Bukobawadau

KUTOKA KWA MBUNGE WA NZEGA; Dr. Hamisi Kigwangalla; Kuanguka kwa Nidhamu na Maadili Kutasababisha Kuanguka kwa Taifa!

Leo nimependa kuchangia kidogo tu kuhusu nidhamu na umuhimu wake katika kuleta maendeleo ya Taifa lolote lile, ama ya taasisi yoyote ile, ama ya mtu yeyote yule. Nidhamu ninayoiongelea hapa ni ile inayohusiana na kuheshimu misingi yote ya maadili, misingi ya kazi na ya maisha; kuheshimu kanuni na sheria zilizowekwa na kufuata maelekezo yaliyopo. Kufanya hivyo kunasadikiwa kuwa ni njia ya kistaarabu. Ni njia ambayo watu waliostaarabika wanaifuata ili kujiletea maendeleo na ili kuishi kwa amani na watu wengine, na mazingira yanayowazunguka.


Maadili ni msingi mkubwa sana wa kuleta maendeleo ya watu. Maadili ni dhana inayowataka watu kuheshimu misingi ya sheria, kanuni na taratibu ili kuweza kuishi kwa amani na usawa na baioanuwai nyingine. Maadili ni kujua kipi sahihi na kipi si sahihi. Hivyo kuwa na maadili ni kuhakikisha unafanya kila kitu kwa kufuata misingi ya kutazama uhalisia wa uhalali wa mambo kiusahihi wake. Usahihi unachimbua msingi wake kwenye fikra kwamba haya ni yale mambo ambayo watu wengi wenye akili timamu na bila kulazimishwa wamekubaliana kwa pamoja kwamba hili litakuwa hivi, na lile litakuwa vile na hivyo kulifanya liwe ada.


Misingi hii mikubwa miwili isipoangaliwa na kulindwa inaweza kupelekea Taifa kuchelewa kuendelea mbele ama kuanguka tu. Kwa sababu bila kuwa na nidhamu na maadili watu watajifanyia mambo wanayoona wao yanafaa hata kama hayakubaliwi na watu wengi wenye akili timamu. Kwa mfano leo hii tuna tatizo la rushwa, jambo ambalo halaikubaliki kwenye jamii yoyote ile ya wastaarabu – hii ikikithiri tu inatuvuruga sana, tunaona leo hii rushwa kubwa ilivyosaidia kuwapa ajenda wapinzani wa Chama Cha Mapinduzi, jambo ambalo limepelekea kuondoa imani ya wananchi dhidi ya watawala. Imani ya wananchi inavyozidi kupungua dhidi ya watawala inasababisha migomo na maandamano na hata uasi kwenye baadhi ya nchi – mambo ambayo yanadumaza maendeleo ya Taifa na mahala pengine yameweza kuangusha dola. Ni mtu asiye na maadili tu anayeweza kuchukua rushwa na kuminya haki ya wengine. Mfano mamilioni ya pesa yaliyopotea kutokana na rushwa kusababisha mikataba ya hovyo ya madini kusainiwa


yamesababisha serikali kukosa kodi ambayo ingetusaidia kukuza uchumi wetu kwa kujenga miundombinu na pia kuboresha huduma za jamii.


Dr. Hamisi Kigwangalla, MD, MPH, MBA
Next Post Previous Post
Bukobawadau