanda ni nani” inaturudisha kwenye riwaya ya Shamba la wanyama ambapo viongozi baada ya kunogewa na kulewa uongozi na madaraka wakaanza mbinu za kukiuka misingi ya usawa waliyojiwekea kwenye katiba yao. Wakati katiba yao ilikuwa ikisisitiza kuwa wanyama wote ni sawa, viongozi wakaongeza kuwa lakini baadhi ni sawa kuliko wengine! “All animals are equal but some are more equal than others”.

Kwa mantiki hiyo basi Wasira anajiona sawa kuliko Kibanda! Sijui katika lipi! Ni mwananchi gani anayeuona umuhimu wa Wasira uliotukuka kuliko umuhimu wa Kibanda? Kama yupo ningeomba anieleweshe huo umuhimu wa Wasira nami nipate kuufahamu.

Hebu tumwangalie Kibanda ni nani, pengine itamsaidia Wasira, kama kweli kauli hiyo ilikuwa ya kupitiwa, kusudi huko mbele aweze kupangilia kauli zake kiumakini ili zisiendelee kuleta mkanganyiko kwa wananchi. Na kama alifanya hivyo kwa makusudi katika kuwaonyesha wananchi kuwa wanaishi katika matabaka ya wanaojaliwa usalama na uhai wao na wasiojaliwa, basi aelewe kwamba wananchi hawakuipenda kauli hiyo na yeye hafai kuendelea kuwemo kwenye serikali yao inayowaongoza.

Kibanda ni mwananchi mwenye haki zote za uraia kama alivyo yeye Wasira. Wote wawili wana haki sawa ya kuishi na kuhakikishiwa usalama wao. Ila Kibanda ni mwanahabari na mhariri, kazi ya kitaaluma ambayo si kila mtu anaweza kuifanya hata awe msomi. Wasira ni waziri, kazi isiyo na taaluma yoyote, kazi ambayo mtu yeyote mwerevu anaweza kuifanya bila kuhitaji mafunzo ya ziada pale rais anapokuwa amemuhitaji.

Kibanda anahabarisha na kuelimisha umma kwa njia ya maandishi. Kwa maana hiyo umma unamwelewa na kumhitaji. Lakini umuhimu wa kazi ya Wasira anauelewa yule aliyempa kazi hiyo. Sidhani kama Wasira anafanya kazi inayowagusa moja kwa moja wananchi. Sababu rais anaweza akabadilisha na kumweka mtu mwingine kwenye nafasi hiyo ya Wasira wala watu wasijue kama kuna mabadiliko yaliyofanyika. Hiyo ni kwa sababu anachokifanya Wasira kwenye ofisi ya rais hawakijui wala hawakioni.

Lakini Kibanda alipobadilisha ofisi kutoka Freemedia kwenda Newhabari kila mtu anayejua kusoma aliyaelewa mabadiliko hayo, hiyo ni kwa sababu anachokifanya Kibanda kinawagusa wananchi.

Sasa iweje leo hii Wasira atuulize Kibanda ni nani? Si ajabu kwamba kuna baadhi ya wananchi hawajawahi hata kulisikia jina la Wasira. Mzee mmoja kanitumia ujumbe mfupi wa maadishi, ambao ndio kiini cha makala haya, akiuliza hivi huyu Wasira anayehoji Kibanda ni nani yeye nini nani, ni Mtanzania huyu?

Kama ni kweli, mzee huyo anasema ndiyo mara yake ya kwanza kusikia jina hilo la WAsira! Lakini pamoja na kwamba wapo wanaomchukulia hivyo Wasira, yeye bado anajiona ni “sawa kuliko wengine”! Ni Mtanzania bora kuliko Watanzania wengine, mwenye haki sawa kuliko ya wengine, mwenye thamani sawa kuliko wengine, “some are more equal than others”!

Hiyo inatoa picha ya kwamba Watanzania, ambao tangu uhuru hawakuzizoea kauli za kibaguzi, kwa sasa wamefikishwa ambapo wanalazimishwa kuzizoea kauli hizo za kibaguzi wanataka wasitake. Ni jambo la kusikitisha na kushangaza lakini hawana jinsi, pengine wajipange upya baada ya kuangalia na kupagundua mahali ambapo mambo yameenda tenge.

Kwahiyo kama kauli hiyo ilimtoka Waziri Wasira kwa jazba akidhani analikomoa kundi fulani la watu, pengine katika mtindo ule wa zamani uliotumika enzi za kikoloni, gawanya utawale, aelewe kwamba amewakwaza Watanzania wote katika ujumla wao. Maana Watanzania wanaamini kwamba wao ni kitu kimoja, hakuna Wasira aliye bora wala Kibanda hasiyethaminika kiasi cha kuulizwa yeye ni nani.

Labda kama inawezekana, Wasira atengeneze kauli nyingine ya kuisafisha kauli yake ya mwanzo iliyowachefua wananchi sambamba na kumuomba radhi Kibanda. Kwa njia hiyo atakuwa amemriwadha Kibanda hata kama kwa kufanya hivyo hatakuwa amemuondolea uremavu wake wa kudumu alioupata ukubwani kutoka kwa watu wenye roho za kinyama.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau